BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MRADI WA UKARABATI OFISI YA MAMA SAMIA YAKUMBWA NA HARUFU YA UFISADI


MAKALI ya Wabunge wa Bunge la 11 dhidi ya ufisadi yalijidhihirisha mjini Dodoma jana baada ya kamati yao inayoshughulikia Katiba na Sheria kueleza ilivyoingiwa hofu ya kuwapo harufu ya vitendo hivyo katika mradi wa ukarabati wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu.

Katika taarifa yake iliyowasilishwa bungeni mjini Dodoma jana, kamati ilidai kubaini kuwa ukarabati huo kwenye Ofisi ya Makamu wa Rais iliyopo Mtaa wa Luthuli jijini Dar es salaam, umefanyika chini ya kiwango na hivyo imeagiza uchunguzi ufanyike ili kujiridhisha na matumizi ya fedha zilizotumika kwa kazi hiyo.

Akisoma taarifa bungeni jana, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mohamed Mchengerwa, alisema kuwa katika fungu la 31 la ofisi hiyo, kwenye mradi namba 6389 ambao kamati ilifanya ziara zake imebaini kuwa jengo hilo limejengwa chini ya kiwango.

Alisema kamati imebaini kuwa kulikuwa na matumizi yasiyoridhisha ya fedha za umma katika baadhi ya miradi na kuagiza mamlaka zinazohusika kufanya uchunguzi maalumu kuhusu matumizi ya fedha na ubora wa miradi hiyo na kutoa taarifa kwa kamati.

Mchengerwa alisema katika mradi huo, wameagiza ufanyike uchunguzi na hatua kali zichukuliwe kwa watendaji wote waliohusika.

Tangu Serikali ya awamu ya tano iingie madarakani Novemba, 2015, chini ya utawala wa Rais John Magufuli na makamu wake Samia Suluhu, kasi ya vita dhidi ya vitendo vya rushwa na ufisadi imeongezeka huku ikielezwa kuwa hakuna atakayesalimika pindi ikibainika kuwa anashiriki vitendo vya aina hiyo vinavyokwamisha ufanisi wa miradi mingi ya maendeleo.

OFISI YA MWANASHERIA MKUU
Katika hatua nyingine, Mchengerwa alisema kuwa kamati yao ilibaini pia kuwapo kwa miradi mingi isiyofanikishwa kama ilivyotarajiwa kwa sababu ya kutolewa kwa kiasi kidogo cha fedha kisicholingana na mahitajhi.

Akieleza zaidi, Mchengerwa alisema Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imekuwa ikiomba fedha kiasi cha sh. bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi hiyo kwa miaka mitatu mfululizo bila ya mafanikio.

Alisema kwa mwaka 2014/15, 2015/16 na 2016/17, pamoja na kuomba fedha kwa kipindi hicho haikupokea fedha yoyote kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

MRADI WA NSSF DEGE ECO
Mwenyekiti huyo alizungumzia pia ripoti ya uchunguzi wa miradi ya NSSF ukiwamo wa Dege Eco, akisema kuwa ipo katika hatua za mwisho kukamilishwa na taasisi zinazofanya uchunguzi huo.

“Kamati ilitoa muda kwa Serikali kukamilisha ripoti hizi na inategemea kupewa taarifa kamili ya uchunguzi huu,” alisema Mwenyekiti huyo

Alisema katika ziara ya kamati ilikagua mradi wa nyumba za NSSF za Kigamboni- Mtoni Kijichi lakini imebaini kulikuwa na haja kwa Serikali kwa upande mmoja na NSSF kwa upande mwingine kujiridhisha na ukweli au upotoshaji wa ukweli kuhusu tuhuma zinazoelekezwa katika kufanikisha miradi hiyo.

Mchengerwa aliutaja mradi wa Dege Eco Village uliopo Kigamboni ambao ni wa ubia kati ya NSSF na kampuni ya Azimio Holdings. Aliongeza kuwa katika kikao cha kamati na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Novemba 17, mwaka huu kamati iliarifiwa kuwa taasisi za serikali kama Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru) na vyombo vingine vya usalama, vinaendelea na uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za miradi ya NSSF.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: