BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

KLABU YA SHUPAVU FC YAPIGA HESABU KALI ZA KUIBUKA KINARA LIGI YA MABINGWA WA MIKOA KITUO CHA LINDI

Ligi ya mabingwa wa mikoa 2017/2018 iliyokuwa ianze kutimua vumbi Mei 28 mwaka huu kituo cha Lindi imesogezwa mbele huku klabu ya Shupavu FC ya Ifakara mkoani Morogoro ikiendeleza kupiga hesabu kali za kuibuka vinara lakini na kutimiza lengo la kukusanya fedha kiasi cha sh60 milioni kama bajeti yao.

Akizungumza na gazeti hili mjini hapa, Mwenyekiti wa chama cha soka wilaya ya Kilombero, Tanuwili Bahanuzi alisema kuwa ligi hiyo imesogezwa mbele hadi Juni 15 mwaka huu na shirikisho la soka Tanzania (TFF) na kutoa mwanya zaidi wa maandalizi ya klabu yao.

Bahanuzi alisema kuwa kusogezwa mbele kumetoa mwanya wa maandalizi kuandaa klabu lakini na ukusanyaji wa fedha za ahadi zilizoahidiwa na wadau kuichangia Shupavu FC ili kufanya vizuri ligi ya mabingwa wa mikoa ili kuibuka vinara wa kwanza kituo cha Lindi.

“Hesabu zetu kama chama cha soka wilaya ya Kilombero, klabu, serikali ya wilaya na wadau wa soka kiujumla tumeweka lengo la kuwa vinara wa kituo cha Lindi na hilo linawezekana kwani tumefanya maandalizi ya kutosha na bado tupo vizuri kiuchumi.”alisema Bahanuzi.

Bahanuzi alisema kuwa Mei 22 mwaka huu walipitisha bajeti ya sh60 milioni zinazoendelea kuchangwa na wadau wakiongozwa na mkuu wa wilaya Kilombero, James Ihunyo.

“Bajeti imegawanyika katika sehemu mbili, bajeti ya kwanza ni sh sh30 milioni hii itatumika katika ligi ya mabingwa wa mikoa na sh30 milioni nayo itatumika katika ligi daraja la pili hivi ndivyo mipango yetu tulivyopanga na tuna uhakika wa kuwa washindi wa kwanza.”alisema Bahanuzi.

Aliongeza kwa kusema viongozi hao wanaamini kuwa ili timu isiwe na vikwazo vyovyote katika ushiriki wao wa ligi ya mabingwa wa mikoa kituo cha Lindi ni kuiwezesha kiuchumi ili ibakie kazi ya kusaka ushindi uwanjani ndani ya dakika 90.

Katibu Tawala wilaya ya Kilombero, Robert Selasela alisema kuwa kusogezwa mbele kwa michezo ya ligi hiyo kumetoa nafasi nzuri ya wao kukusanya fedha kutoka kwa wadau wa soka kwa ajili ya kuichangia klabu ya Shupavu FC baada ya kutoa ahidi ya kuichangia wakati wa chakula cha hisani na sh24 milioni zilichangwa kama ahadi.

Selasela alisema kuwa kamati yake inaendelea kuhamasisha wadau ili waendelee kutekeleza ahadi zao za kuichangia timu na kufikia lengo la bajeti ya sh60 milioni ili itimize malengo ya kufanya vyema ligi ya mabingwa wa mikoa na kuibuka vinara.

“Tunataka kuona Shupavu FC ikifanya vyema kwani tayari viongozi wamepitisha bajeti ya sh60 milioni kwa ajili ya ligi ya mabingwa wa mikoa na ligi daraja la pili msimu ujao na wadau wameonyesha nia thabiti ya kuiunga mkono klabu yao isonge mbele.”alisema Selasela.

Kwa upande wa Kocha mkuu wa Shupavu FC, Steven Mtenga alisema kuwa benchi la ufundi linaendelea kuwanoa wachezaji kwa kuwafanyisha mazoezi kutwa mara tatu.

“Benchi la ufundi halina wasiwasi na ligi ya mabingwa wa mikoa, tunaenda Lindi kwa dhamira moja tu ya kusaka ushindi kwa kila mchezo kwani lengo letu ni kucheza ligi daraja la pili na ili tuingie huko inatulazimu tufanye vizuri na kuibuka vinara kundi letu na hii itakuwa furaha kwa wanaKilombero na mkoa kiujumla.”alisema Mtenga.

Mtenga alisema kuwa kikosi chao kipo imara na kitaonyesha ushindani wa hali ya juu kwani baada ya kusogezwa mbele, benchi la ufundi limekuwa likiongeza mbinu zaidi za kiufundi kwa wachezaji ikiwemo nidhamu ndani ya uwanja itayofanya timu yao iwe moto wa kuotea mbali na tishio kutokana na kutandaza soka la kitabuni.
Share on Google Plus

About Juma Mtanda

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
Post a Comment