MKUU wa Majeshi ya Ulinzi mstaafu, Jenerali Davis Mwamunyange amesema jambo kubwa lililomtikisa katika uongozi wake ni milipuko ya mabomu ya jeshi katika kambi zake za Mbagala na Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam iliyosababisha maafa kwa raia.
Aprili 29, 2009 mabomu yalilipuka katika ghala ya silaha la kambi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) namba 671 KJ.
Mabomu hayo yaliyokuwa yakilipuka kwa mfululizo yalisababisha vifo vya watu zaidi ya 20, kujeruhi zaidi ya watu 200 na mamia kadhaa, wengi wao wakiwa ni watoto, kupotea kabla ya kupatikana baada ya kutulia kwa taharuki.
Athari nyingine ilikuwa ni uharibifu wa nyumba na mali.
Kati ya watu waliopoteza maisha katika mkasa huo ni mama mmoja ajulikanaye kwa jina la Sophia Shango, mkazi wa Mbagala Kuu pamoja na mtoto wake. Wote walifyekwa vichwa na moja ya mabomu yaliyokuwa yakifyatuka kutoka kambi hiyo ya jeshi.
Miaka miwili baadaye, Februari 17, 2011 palikuwa na mlipuko mwingine kwenye kambi ya jeshi Gongo la Mboto katika kambi ya Jeshi ulitokea mlipuko mwingine na kusababisha watu kadhaa kujeruhiwa na wengine kufariki.
Akizungumza katika hafla ya kumwapisha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venancy Mabeyo, Jenerali Mwamunyange alisema kuwa katika kipindi chake chote cha uongozi hatasahau matukio hayo kwa kuwa yalikuwa ni makubwa na yalileta madhara kwa wananchi.
“Kipindi kigumu ni wakati ule tulipopata ajali kule Mbagala na baadaye Gongo la Mboto, ile ilikuwa ni ajali mbaya sana na bahati mbaya ajali hizo zilitokea nikiwa katika wadhifa mkubwa mkuu wa kijeshi,” alisema Jenerali Mwamunyange.
"Hicho kilikuwa kipindi kigumu sana kwangu, mambo mengine hayakuwa magumu sana, ila ajali ile ilisababisha watu kuumia, kupoteza mali."
Alisema wakati akiwa jeshini anakumbuka matukio mbalimbali ikiwamo vita dhidi ya Iddi Amini, kushiriki Commoro, kulinda amani Darful na Lebanon.
Naye Mkuu wa Majeshi, Jenerali Venency Mabeyo alisema ataendeleza ulinzi wa taifa kwa kuwa JWTZ ina dhamana ya ulinzi wa wananchi.
“Uongozi mahiri, ubunifu kwa ujumla... nimejifunza mambo mengi ya uongozi kutoka kwa Jenerali Mwamunyange,” alisema Jenerali Mabeyo.
Alisema ataanzia pale Jenerali Mwamunyange alipoishia, na kwamba Jeshi la wananchi wa Tanzania litaendelea kulinda amani katika nchi mbalimbali kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.
Tangu kuundwa upya baada ya uasi wa 1964, JWTZ imeongozwa na wakuu wa majeshi wafuatao: Jenerali Mrisho Sarakikya (1964-1974), Jenerali Abdalah Twalipo (1974-1980), Jenerali David Musuguri (1980-1988), Jenerali Ernest Kyaro(1988-1994), Jenerali Robert Mboma (1994-2001), Jenerali George Waitara (2001-2007) na Jenerali Mwamunyange (2007-2017).
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment