BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MAHAKAMANI: MBUNGE WA ARUSHA MJINI GODBLESS LEMA KULA KRISMASI NA MWAKA MPYA GEREZANI KUU LA KISONGO

Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, imetupilia mbali rufaa ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) ya kuomba dhamana yake na hatimaye kurudishwa katika Gereza la Kisongo jijini hapa.

Atakuwa katika mahabusu ya gereza hilo hadi Februari 2 mwakani atakaporejeshwa mahakamani kusikiliza kesi yake ya msingi. Hii ina maana kwamba, sikukuu zote za mwisho wa mwaka, yaani Krismasi na Mwaka Mpya zitamkuta mbunge huyo akiwa mahabusu.

Mbunge huyo anashikiliwa kwa mwezi mmoja sasa katika Gereza Kuu Kisongo, baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha kufutilia mbali rufaa yake.

Akisoma uamuzi mdogo wa Jaji Fatuma Masengi, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Angelo Rumisha, alisema Mahakama imeifuta rufaa hiyo kutokana na wakata rufaa kufanya hivyo nje ya muda.

Rumisha alisema waomba rufaa walitakiwa kuonesha kusudio la kukata rufaa ndani ya siku 10 tangu maamuzi ya maombi ya marejeo kutupwa na Mahakama Kuu, yaliyokuwa mbele ya Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Sekela Moshi, Novemba 11 mwaka huu.

“Hivyo Mwomba rufaa hii (Lema) kupitia Mawakili wake alitakiwa kuonesha kusudio au kutoa notisi kuonesha Mahakama sababu ya kukata rufaa na Novemba 21 walipaswa kukata rufaa, lakini wao walikata Novemba 22 nje ya muda wa kukata rufaa,” alisema.

Alisema kutokana na hali hiyo, Mahakama imekubaliana na upande wa pingamizi lililowekwa na upande wa Serikali kupitia Wakili Paul Kadushi akishirikiana na Martenus Marandu kuwa rufaa hiyo haikufuata misingi ya kisheria kuikata sababu hakuna kusudio la kukata rufaa na kuiomba Mahakama hiyo itupilie mbali rufaa hiyo.

Rumisha alisema baada ya pingamizi hilo kutolewa na upande wa Lema kuomba Mahakama ilitupilie mbali pingamizi hilo, kwani rufaa yao ipo ndani ya muda na imewasilishwa kwa hati ya dharura, Mahakama ilivyopitia hoja za pande zote mbili imeona rufaa hiyo imeletwa Mahakamani hapo nje ya muda unaotakiwa.Kesi ya msingi imepangwa kusikilizwa Februari 2, mwakani.

Aidha alisema mbali na nje ya muda pia wakata rufaa hawakuzingatia sheria inavyotaka kuwa ukikata rufaa lazima uanze na kutoa siku 10 za kusudio la kukata rufaa, na hivyo kuifutilia mbali rufaa hiyo.

Baada ya uamuzi huo wa Msajili Rumisha, Wakili wa Lema Adam Jabir, aliomba Mahakama hiyo itoe angalizo kwa askari wanaokwenda Mahakamani hapo kuweka ulinzi, kwani wanawazuia lakini pia raia wanawake wanapekuliwa na askari wanaume.

Alisema mteja wao (Lema) anasikitika kuona hali hiyo ikijitokeza wakati yeye ni Mbunge na kesi inasikilizwa chumba cha wazi ili kila mmoja asikilize na kufahamu kinachoendelea.

Akijibu hoja hiyo, Msajili Rumisha alisema Mahakama ikiruhusu watu wote wanaokuja katika kesi hiyo kuingia kutakuwa na uhaba wa sehemu za kukaa, kwa vile chumba ni kidogo na ndio sababu watu wanadhibitiwa.

Nje ya chumba cha Mahakama Wakili wa Lema, John Mallya aliwaambia waandishi wa habari, kuwa baada ya kuzungumza naye, Mbunge huyo aliwaomba kutojishughulisha na suala lolote la kukata rufaa, ingawa wao kama mawakili wanaona bado kuna njia za kufanya hivyo katika Mahakama za juu.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: