BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

KAMISHNA MSAIDIZI JESHI LA POLISI AELEZA KUUAWA KUPO NJE NJE VITA YA MADAWA YA KULEVYA



WAKATI vita mpya dhidi ya mihadarati ikiendelea, Mkuu wa Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya wa zamani, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi mstaafu Godfrey Nzowa, amesema kampeni hiyo huambatana na hatari ya kuuawa.

Akizungumza na Nipashe jana jijini Dar es Salaam, Nzowa alisema moja ya changamoto kubwa ambazo alikutana nazo akiwa mkuu wa kitengo hicho ni hatari kwa maisha.

Alisema kadri nguvu ya mapambano dhidi ya dawa za kulevya inavyoongezwa, ndivyo changamoto ya mhusika kujiweka kwenye hatari ya "kumalizwa" hujitokeza.

Kamishna Nzowa alisema pamoja na changamoto hiyo, kubwa ambalo litafanikisha vita hiyo ni kumtegemea Mungu na kutohofu vitisho vya mapapa wa biashara ya dawa za kulevya.

“Changamoto kubwa ni namna unavyoongeza nguvu ya mapambano, ndivyo hatari na vitisho kutoka kwa watu hao hujitokeza," alisema Nzowa.

"Unapokamata mateja ‘wabwia unga’ hawa hawana tatizo, lakini kukamata kilo 200 za dawa za kulevya ujue umewagusa watu fulani ambao ndio mapapa wenyewe.

"Unapozungumzia kilo moja maana yake unazungumzia Sh. milioni 90, lakini kilo hiyo hiyo moja kwa nchi za wenzetu inauzwa zaidi ya mara nne ya bei ya hapa nyumbani.

“Kwa hiyo unapopambana naye ujue hupambani na mtu wa kawaida, ujue unapambana na mtu mwenye kila kitu... ana fedha, ana akili, ana silaha tena za kisasa na anaweza kukupa msongo wa mawazo na vitisho.

"Ujue hupambani na mtu mmoja bali genge la wafanyabiashara wa unga,” alisema.

Nzoa alisema genge hilo limekuwa na mbinu tofauti za ufanyaji wa biashara hiyo ikiwa pamoja na kubadili njia pindi wanapogundua kuna kufuatiliwa.

Pia alisema watu hao wana mtandao mkubwa wa kisasa wa mawasiliano ambao hushirikisha baadhi ya watu wasio waaminifu ambao wanaaminika wako kwenye mapambano hayo.

“Watu hawa wana uelewa mkubwa. Wana mawasiliano ya kisasa. Mnapopata taarifa za kuwapo kwa dawa zinazosafirishwa ukanda wetu wa Bahari ya Hindi, wakati mnafuatilia miongoni mwenu unakuta mtu anatuma taarifa kwa wahusika kueleza mbinu na mikakati mnayoifanya.

"Au wanaweza kukuchomea hata wewe bosi wao, bosi amevaa hivi, yuko na gari hili, kwa hiyo suala hili ili ufanikiwe ni kumweka Mungu mbele na kutoogopa vitisho,” alisisitiza.

MBINU NYINGI
Alisema watu hao wana mbinu nyingi za kujificha na hutumia vifungashio vya bidhaa mbalimbali kuficha dawa za kulevya.

“Wanaweza kutumia kifungashio cha majani ya chai, wewe ukafiriki wanasafirisha majani ya chai kumbe ndani yake kuna heroine,” alisema.

Pia alisema ili kufanikisha mapambano dhidi ya genge hilo ni lazima serikali ijiimarishe maeneo yote ikiwa pamoja na kushirikiana na nchi zingine duniani katika mapambano hayo.

“Mtandao huu ni mpana. Huwezi kupambana nchi moja ukafanikiwa. Hawa watu wana mtandao mkubwa duniani kwa hiyo ni lazima kila nchi ishiriki kwenye mapambano hayo,” alisema Nzowa.

Mkoa wa Dar es Salaam uko katika awamu yake ya pili ya vita dhidi ya biashara ya dawa za kulevya.

Baada ya kutaja majina ya wasanii wiki iliyopita, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, katikati ya wiki aliwaita kwenda polisi wafanyabiashara, wanasiasa na viongozi wa dini kulisaidia jeshi hilo.

Katika awamu ya kwanza, Makonda alitaja wasanii na polisi 12 na wiki hii akaongeza 'vigogo' 65.

'Vigogo' hao walitakiwa kwenda Kituo Kikuu cha Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam jana, ingawa baadhi, akiwamo Askofu Josephat Gwajima wa Kanisa la Uzima na Ufufuo, walifika juzi.

Tahadhari ya Nzowa inatolewa siku moja tangu Baraza la Viongozi wa Dini la Kupambana na Dawa za Kulevya, limwombe Rais John Magufuli na mamlaka inayohusika kumwongezea ulinzi Makonda kutokana na vita yake ya mihadarati aliyoanzisha. 


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juzi, Mwenyekiti wa baraza hilo ambaye pia ni Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, alisema vita hiyo inahitaji ulinzi wa kutosha.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: