Na Mwinyimvua Nzukwa, Zanzibar
Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi amesema Serikali imelazimika kuchukua uamuzi wa kusimamia moja kwa moja uchimbaji wa mchanga na kutoa bei elekezi ili kudhibiti uharibifu wa mazingira na ulanguzi wa malighafi hiyo inayotumika kwa ujenzi.
Akifunga mkutano wa tatu wa baraza la 10 la wawakilishi Zanzibar Chukwani nje kidogo ya mji wa Zanzibar, Balozi Seif amesema pamoja na hatua hizo serikali imeweka utaratibu wa maeneo ya kuchimbwa bidhaa hiyo huku ikipiga marufuku kwa maeneo ya kilimo kutumiwa kwa uchimbaji.
Amesema hatua hiyo imekuja kutoaka na kuwepo kwa dalili za kumalizika kabisa maeneo ya uchimbaji wa mchanga jambo ambalo litaongeza ukali wa maisha kwa wananchi wa Zanzibar kutokana na kuongezeka kwa gharama za ujenzi.
Amesema kamati ya wataalamu kwa kushirikiana na kamati ya mawaziri wa wizara zinazohusika na maliasili na mazingira zimetoa maamuzi kuwa serikali itayafungua mashimo ya mchanga yaliyozuiliwa ili kupunguza usumbufu kwa wananchi wanaohitaji rasilimali hiyo.
Aidha amesema udhibiti huo unaofanywa na serikali wa rasilimali mchanga unaweza kupelekea wananchi kuvamia maeneo ya fukwe na kuchimba mchanga hivyo amezitaka mamlaka husika kuweka ulinzi katika maeneo hayo ili kuepusha madhara zaidi.
Balozi Seif pia aliesema serikali haitosika kutoa adhabu kwa wamiliki wa magari ya punda na n’gombe watakaokamatwa wakichota mchanga katika maeneo yasioruhusiwa ikiwa ni pamoja na kutaifishwa magari yao.
Akizungumzia suala la dawa za kulevya, Balozi Seif alisema serikali inaendeleza mapambano yaliyoanza katika maeneo mengine ya Tanzania na kwamba Zanzibar haitakuwa jaa na kimbilio la wahusika wa biashara hiyo.
Alisema katika kuhakikisha vita hiyo inashinda, alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama na wananchi kushirikiana na kuwafichua watu wanaoendeleza biashara ya dawa za kulevya na kuifanya Zanzibar kuwa gereza la kuwatia hatiani ili kukomesha janga hilo.
Akizungumzia kukithiri kwa vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia, Balozi Seif alisema serikali ya Zanzibar itaendelea na mapambano hayo na kutovifumbia macho ambapo inakusudia kubuni mbinu mbadala za ushughulikiaji kesi zinazohusiana na udhalilishaji ili zipate hukumu kwa lengo la kupunguza na kukomesha tatizo hilo.
Wakati huo huo kabla ya baraza hilo kuahirishwa hadi mei 10 mwaka huu saa 3 asubuhi, wajumbe wa baraza hilo walimchagua mwakilishi wa jimbo la Magomeni Rashid Makame Shamsi kuwa kamishna wa Tume ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi wa mjumbe wa tume ya bajeti ya baraza hilo ili kuweza kutetea maslahi ya Wafanyakazi na Wajumbe wa Baraza hilo.

0 comments:
Post a Comment