
Beki wa kulia wa Azam FC, Shomari Kapombe (kushoto) wakiwania mpira na mchezaji wa African Lyon, Omary Salum wakati wa mechi ya Ligi Kuu Bara iliyofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam jana. Timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana.
SIMBA jana ilirudi kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu bara baada ya kuifunga Ndanda mabao 2-0 katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona Mtwara.
Tangu kuanza kwa Ligi Kuu msimu huu, Simba imekuwa kileleni mwa msimamo kabla ya juzi kushushwa kwa muda na mtani wake Yanga iliyoifunga JKT Ruvu mabao 3-0. Simba sasa imefikisha pointi 38 na Yanga 36.
Matokeo ya mechi ya jana yamerudisha matumaini Simba kwani ilimaliza mzunguko wa kwanza vibaya baada ya kupoteza mechi ya mwisho kwa kufungwa mabao 2-1 na Prisons.
Iliilazimu Simba kusubiri mpaka dakika ya 63 kuandika bao la kuongoza lililofungwa na Muzamil Yassin kwa shuti kali akiunganisha pasi ya Mohamed ‘Mo’ Ibrahim.
Yassin aliingia uwanjani dakika ya 19 kuchukua nafasi ya mchezaji mpya wa Simba, Mghana James Kotei aliyeumia baada ya kugongana na Kiggi Makasi wa Ndanda. Bao hilo liliibadilisha Ndanda ambayo sasa wachezaji wake walionekana kuchanganyana, hali iliyowafanya kuruhusu mashambulizi ya mara kwa mara langoni mwao.
Mo aliihakikishia Simba kuondoka na pointi baada ya kufunga bao la pili katika dakika ya 81 akimalizia kazi nzuri ya Yassin. Katika uwanja wa Uhuru Dar es Salaam, African Lyon ilitoka sare ya bila kufungana na Azam FC, huku Mbao FC ikiifunga Stand United bao 1-0.
Bao la Mbao lilifungwa na Jamal Mwambeleko aliyeunganisha vyema pasi ya Rajesh Kotecha dakika ya 56. Kwenye uwanja wa Sokoine Mbeya, Prisons iliifunga Majimaji bao 1-0.
Kikosi cha Simba jana: Daniel Agyei, Janvier Bokungu, Mohammed Hussein/Abdi Banda, Method Mwanjali, Jonas Mkude, Shiza Kichuya, James Kotei/Muzamil Yassin, Frederic Blagnon/ Laudit Mavugo, Ibrahim Ajib/Said Ndemla na Mohammed ‘Mo’ Ibrahim.
Kikosi cha Ndanda: Jeremiah Kisubi, Kiggi Makassy, Bakari Mtama, Paul Ngalema, Hemed Khoja/Benito John, Salvatory Ntebe, Nassor Kapama, Salum Minelly, Salum Telela, Omar Mponda/Helbert Lukindo na Riffat Khamisi.

0 comments:
Post a Comment