WEMA SEPETU AENDELEA KUSOTA RUMANDE KITUO KIKUU CHA POLISI DAR ISHU YA MADAWA YA KULEVYA
Msanii wa filamu nchini, Wema Sepetu.
Dar es Salaam. Wakati wasanii 13 wakipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa nyakati tofauti na kuweka chini ya uangalizi, wenzao wawili, Wema Sepetu na Omari Micheri wameendelea kusota rumande kwa zaidi ya saa 120.
Wema na Omari ndiyo pekee katika kundi la wasanii waliojisalimisha katika Kituo Kikuu cha Polisi tangu Ijumaa iliyopita kwa tuhuma za ama kutumia au kuuza dawa za kulevya waliodaiwa kukutwa na vielelezo.
Wakati Wema akidaiwa kukutwa na misokoto ya bangi, Omari anadaiwa kukamatwa na kete nne za dawa za kulevya ambazo hazijafahamika.
Juzi, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Siro alisema wasanii hao wangepelekwa mahakamani juzi pamoja na wenzao, lakini wawili hao hawakupelekwa hadi jana.
Baada ya kufikishwa mahakamani, wasanii watano kati ya 13 waliwekwa chini ya uangalizi wa mahakama kwa miaka mitatu huku wenzao wanane wakiwekwa chini ya uangalizi wa mahakama wa mwaka mmoja.
Waliowekwa chini ya uangalizi wa miaka mitatu na Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha na kutakiwa kuripoti polisi mara mbili kwa mwezi ni Ahmed Hashim maarufu kama Petitman, Said Masoud Linnah maarufu kama Said Alteza, Nassoro Mohamed Nassoro, Bakar Mohamed Khelee na Lulu Abbas Chelangwa maarufu kama Luludiva.
Katika kesi ya pili iliyosomwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, wasanii wanane waliwekwa chini ya uangalizi wa mahakama kwa mwaka mmoja tofauti na miaka mitatu iliyoombwa na upande wa mashtaka.
Wasanii hao ni Hamidu Salum Chambuso maarufu kama Dogo Hamidu, Rajabu Salum, Romeo George Angala maarufu kama Rommy Jones, Cedou Madigo, Khalid Salum Mohamed maarufu TID, Johana Johannes Mathysen, Rechoel Josephat na Anna Patric Kimario maarufu Tunda.
0 comments:
Post a Comment