BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

RAIS MAGUFULI AWA KIBURI WAMACHINGA

WAFANYABIASHARA ndogo maarufu Machinga katika Jiji la Mwanza, jana walilipuka kwa furaha huku wakizunguka mitaa ya katikati ya jiji, wakiimba nyimbo za kumsifu Rais John Magufuli huku wakimtakia afya na maisha mema kwenye uongozi.

Walifanya hivyo baada ya kutoa agizo la machinga hao na wa mikoa mingine, kutoondolewa katika maeneo hayo hadi pale mamlaka husika zitakapokamilisha maandalizi ya maeneo watakapohamishiwa kwa kuwashirikisha machinga wenyewe.

“Rais, Rais, Rais….tunakutakia maisha marefu uendelee kutuongoza Watanzania wanyonge 2020 tutakupa kura zote,” walisikika machinga hao jana alasiri baada ya kupata taarifa za uamuzi huo alioutoa Rais Magufuli akiwa Ikulu, Dar es Salaam.

Machinga Haruna Wambura ambaye ni mkazi wa Mji Mwema, alisema Rais Magufuli amefanya jambo jema la kuwarudisha katikati ya mji ambako watafanya biashara zao na kujiongezea kipato.

Dorica Mbisire wa Mahina Tambukareli ambaye pia ni machinga, aliupongeza uamuzi uliochukuliwa na Rais John Magufuli wa kuwarudisha mjini kuendelea na biashara zao. “Rais adumu milele na mwaka 2020 tutampa kura zote,” alieleza mwanadada huyo.

Aidha, gazeti hili liliwashuhudia baadhi ya machinga katika maeneo ya Makoroboi, wakianza kujigawia maeneo kwa kuweka alama na wengine wakichimba mashimo tayari kwa kurudisha vibanda vyao.

Katika uamuzi wake jana Ikulu, Rais Magufuli alimuagiza Waziri na Katibu Mkuu katika Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kusitisha mara moja utekelezaji wa kazi ya kuwaondoa machinga katika Jiji la Mwanza pamoja na mikoa mingine mpaka hapo mamlaka husika zitakapokamilisha maandalizi ya maeneo watakapohamishiwa na kwa kuwashirikisha machinga wenyewe.

Akiwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Rais Magufuli ameonya kuwa kiongozi yeyote ambaye hayupo tayari kutekeleza agizo hilo aachie ngazi.

“Kumeibuka tabia ya wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi kuwafukuza machinga bila utaratibu wowote wa wapi wanawapeleka na wakati mwingine wanapelekwa maeneo ya mbali ambayo hayafai hata kwa kufanya biashara, wakati mwingine wanawafukuza wachimbaji wadogo kwenye maeneo wanayofanya shughuli zao na pia wanawafukuza wafugaji katika maeneo wanayolisha mifugo yao, hili sio sawa.

“Sipendi wamachinga wafanye biashara kwenye hifadhi ya barabara, lakini hakuna sheria katika nchi hii inayosema mtu wa biashara ndogo au machinga hatakiwi kukaa katikati ya mji, tukianza kwenda kwenye utaratibu wa namna hiyo maana yake tunaanza kutengeneza madaraja ya Watanzania, kwamba kuna Watanzania fulani wa daraja fulani wanapaswa kukaa katikati ya mji na Watanzania wa daraja fulani hawatakiwi kukaa katikati ya mji, huo sio mwelekeo wetu na wala Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ambayo mimi na wewe (Makamu wa Rais) tulipita kuinadi, haisemi tutengeneze madaraja ya watu wanaostahili kukaa mjini na wengine hawastahili kukaa mjini, sasa nimeona hili nilizungumze na nataka kulirudia kwa mara ya mwisho,” alisema Rais Magufuli.

Ameelekeza kuwa machinga waliondolewa katika maeneo yao jijini Mwanza, waachwe waendelee na shughuli zao mpaka hapo Halmashauri ya Jiji la Mwanza itakapokamilisha maandalizi ya mahali watakapohamishiwa na kwa kuwashirikisha machinga wenyewe.

“Narudia na hii ni mara ya mwisho, kawaambieni hata machinga wa Mwanza warudi kwenye maeneo yao mpaka watakapowatengenezea utaratibu mzuri, Kigamboni hapa palikuwa na machinga eneo fulani wamehama vizuri kweli, wakatengenezewa miundo mbinu yao katika soko lao na sasa hivi wanafanya kazi vizuri, na waliwashirikisha viongozi wa machinga, lakini Mwanza imekuwa ni amri tu na wengine wanatumia hata msemo wa Hapa Kazi Tu, mimi sikusema msemo wa Hapa Kazi Tu wa namna hiyo, nadhani mmenielewa,” alisisitiza Rais Magufuli akiwaelekeza Naibu Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo na Katibu Mkuu Tamisemi, Mussa Iyombe.

Wakati huo huo, Rais Magufuli ameagiza Wizara ya Nishati na Madini kusitisha mara moja kuwaondoa wachimbaji wadogo katika Kijiji cha Nyaligongo kilichopo katika Kata ya Mwakitolyo mkoani Shinyanga na badala yake wachimbaji hao waachwe waendelee na shughuli zao, na leseni ya mwekezaji anayedai eneo hilo ni lake, aondolewe.

“Wale waliofukuzwa Shinyanga wabaki palepale, kama ni leseni ya huyo mwekezaji ifutwe, Mheshimiwa Makamu wa Rais fuatilia hili, mweleze Waziri wa Nishati na Madini, waache kufukuza wananchi hovyo hovyo, wale wanapata riziki yao, wanasomesha watoto wao lakini wanafukuzwa tu. “Na hizi ndizo ajira zenyewe, tulisema tunatengeneza ajira, wewe mwekezaji ni mmoja unakwenda kuwafukuza watu 5,000? Haiwezekani na wala haingii akilini,” alisisitiza.

Rais Magufuli amekemea vitendo vya wawekezaji wakubwa kupewa maeneo ambayo wachimbaji wadogo wanaendesha shughuli zao tena kwa mtindo wa kutengeneza nyaraka zinazoonesha mwekezaji husika alipewa eneo hilo kabla ya wachimbaji wadogo na kusisitiza kuwa mchezo huo hautavumiliwa.

Hata hivyo, Rais Magufuli amesema maagizo yake hayana maana kuwa machinga na wachimbaji wadogo waendeshe shughuli zao kwa kuvunja sheria, bali wazingatie sheria na mamlaka zisiwanyanyase watu wanyonge.

Kwa upande wao, wakazi wa Jiji la Mwanza wamekuwa na maoni tofauti juu ya agizo la Rais Magufuli, wengine wakipongeza hatua hiyo na wengine wakitofautiana naye.

Enze Paulo ambaye ni mkazi wa Isamilo, alisema hatua iliyochukuliwa na Rais ya kupinga uamuzi uliofanywa na Mkoa na Halmashauri ya Jiji imeonesha jinsi mamlaka zinavyotumia kodi za wananchi bila utaratibu.

“Hebu kwenye zoezi hili fedha nyingi zimetumika, mgambo walikuwa wanalipwa fedha na askari polisi, lakini ni nani atagharimikia hasara kwa bidhaa za machinga, maana bidhaa zingine zimeharibika,” alihoji Paulo.

David Mgumba anayeishi Kilimahewa aliunga mkono uamuzi uliochukuliwa na Rais Magufuli kwa madai kuwa jiji lilikuwa limepooza kama kuna msiba na kwamba wangezalishwa vibaka na majambazi wengi.

Mkazi wa Mkolani, Fredy Julius alisema Rais amefanya jambo jema kwa madai mwaka 2008 uongozi wa Jiji la Mwanza ulipowafukuza wamachinga mjini, matukio mengi ya uhalifu yaliongezeka kwa kasi.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: