BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

PAUL MAKONDA NAMNA ANAVYOMPATIA RAIS MAGUFULI KIUBWETE

Rais John Magufuli akimuapisha Paul Makonda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam katika hafla iliyofanyika Ikulu. Picha na Maktaba

Dar es Salaam.
Jina la Paul Makonda huenda ndilo linalotajwa zaidi hivi sasa miongoni mwa viongozi wa Awamu ya Tano. Hiyo ni kutokana na staili yake ya utendaji kwani karibu kila hatua anayochukua imekuwa ikiibua mjadala mzito.

Kisiasa, Mkuu huyo wa Mkoa wa Dar es Salaam, ni kama amekuwa akijua kucheza na alama za nyakati kwani licha ya kupata upinzani mkubwa kutoka kwa baadhi ya wanasiasa na hata viongozi, misimamo yake mingi imekuwa ikipata baraka za Rais John Magufuli tena hadharani.

Utendaji wake ulionekana kumvutia Rais Magufuli tangu akiwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni hasa baada ya kuanzisha mkakati wa ujenzi wa madarasa wilayani humo Desemba 2015 ukilenga kujenga shule sita za sekondari ili kuwapa nafasi wanafunzi 3,000 waliokuwa wamefaulu darasa la saba wilayani humo.

Hatua hiyo ya Makonda kuchangisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ilimvutia Rais Magufuli ambaye aliwataka mawaziri wote kukatwa Sh1 milioni moja kwenye mishahara yao wakiwamo pia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Rais Magufuli alisema hayo alipokuwa akizungumza na Taifa kupitia mkutano wake na wazee wa Dar es Salaam, baada ya kuelezwa matatizo ya ongezeko la wanafunzi wa darasa la kwanza katika mkoa huo, lililotokana na utekelezaji wa ahadi ya elimu bure.

Katika Mkutano huo uliofanyika Februari 13, 2016 katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Rais Magufuli alimsifu Makonda akisema kwa jitihada hizo, hata akipandishwa cheo watu wasishangae.

Pamoja na sifa hizo, baadhi ya viongozi wamekuwa wakimwona Makonda kama mwanasiasa anayetafuta sifa kwa Rais.

Meya wa Manispaa ya Kinondoni wakati huo, Boniface Jacob aliwahi kukaririwa akimtaka Makonda kuacha kutafuta sifa ili aonekane ni mchapakazi akidai kwamba anadandia kazi zisizomuhusu.

Alisema Makonda hapaswi kuingilia kazi za halmashauri hadi awasilishe barua ya maombi kwa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri husika au meya kama anahitaji kufanya jambo lolote.

Wakati wa malumbano, mkuu huyo wa mkoa aliingia katika mgogoro na aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe ambaye sasa ni marehemu.

Mgogoro baina ya Makonda alimtuhumu Kabwe kuingia mikataba yenye utata na wafanyabiashara katika Stendi Kuu ya Mabasi yaendayo Mikoani Ubungo (UBT) na kuitaka mamlaka ya uteuzi kumwondoa katika mkoa wake na kumpangia kazi nyingine.

Akizungumza katika uzinduzi wa Daraja la Kigamboni, Aprili 19, 2016 mbele ya Rais Magufuli, RC Makonda alitoa taarifa ya uchunguzi wa ufisadi wa utekelezwaji wa mikataba mitatu, iliyohusu maeneo ya ukusanyaji mapato ya UBT na kodi ya uegeshaji magari katikati ya mji na kuisababishia Serikali hasara ya Sh3 bilioni.

Alisema Kabwe alisaini mikataba miwili, wa 2004 na wa 2009. Mkataba wa 2004 ulipelekwa jiji na ule wa 2009 ukapelekwa kwa mzabuni, hivyo kusema jiji lilikuwa linajua kuwa basi linatozwa Sh4000 kwa mwezi wakati mzabuni akitozwa 8,000 kwa mwezi.

Rais alitoa majibu ya malalamiko hayo ya Makonda hapohapo kwenye uzinduzi baada ya kutangaza kumsimamisha kazi Kabwe na kuagiza vyombo vya dola vianze uchunguzi mara moja ili hatua zaidi za kisheria zichukuliwe.

Mapema Machi 2016, Makonda aliwataka wamiliki wote wa silaha jijini Dar es Salaam kuwasilisha taarifa za uhalali wa silaha zao na kusajiliwa upya kwa wakuu wa polisi wa wilaya (OCD).

Aliwataka watu wote wanaomiliki silaha hizo kinyume cha sheria kuzisalimisha kabla ya kuanza kwa operesheni ya ukaguzi Julai Mosi mwaka huu.

Agizo hilo liliitikiwa na Rais Magufuli ambaye, Machi 21, alimwita Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro kuhakiki silaha zake.

Novemba 25, 2016, Makonda akiwa katika ziara ya siku 20 katika mkoa wake iliyopewa jina la ‘Dar mpya’ akitembelea maeneo mbalimbali ya mkoa wake kusikiliza kero za wananchi na kuzitolea maelezo, Rais Magufuli alimpigia simu na kumpongeza kwa juhudi anazofanya katika kusikiliza na kutatua kero za wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam.

“Endelea hivyo, kutembelea wananchi na kutoa ufafanuzi kwa sababu nyingine ufafanuzi huu kama ungetolewa mapema wala wananchi wasingekuwa na sababu ya kuja kuuliza maswali.

“Kwa hiyo endeleeni hivyohivyo Dar es Salaam na wakuu wa wilaya yako na watendaji wote hongereni kwa kazi nzuri mnazozifanya kwa kusikiliza kero zao bila kujali vyama vyao bila kujali makabila yao...,” alisema Rais Magufuli.

Vita dhidi ya dawa za kulevya
Mwanzoni mwa mwezi huu, Makonda alianzisha vita ya kupambana na dawa za kulevya kwa staili ya aina yake. Alianzisha utaratibu wa kutaja majina ya watu akielekeza wafike katika Kituo Kikuu cha Polisi kuonana na Kamanda Sirro akiwahusisha kwa njia moja au nyingine na dawa hizo. 


Alianza utaratibu huo Februari 2 alipotaja majina ya wasanii na maofisa wa Jeshi la Polisi.

Wasanii waliotajwa walifika polisi kabla ya kupandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambako waliwekwa chini ya uangalizi maalumu.

Hatua hiyo ilianza kuungwa mkono na Inspekta Jenerali wa Polisi, IGP Ernest Mangu ambaye alitangaza kuwasimamisha kazi maofisa 12 wa jeshi hilo waliotajwa na Makonda katika sakata hilo.

Hata hivyo, kabla ya kufikishwa kizimbani na kuhukumiwa, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye alitaka busara itumike katika kushughulikia sakata la wasanii hao akisema pamoja na wizara yake kuunga mkono vita dhidi ya dawa za kulevya, alitaka wasihukumiwe kwa tuhuma.

Alitaka suala hilo lifanywe kwa namna ambayo italinda haki ya mtuhumiwa na kurejesha heshima yake akibainika hana kosa.

“Sisi kama wizara tunaunga mkono jitihada za vyombo mbalimbali katika kupambana na jambo hili lakini ni vizuri tukaangalia tukalifanya katika namna ambayo inalinda haki ya mtuhumiwa

“Ni vyema ikalinda haki ya mtuhumiwa na kumpa nafasi ya kesho na keshokutwa kama ikithibitika hahusiki bado a regain (arudishe) heshima aliyokuwa nayo. It’s a little bit complicated (ni jambo linachanganya kidogo)”.

Lakini siku chache baadaye Rais Magufuli alipigilia msumari suala hilo. Akizungumza wakati wa kuwaapisha viongozi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na viongozi wengine, Rais Magufuli alisema wote wanaotuhumiwa wakamatwe bila kujali umaarufu wao ili wataje mtandao wote.

Huku akimpongeza Makonda, Rais Magufuli alimwambia, “Tembea kifua mbele katika vita hii ya dawa za kulevya, hakuna mtu maarufu, hakuna mwanasiasa, hakuna askari, hakuna waziri, au mtoto wa fulani ambaye akijihusisha aachwe. Hata angekuwa mke wangu Janet shika tu. 


Kwa sababu dawa za kulevya kwa Taifa letu sasa hivi zimefikia mahali pabaya.” Pia alimpongeza IGP Mangu kwa kuwasimamisha maofisa waliotuhumiwa akisema hatua hiyo imeleta taswira nzuri kwa jeshi hilo dhidi ya vita hiyo.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: