BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WALIOFUKUZWA KIMIZENGWE NDANI YA CCM, WAKINGIWA KIFUA NA NAIBU KATIBU MKUU WA CCM ZANZIBAR

NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai.
 
Na Mwinyimvua Nzukwi, Zanziba.
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai ameuagiza Uongozi wa chama hicho wilaya ya Mjini kichama kufuatilia sababu za kufukuzwa kwa viongozi wawili wa jimbo la Jang’ombe na kulitafuta ufumbuzi wa tatizo hilo haraka kupitia muongozo na kanuni za chama hicho.

Alisema CCM ina utaratibu wa kushughulikia migogoro inayojitokeza ndani ya chama na jumuiya zake kwa ngazi mbali mbali kwa kufuata misingi ya katiba hivyo ni lazima kasoro zinazojitokeza ndani ya taasisi hiyo ni lazima zitatuliwe kwa utaratibu uliowekwa na sio matakwa binafsi ya baadhi ya Viongozi.

Vuai alifafanua kwa mujibu wa Kanuni za masuala ya uongozi kamati za siasa za majimbo hazina mamlaka ya kuwafukuza ama kuwaondosha katika nafasi za uongozi kwa ngazi za majimbo badala yake wanatakiwa kufanya vikao vya kikatiba kuwajadili watu wanaotuhumiwa na kuwasilisha mapendekezo yao kwa ngazi ya wilaya ili ijadili na kuchukua hatua stahiki kwa kuzingatia taratibu za chama.

Agizo hilo limetokana na kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa viongozi wawili waliovuliwa nafasi za uongozi katika jimbo hilo kumueleza kiongozi huyo kuwa wameonewa kwani wamefukuzwa wakiwa hawajui kosa linalowakabili na bila kupewa nafasi za kujieleza.

Akitoa ufafanuzi juu ya malalamiko hayo Vuai aliutaka uongozi wa wilaya hiyo kufuatilia kwa karibu mgogoro huo ili umalizike bila kuathiri uongozi wa jimbo hilo.

“Chama Cha Mapinduzi kinaongozwa kwa misingi ya katiba na maamuzi yanayofanyika yanafuata muongozo huo na kila ngazi imepewa majukumu yake hivyo nakukumbusheni kuwa viongozi tuwe makini kuhakikisha tunasoma kwa makini Katiba na Kanuni zinazotuongoza na tusikubali kugawanyiwa na tofauti ndogo ndogo zinazojitokeza”, alisema Vuai.

Aidha aliwataka wanachama na viongozi hao kuwa tayari kwa mabadiliko ya kimuundo yanayofanyika ndani ya taasisi hiyo yanalenga kukijenga chama kuwa na nguvu za kiuchumi na kuisimamia kikamilifu serikali juu ya matumizi mazuri ya rasilimali zake kwa maslahi ya wanachama wote.

Akitoa ufafanuzi juu ya tuhuma hizo Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mjini, Juma Fakih Choum alieleza kuwa baada ya kupata malalamiko ya kufukuzwa kwa viongozi hao wilaya hiyo ilichukua hatua za kuuagiza uongozi wa jimbo kukutana pamoja ili kujadiliana namna ya kuutafutia ufumbuzi mzozo huo.

Mwenyekiti huyo alisema kuwa ndani ya wilaya hiyo wamejiandaa kikamilifu kushiriki katika uchaguzi wa chama na jumuiya zake ili kupata viongozi na watendaji imara wa ngazi mbali mbali watakaoweza kusimamia mikakati ya ushindi mwaka 2020.


Naibu Katibu Mkuu huyo yupo katika ziara ya kichama ndani ya mkoa wa mjini macharibi kwa lengo la kukagua uhai wa chama na amekwa akiwakumbusha viongozi na watendaji wa chama hicho kusimamia vizuri miradi ya CCM ili isaidie shughuli za kiutendaji na kuwanufaisha wanachama wote badala ya watu wachache
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: