BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

VIGOGO NDANI YA SERIKALI YA RAIS MAGUFULI WAKUMBWA NA HOFU BAADA YA CAG KUJITINGISHA KIDOGO


CAG sasa aibua hofu mpya vigogo ufisadi

KUNA taarifa kuwa hofu mpya imeibuka kwa baadhi ya vigogo na watu wengine mbalimbali waliotumia nafasi zao kufanikisha ‘dili’ haramu za kifisadi zilizowaingizia mabilioni ya fedha kwa manufaa yao binafsi.


Inaelezwa kuwa hali hiyo inatokana na dondoo alizozigusia Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad, kuhusiana na kile kilichomo katika taarifa yake ijayo ya ukaguzi kwa mwaka wa fedha wa 2015/2016.

Mwishoni mwa wiki, Prof. Assad aliyekuwa pamoja na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Valentino Mlowola, alikaririwa akisema kupitia kituo cha runinga kuwa kuna maeneo katika ripoti ijayo “yatashtua” na pengine kuwafikisha baadhi ya vigogo kortini baada ya taasisi za uchunguzi wa masuala hayo kukamilisha kazi yake.

Prof. Assad na Mlowola walikuwa wakizungumzia wiki ya kampeni ya mwezi mmoja kuelekea siku ya maadili na haki za binadamu itakayoadhimishwa Desemba 10.

Hata hivyo, Prof. Assad hakuwa tayari kueleza kiundani juu ya mambo hayo “yatakayoshtua” katika taarifa yake ijayo ambayo chanzo kimoja kimeiambia Nipashe kuwa itatolewa rasmi mwakani, kati ya Machi 26 na 28.

Akiwasiliana na Nipashe jana, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano katika Ofisi ya CAG, Sarah Ruben hakuwa tayari kufafanua zaidi juu ya taarifa iliyogusiwa na bosi wao, Prof. Assad, akisema kuwa jana (Jumamosi) ni siku ya sabato kwake na hivyo asubiri.

Hata hivyo, vyanzo mbalimbali viliiambia Nipashe kuwa baadhi ya mambo yatakayoshtua katika taarifa ijayo ya CAG ni pamoja na suala la mishahara hewa; wanafunzi hewa wa msingi na sekondari; mikopo hewa kwa wanafunzi wa elimu ya juu; miradi hewa ya maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini; mikataba ya utata katika halmashauri mbalimbali na pia sakata lililotikisa kwa miezi kadhaa sasa la tuuhuma za ulaji wa mkataba wa kampuni ya Lugumi na Jeshi la Polisi.

“Kama CAG alivyogusia, ni kweli taarifa ijayo ya ukaguzi itashitua sana kwa sababu itawaumbua wengi wanaojihusisha na vitendo vyenye ishara ya ufisadi,” chanzo kimojawapo kiliiambia Nipashe.

“Na hii Mahakama ya Ufisadi iliyoanza kupokea mashauri ndiyo inayoongeza hofu mpya kwa vigogo wengi kwa sababu hivi sasa hakuna tena kulindana… wahusika wanajua kuwa wakikuitwa na hatia wataozea jela na kufilisiwa. Kwa ufupi hali ni tete,” chanzo kingine kilisema na kuongeza:

“Huu msukumo wa Mkuu (Rais Magufuli) katika kupambana na rushwa na ufisadi ndiyo utakaowaponza wengi. Wale waliojihusisha na ulaji kama wa mishahara hewa na mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu hawana raha hata kidogo kwa sababu Magufuli ameapa kuwa nchi imeshaliwa sana na sasa basi, na vyombo vya uchunguzi havina tena muda wa kumlinda mtu.”

HOFU ZAIDI
Akizungumzia kasi zaidi waliyo nayo katika kuandaa taarifa za ukaguzi, Prof. Assad alisema hivi sasa wanapata moyo zaidi wa kufanya kazi kwa nguvu baada ya kuona kuwa serikali imeonyesha dhamira ya dhati ya kupambana na ufisadi.

Akizungumzia kile alichokieleza Prof. Assad, Mkurugenzi wa Takukuru, Mlowola, alisema wao wanasubiri ripoti hiyo (2015/2016) ya CAG ili waifanyie kazi. Alisema pia wanashirikiana na ofisi ya manunuzi ya umma (PPRA) kwa sababu nako kuna maeneo kadhaa yenye viashiria vya ufisadi.

Aidha, katika kile kinachoonyesha kwamba hata waliotajwa kwenye ripoti za CAG zilizotangulia hawako salama, hotuba ya Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa, ya kuahirisha mkutano wa tano wa Bunge la 11, imedhihirisha kuwa wahusika wa vitendo vya ufisadi wako katika wakati mgumu.

“Katika mkutano huu, wabunge wamepata fursa ya kujadili Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na Taarifa za Kamati za Kudumu za Bunge za PAC na LAAC kuhusu Hesabu za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Serikali za Mitaa zilizokaguliwa kwa mwaka ulioishia tarehe 30 Juni, 2014 na tarehe 30 Juni, 2015.

“Serikali imepokea michango na Hoja za Waheshimiwa Wabunge na itazifanyia kazi,” ilisema sehemu ya hotuba ya Majaliwa.

TUHUMA ULAJI LUGUMI
Kati ya hoja zilizotarajiwa kuwasilishwa na PAC kwenye mkutano wa tano wa Bunge la 11 na kuahirishwa na sasa inatarajiwa kuwapo tena kwenye ripoti ijayo ya CAG ni sakata la Mkataba wa Kumpuni ya Lugumi Enterprises Limited.

Mkataba huo unaotajwa kuwa ni wa Sh. bilioni 37 kati ya kampuni hiyo na jeshi la Polisi ulilenga kufungwa kwa vifaa maalumu vya utambuzi wa alama za vidole kwenye vituo vya polisi, umeonekana kuwa moto lakini katika ripoti ijayo ya CAG, unatarajiwa kuwapo tena baada ya kutojadiliwa katika mkutano ulihitimishwa Ijumaa.

WANAFUNZI HEWA MSINGI, SEKONDARI
Hili ni eneo jingine linalotajwa kuwa litawaliza vigogo wengi waliojinufaisha kwa kuwasilisha orodha ya kughushi ya idadi ya wanafunzi na kutwaa fedha za ziada zinazotolewaa na Serikali kila mwezi kugharimia utoaji wa elimu bure.

Hivi karibuni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene, aliwaambia waandishi wa habari kuwa, serikali imefanikiwa kuokoa Sh. milioni 931.31 baada ya kubaini wanafunzi ‘hewa’ katika shule za msingi na sekondari nchini.

Alisema kiasi hicho kimeokolewa baada ya kufanyika uhakiki na kubaini kuwapo wanafunzi ‘hewa’ 52,783 wa shule za msingi na sekondari walipatikana 12,415.

“Idadi ya wanafunzi kabla ya uhakiki huo Machi mwaka huu, kulikuwapo na wanafunzi 9,746,534 wa shule za msingi na 1,483,872 wa sekondari, lakini baada ya uhakiki huo, ilibainika kuwapo wanafunzi wa shule za msingi 9,690,038 na sekondari 1,429,314,” alisema Simbachawene.

MIKOPO HEWA ELIMU YA JUU
Mikopo hewa pia iantajwa kuwapa hofu kubwa wanufaika ambao ripoti ijayo ya CAG haitawaacha. Kuna upotevu mkubwa wa fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.

Tangu Juni, Serikali imekuwa ikipambana na suala hilo na ilipofika Agasiti, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, alisema serikali imebaini kwamba Sh. bilioni 3.85 zililipwa kwa wanafunzi hewa 2,192 kwa kipindi cha mwaka 2015/16.

Kiasi hicho cha fedha kiligundulika kulipwa wanafunzi hewa katika vyuo 29 kati ya 31 vilivyokaguliwa, alisema
Alisema mbali na fedha hizo, baada ya serikali kutangaza kuanza uchunguzi wa wanafunzi hewa wanaopata mikopo, baadhi ya vyuo vilirejesha Sh. bilioni 2.6 kimiakimia ambazo zilikuwa zimetolewa kwa ajili ya mikopo kwa wanafunzi mbalimbali.

MISHAHARA HEWA
Tangu serikali ya Rais John Magufuli kuanza kupambana na watumishi hewa, imeelezwa kwamba kwa sasa serikali inaokoa zaidi ya Sh bilioni 16 zilizokuwa zinalipwa kwa watumishi hao.

Hata hivyo ni wazi kwamba, ripoti ya CAG itatoa picha halisi ya hali ilivyo na kama tatizo hilo limepungua kwa kiasi gani.

Oparesheni ya kupamba na watumishi hewa, ilifanya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anna Kilango, kuwa mkuu wa mkoa wa kwanza kwenye serikali ya Rais Magufuli kufukuzwa kazi kwa kutoa taarifa zisizo sahihi.

MIRADI HEWA YA MAENDELEO
Eneo jingine linalowapa hofu baadhi ya viongozi na watumishi wa umma wasio waaminifu ni utekelezaji wa miradi mbalimbali ambayo kwenye ripoti zilizopita, ilibainika kuwapo na miradi hewa ambayo imekuwa ikitafuna mabilioni ya fedha. 


Ili kuhakikisha asilimia 40 ya bajeti ya serikali ya mwaka 2016/17, iliyotengwa kwa shughuli za maendeleo inafanya kazi, ni dhairi watakaobainika kufuja fedha kwenye ripoti iyayo ajira zao zitakuwa shakani.Nipashe
Share on Google Plus

About Juma Mtanda

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
Post a Comment