BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

BAJETI YA FEDHA YA TANZANIA KWA MWAKA 2017/2018 KUWASILISHWA LEO BUNGENI NA WAZIRI WA FEDHA


Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango.

NCHI za Afrika Mashariki ikiwamo Tanzania zinawasilisha bajeti zao kwa mwaka wa fedha 2017/2018. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango anatarajiwa kuwasilisha bajeti hiyo bungeni leo mjini hapa kuanzia saa 10 kamili jioni.

Kabla ya kufanya hivyo, asubuhi Dk Mpango atawasilisha Taarifa ya Hali ya Uchumi ya nchi, ambayo itajikita katika kueleza mipango ya maendeleo kwa mwaka ujao. Kwa mujibu wa ratiba ya Bunge la Tanzania katika Mkutano wake wa Saba wa Bunge la Bajeti, wabunge watatumia kesho kusoma na kutafakari hotuba hiyo.

Kuanzia Jumatatu ijayo Juni 12 hadi Juni 20, mwaka huu, wabunge watajadili Taarifa ya Hali ya Uchumi na Bajeti ya Serikali kwa siku saba kabla ya jioni ya Juni 20, mjadala kuhitimishwa kwa upigaji kura ya wazi.

Machi 29, mwaka huu, Dk Mpango alisoma bungeni mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na kiwango cha ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa 2017/18, na kueleza kuwa serikali katika bajeti hiyo inatarajia kuwa na ukomo wa Sh trilioni 31.6.

Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2016/2017 inayomalizika Juni 30, mwaka huu ilikuwa ya Sh trilioni 29.5. Katika Sh trilioni 31.6, za maendeleo zimeongezeka kutoka Sh trilioni 11.8 katika mwaka 2016/17 hadi Sh trilioni 11.9 katika mwaka wa bajeti 2017/18.

Ongezeko hilo ni kiasi sawa na asilimia 38 ya bajeti hiyo tarajiwa. Dk Mpango alisema maeneo kipaumbele ya bajeti ni miradi ya maendeleo inayolenga kufanikisha utekelezaji wa Malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.

Aliitaja miradi ya maendeleo ni ule wa makaa ya mawe wa Mchuchuma na Liganga, ujenzi wa reli ya kati kutoka Dar es Salaam, Tabora hadi Kigoma yenye urefu wa kilometa 1,251 kwa kiwango cha standard gauge.

Pia ujenzi huo ni pamoja na matawi ya Tabora kupitia Isaka hadi Mwanza (kilometa 379), Isaka hadi Rusumo (kilometa 371), Kaliua kupitia Mpanda hadi Karema (Kilometa 321), Uvinza kutoka Hoima, Uganda hadi Tanga, Tanzania na kusomesha vijana wengi zaidi katika stadi za mafuta na gesi, uhandisi na uboreshaji huduma za afya.

“Maeneo mengine ni viwanda vya kukuza uchumi wa viwanda, kuwianisha maendeleo ya uchumi na ya watu na mazingira ya wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji,” alieleza Dk Mpango.

Aidha, alilitaja eneo jingine muhimu ni uendelezaji sekta za ubia kati ya sekta ya umma na binafsi pamoja na maeneo mengine muhimu kwa ukuaji wa uchumi na ustawi wa taifa.

Alisema lengo la uandaaji wa mpango wa bajeti, unaongoza serikali katika kusimamia mambo ya uchumi ikiwamo kuongeza kasi ya ukuaji wa Pato la Taifa kufikia asilimia 7.5 katika mwaka huu, asilimia 7.9 mwakani na asilimia 8.2 mwaka 2019.

Aliongeza kuwa mpango huo unalenga kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kubaki na tarakimu moja hadi kufikia asilimia 5.0 katika kipindi cha muda wa kati, kuwa na pato ghafi la taifa la Sh trilioni 123.9 kwa mwaka 2017/18, Sh trilioni 139.7 kwa mwaka 2018/19 na Sh trilioni 165.4 mwaka 2019/2017 na mapato ya kodi kufikia asilimia 14.6 ya pato la taifa mwaka 2017/18, asilimia 15.5 mwaka 2018/19 na asilimia 15.8 mwaka 2019/20.

Alifafanua kuwa Sh trilioni 31.6 zitakazokusanywa na kutumika 2017/18, mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa Sh trilioni 20.872 sawa na asilimia 63 ya mahitaji yote. Kati ya mapato hayo, serikali inalenga kukusanya mapato ya kodi ya Sh trilioni 18.097 (sawa na 87% ya mapato ya ndani), na mapato yasiyo ya kodi Sh trilioni 2.022 na kutoka vyanzo vya halmashauri yanatarajiwa kuwa Sh bilioni 753.3.

Alieleza kuwa serikali inategemea kukopa kiasi cha dola za Marekani milioni 900 (Sh trilioni 2.080) kutoka vyanzo vya nje vyenye masharti ya kibiashara na Sh trilioni 4.434 zinazotarajiwa kupatikana kutokana na mikopo ya ndani ili kulipia hatifungani na dhamana za serikali zinazoiva.

Kwa mujibu wake, Sh trilioni 1.859, sawa na asilimia 1.5 ya Pato la Taifa ni mikopo mipya ya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Pia washirika wa maendeleo wanatarajiwa kuchangia Sh trilioni 3.7.

Kati yake, Sh bilioni 496.3 ni misaada na mikopo nafuu ya kibajeti (GBS), Sh trilioni 2.821 ni misaada na mikopo kwa ajili ya miradi ya maendeleo na Sh bilioni 382.4 ni misaada na mikopo nafuu ya mifuko ya pamoja ya kisekta.

Aidha, matumizi ya maendeleo yatakuwa Sh trilioni 13.164, sawa na asilimia 40 ya bajeti yote, ambapo fedha za ndani ni Sh. trilioni 9.960, sawa na asilimia 76. Wakitoa maoni yao yao juzi, wabunge wengi waliishauri serikali kuongeza fedha zaidi kwenye sekta ya maji na sekta ndogo ya umeme ili kuharakisha maendeleo pamoja na kuondoa kero za wananchi wengi wa vijijini.

Pia walipendekeza katika bajeti hiyo ya leo serikali ipunguze Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) hadi kufikia asilimia 16 kutoka 18 ya sasa na iondoe kodi hiyo katika bidhaa zinazoagizwa kutoka nje.

Aidha, walitaka VAT iondolewe katika malighafi za mazao yanayozalishwa nchini, na kusiwapo na ushuru wa bidhaa katika pembejeo za kilimo, pamoja na kutopandisha ushuru wa bia na vinyaji baridi.

Akizindua kituo maalumu cha ukusanyaji kodi jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Rais John Magufuli pia aligusia suala la bajeti kila mwaka kupandisha kodi katika vinywaji baridi na bia, akitaka mamlaka husika zitafune namna ya kupata kodi katika vyanzo vingine vya mapato.

Aidha, katika bajeti inayofikia ukomo Juni 30, mwaka huu, wabunge walilalamikia baadhi ya kodi zilizopitishwa. Baadhi yake ni VAT kwenye miamala ya benki na kampuni za simu za mikononi, pamoja na kukatwa kodi katika kuweka vocha za matumizi ya simu hizo.

Mbali na kodi hizo, ongezeko la VAT kwenye mizigo inayosafirishwa nje ya nchi pamoja na kwenye utalii zimeelezwa kuyumbisha kwa kiasi kikubwa sekta hizo. Katika mijadala yao, pia wabunge wametaka kuongezwa kwa tozo ya mafuta kutoka Sh 50 hadi kufikia Sh 100 ili fedha zinazopatikana ziende kusaidia sekta ya maji vijijini hasa kwa kuwa na Mfuko wa Maji Vijijini.

Aidha, akijibu swali bungeni juzi, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji alieleza kuwa serikali itawasilisha katika bajeti yake mapendekezo ya kufuta misamaha ya kodi isiyo na tija.

Dk Kijaji alisema mpango wa serikali ni kuhakikisha misamaha ya kodi inashuka mwaka hadi mwaka na katika mwaka ujao wa fedha, serikali italeta mapendekezo ya marekebisho ndani ya bajeti itakayosomwa kesho.

Majibu ya hoja hizo na nyinginezo, yatakuwa yamepata ufumbuzi au kujulikana jinsi serikali ilivyoyazingatia wakati itakapofika saa 12 jioni leo, wakati Dk Mpango atakapokuwa amekamilisha hotuba yake ya bajeti ya pili ya utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: