BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

POLISI MORO YAVUTWA KOTI NA COASTAL UNION MOROGORO

Mshambuliaji wa Coastal Union, Michael Minda akijaribu kumiliki mpira dhidi ya mlinzi wa Polisi Moro, Abdulraham Hija wakati wa ligi daraja la kwanza Tanzania bara mzunguko wa pili uliofanyika kwenye uwanja wa jamhuri Morogoro na kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Juma Mtanda, Morogoro.

Klabu ya Polisi Moro SC imevutwa sharti na kulazishwa sare dhidi ya Coastal Union (Wagosi wa Kaya) katika mchezo mkali uliojaa ushindani ligi daraja la kwanza Tanzania bara mzunguko wa pili kufuatia kumalizika kwa sare ya bao 1-1 uliopigwa kwenye uwanja wa jamhuri mkoani Morogoro.

Mshambuliaji wa Polisi Moro, Ramadhan Kapera (Pires) wa ndiye aliyeanza kuipatia timu yake bao dakika ya pili kwa njia ya mkwaju wa penalti baada ya mlinzi wa Coastal, Anderson Solomon kuunawa mpira eneo la hatari na mwamuzi wa mchezo huo, Dominic Nyamsana kutoka Dodoma kutoa adhabu hiyo.

Coastal Union ilipata bao la kusawazisha dakika ya 78 lililofungwa na Said Seleman kwa kichwa baada ya mpira wa adhabu ndogo uliochongwa na Mustafa Athuman kufuatia Michael Minda kufanyiwa madhambi na mlinzi wa Polisi Moro, Abdulhaman Haji na shuti lake kupanguliwa na kipa Benjamin Haule kabla ya kumkuta mfungaji.

Akizungumzia mchezo huo na mwandishi wa MTANDA BLOG, Kocha Msaidizi wa Polisi Moro, John Tamba alieleza kuwa mchezo huo ulikuwa mgumu hali iliyopelekea kugawana pointi.

Tamba alisema kuwa lengo lao ni kuondoka na pointi tatu lakini kutokana na ushindani wa mchezo huo Coastal hawakuwa tayari kupoteza mchezo huo kwani katika mchezo wa kwanza Polisi Moro waliibuka na ushindi wa bao 2-0 kwenye uwanja wa Mkwakwani.

“Coastal ni wazuri na wamebadilika tofauti na mchezo wa kwanza, tumepata bao la mapema na tumekosa nafasi nyingi za wazi za kufunga lakini mchezo wa soka ndio ulivyo, leo unaweza kufanya vibaya na kasha ukafanya vizuri hivyo tunajipanga na mchezo huo dhidi ya Njombe Mjini kwao.”alisema Tamba.

Kwa upande wa Kocha mkuu wa Coastal Union, Mohamed Kampira alieleza kuwa pointi moja waliyoipata mbele ya Polisi Moro haijawakatisha tamaa na akili wanaelekea kwenye mchezo mwingine dhidi ya Kimondo FC uwanja wa Mkwakwani.

Kampira alieleza kuwa katika mchezo na Kimondo wanajipanga ili kuibuka na ushindi na kuongeza idadi ya pointi ya sasa ya pointi sita.

“Tumecheza vizuri na tumefanikiwa kusawazisha bao, timu bado nzuri na tunaelekeza akili kwenye mchezo dhidi ya Kimondo FC jumamosi hii na baada ya hapo hesabu zetu zitakaa sawa”alisema Kampira.

Coastal Union iliyopewa adhabu ya michezo mitatu na shirikisho la soka Tanzania (TFF) italazimika, michezo miwili kucheza bila mashabiki wake huku mchezo mmoja wakilazimika kucheza nje ya uwanja wa Mkwakwani.

Adhabu hiyo inatokana na kuadhibiwa na TFF kufuatia vurugu zilizojitokeza kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza baada ya mashabiki wa timu hiyo kumshambulia mwamuzi wa kati baina ya timu yao na KMC Fc uliofanyika Mkwakwani na kupoteza.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: