
SHINYANGA, Tabora, Mara na Dodoma ni mikoa ambayo inaongoza kwa ndoa za utotoni, Bunge lilielezwa jana mjini hapa.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Vijana, Dk. Hamisi Kigwangalla, alisema mikoa hiyo inaongoza kwa vitendo hivyo kwa zaidi ya asilimia 50 kila mmoja kulinganisha na mingine.
Akijibu swali la Anne Kilango Malecela (Kuteuliwa), Dk. Kigwangalla alisema Shinyanga ndiyo kinara kwa asilimia 59 ikifuatiwa na Tabora asilimia 58. Mingine na asilimia kwenye mabano ni Mara (55) na Dodoma (51).
Katika swali hilo, Malecela alitaka kujua serikali ina mkakati gani wa kutokomeza ndoa za utotoni ambazo kwa sasa zimeathiri sana na zina athari kubwa ndani ya jamii.
Naibu Waziri alisema serikali inatambua athari kubwa zinazosababishwa na ndoa za utotoni ambazo zimekuwa zikiwanyima watoto wa kike fursa ya kupata elimu na kwamba ili kukabaliana na tatizo hilo, imechukua hatua mbalimbali.
Aidha alisema mimba za utotoni ni hatari kwa afya ya mama na mtoto kwa kuwa maumbile ya kibaiolojia ya mtoto hayawezi kuhimili mchakato wa uzazi na mara nyingi mimba hizo husababisha vifo.
Dk. Kigwangalla alisema katika kukabiliana na changamoto hiyo, serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwamo kutoa elimu ya malezi chanya kwa wazazi na walezi ili kutambua umuhimu wa kumwendeleza mtoto wa kike.
“Halmashauri za wilaya, manispaa na miji 72 zimepata elimu hii na msukumo umeongezwa zaidi katika kuelimisha familia, wazee wa mila na jamii kuachana na mila na tamaduni zilizopitwa na wakati za kuoza watoto wa kike,” alisema.
Hata hivyo, alisema kwa upande wa muundo wa kisera na kisheria, serikali imezifanyia maboresho ili kumlinda mtoto wa kike dhidi ya ndoa na mimba za utotoni.
Alisema mpango kazi wa taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto uliozinduliwa Desemba 13, mwaka jana, umelenga kupunguza mimba za utotoni kutoka asilimia 47 hadi asilimia 10 ifikapo mwaka 2022.
Alisema mpango kazi huo utaanza kutekelezwa Julai, mwaka huu na umelenga zaidi kuzuia na kupunguza vitendo vyote vya ukatili dhidi ya watoto kwa asilimia 50 na umeweka lengo la kupunguza kutoka asilimia 47 hadi 10 ifikapo 2022.NIPASHE

0 comments:
Post a Comment