RAIS MAGUFULI AKUBALI BILA KINYONGO KUSTAAFU KWA MKUU WA JESHI LA MAGEREZA TANZANIA
Aliyekuwa Kamishna Jenerali wa Magereza, John Minja
RAIS John Magufuli amekubali na kuridhia ombi la kusitisha mkataba na kustaafu kwa Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini Kamishna Jenerali wa Magereza, John Minja.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu jijini Dar es Salaam jana ilisema mkataba huo ulisitishwa kuanzia jana.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais Magufuli amempongeza Kamishna Jenerali wa Magereza mstaafu Minja kwa utumishi wake na amemtakia maisha mema ya kustaafu.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amemteua Kamishna wa Magereza, Dk Juma Malewa kuwa Kaimu Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini hadi hapo uteuzi wa Kamishna Jenerali wa Magereza utakapofanyika.
Hatua hiyo imekuja ikiwa zimepita siku chache baada ya Rais Magufuli kufanya ziara ya kushtukiza katika Gereza la Ukonga jijini Dar es Salaam.
Akiwa gerezani hapo pamoja na mambo mengine Rais Magufuli alipiga marufuku uuzwaji wa sare za majeshi nchini na watu binafsi na kutaka wale wote wanaouza sare hizo wazikabidhi kwa majeshi husika mara moja.
Baada ya ziara hiyo Ikulu ilisema kwamba Rais Magufuli amepiga marufuku hiyo kutokana na maelezo kutoka kwa baadhi ya askari wa Jeshi la Magereza kwamba wamekuwa wakinunua sare za jeshi hilo kutoka kwa watu binafsi, kinyume cha taratibu za majeshi nchini.
Rais Magufuli alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuwachukulia hatua mara moja wale wote watakaobainika kuuza sare za majeshi ya nchini.
Hali kadhalika Rais Magufuli alipiga marufuku kwa majeshi yote nchini kuingia ubia na watu binafsi kupangisha ama kuuza maeneo yao kwa ajili ya kufanya biashara na kutaka maeneo yote ya majeshi yabaki katika jeshi husika.
“Haiwezekani sare za majeshi yetu hapa nchini kuuzwa na watu binafsi hilo haliwezekani kamwe labda baada ya kumaliza muda wangu,” alisema Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli alitoa Sh bilioni 10 kwa Jeshi la Magereza kwa ajili ya kujenga nyumba mpya zitakazotumika kwa ajili ya makazi ya askari wa Jeshi la Magereza katika Gereza la Ukonga jijini Dar es Salaam.
Hatua hiyo ilitokana na kilio cha askari Magereza kuwa wengi wao wamekuwa wakiishi uraiani kitu ambacho ni tofauti na taratibu za majeshi nchini na hata kuzorotesha utendaji kazi wa askari wa jeshi hilo.
0 comments:
Post a Comment