BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MAMLAKA YA MAPATO TANZANIA YAKOMAA NA WAFANYABIASHARA VITUO VYA MAFUTA JUU YA MASHINE YA EFDs


Kamishna wa Kodi za Ndani wa TRA, Elijah Mwandumbya

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imesema kwamba licha ya kufungia mamia ya vituo vya mafuta nchi nzima, leo itaendelea na operesheni hiyo ya kufunga vituo vingine vya mafuta ambavyo havijafunga moja kwa moja mashine za malipo za kielektroniki (EFDs) na pampu.


Kamishna wa Kodi za Ndani wa TRA, Elijah Mwandumbya alisema jana kuwa wale TRA imewafungia vituo vyao, watafunguliwa tu iwapo watakidhi vigezo ambavyo ni pamoja na kulipia mashine na kuingia makubaliano na mamlaka hiyo kuwa ni muda gani mafundi watakuwa wamefunga mashine hizo. 


Mwandumbya alisema kwa sasa TRA haitaruhusu wenye vituo vya mafuta waendelee kutumia mashine za mkono ambazo ziko nje ya mashine kwani wametumia mwanya huo kukwepa kodi ya serikali.

Alisema kati ya watu 10 wanaojaza mafuta, ni wawili tu ndio walikuwa wanapewa risiti hizo tena kwa kuzidai. “Tunatoa mwito kwa wale ambao tumeshawafungia wafuate vigezo ili waweze kufunguliwa, wakalipie na waingie na makubaliano na TRA mkoa kwamba ni lini watafunga mashine baada ya kuzilipia,” alisema Mwandumbya. 


Alisema TRA itafuatilia muda huo ambao wameingia makubaliano na mwenye kituo cha mafuta kama atatimiza ahadi.

Alisema operesheni ya kukagua vituo itaendelea kufanyika nchi nzima na akaongeza kuwa leo watatangaza ni vituo vingapi hadi jana vilikuwa vimeshafungiwa kwa kukaidi kufunga mashine hizo.


“Kwa Dar es Salaam peke yake tumeshafungia vituo 71, kesho (leo) tunacompile (tunakusanya) takwimu za nchi nzima na tutatoa taarifa kwa vyombo vya habari,” alisema Mwandumbya.

Alipoulizwa kuwa TRA haioni kwamba hatua ya kufungia vituo italeta usumbufu kwa wananchi, Mwandumbya alijibu: “Kamwe hatutaruhusu wafanyabiashara waendelee kukwepa kodi kwa kisingizio cha wananchi kuteseka kwa kukosa huduma, tunachotaka wafuate sheria.” 


Kuhusu madai yanayotolewa na baadhi ya wafanyabiashara wa mafuta kwamba TRA imekurupuka kuchukua hatua hizo, kwani walishaingia makubaliano na wenye vituo vya mafuta vya kusogeza mbele muda wa kufunga mashine, Mwandumbya alisema sio kweli kwani changamoto zilizokuwepo hapo awali zote zilishatatuliwa na serikali.

Alisema ni kweli kwamba awali wakati serikali inatoa agizo la kuhakikisha vituo hivyo vinafunga mashine za EFDs kwenye pampu za mafuta, kulikuwa na changamoto za gharama za mashine kuwa juu. 


Alitoa mfano kuwa awali mashine moja ya EFDs ilikuwa inauzwa kwa Dola za Marekani 3,500 na baadaye Dola 2,500. Alisema kwa hali hiyo mtu ambaye alikuwa na mashine nne alitakiwa kulipia Dola za Marekani 10,000 jambo ambalo alikiri kuwa lilikuwa ni gharama kubwa.

Alisema kutokana na hatua hiyo, serikali ilichukua hatua kwamba kwa kila pampu nne za mafuta, ifungwe EFDs moja ili kuwapunguzia gharama wafanyabiashara. “Baada ya hatua hizi, serikali ikaagiza kwamba kuanzia Septemba 30, 2016 vituo vyote viwe vimefunga mashine hizo, lakini hawakuitikia agizo hilo,” alifafanua Alisema kwa kuweka mfumo wa mashine moja kuhudumia pampu nne ilikuwa ni lengo la kurahisisha gharama kwa wafanyabiashara hao.

Alisema kwa yule ambaye ana pampu 12 za mafuta anatakiwa kufunga mashine tatu tu za EFDs. “Haruhusu pampu zaidi ya nne kwa mashine moja, ukiunganisha zaidi ya pampu nne, uwezo wake unapungua, foleni ya kutoa risiti inakuwa kubwa ndio maana tukaona ziwe mashine nne ili risiti zitoke haraka na mteja apate haraka risiti yake na kuondoka,” alieleza Kamishna huyo wa TRA.


Alisisitiza kuwa kwa sasa hakuna tena changamoto ya bei na madai yao kwamba TRA imekurupuka sio ya kweli, kinachotakiwa wa wafuate sheria wakalipie mashine na tutawafungulia.

“Ndio maana tumesema kwamba tutamruhusu mtu ambaye ameshalipia aendelee na kazi.” Aliahidi kuwa TRA itawabana mawakala wanaosambaza EFDs watimize ahadi wanazozitoa za kufunga mashine ndani ya muda walioahidi. 


Alitoa mfano kuwa kufunga mashine kwenye kituo cha mafuta sio zaidi ya saa tatu. Hatua ya kufungia vituo vya mafuta ilianza kuchukuliwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango baada ya kufunga kituo kimoja cha GBP jijini Dar es Salaam mapema wiki iliyopita baada ya kukuta hakijaunganishwa na mashine ya EFDs.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: