Akizungumza na gazeti hili jana muda mfupi kabla ya kuingia kwenye mazoezi jana jioni yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini, Kocha wa Yanga, Mzambia George Lwandamina, alisema matokeo hayo ya
Simba kwao yamewapa changamoto ya kuhakikisha wanaendeleza ushindi kwenye michezo iliyobaki ili kutetea ubingwa wao.
Alisema mbio za ubingwa zimebaki kwa timu mbili (Yanga na Simba) na kufungwa kwa Simba na Kagera Sugar kumewapa nafasi ya kujipanga zaidi.
"Unajua ili Yanga itetee ubingwa wake kwanza ilikuwa lazima Simba iteleze, na hilo limetokea na tunaongoza ligi kwa sasa... bado kazi haijaisha na ndio kwanza imeanza, tunachotakiwa kufanya kwa sasa ni kuongeza nguvu kwenye michezo yetu iliyobaki na kuhakikisha hatupotezi," alisema Lwandamina.
Simba juzi Jumapili ilikubali kipigo cha mabao 2-1 ikiwa ugenini mbele ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Aidha, alisema taratibu kikosi chake kimeanza kuimarika hasa baada ya adhabu ya kadi zilizokuwa zikiwakabili Kelvin Yondani na Hassan Kessy kumalizika.
"Tunafuatilia kwa karibu hali za Ngoma (Donald) na Tambwe (Amissi)... Ngoma muda wowote atarudi uwanjani kwa sababu ameanza mazoezi na nafikiri mambo yakienda sawa anaweza akacheza mchezo ujao," aliongezea kusema Lwandamina.
Yanga inayoongoza ligi kwa tofauti ya pointi moja baada ya kukusanya pointi 56 ikifuatwa na Simba, Jumamosi hii itacheza mchezo wake wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya MC Alger ya Algeria kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mabingwa hao watetezi hawatakuwa na mchezo wa ligi mpaka mwanzoni mwa mwezi ujao itakapocheza na Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Taifa baada ya kumaliza mechi zake mbili dhidi ya MC Alger.

0 comments:
Post a Comment