MATAMSHI YA JOHN MNYIKA, PETER MSIGWA YA KUSEMA BUNGE DHAIFU HUZAA SERIKALI DHAIFU YAMKASIRISHA SPIKA WA BUNGE JOB NDUGAI DODOMA
Dodoma. Spika wa Bunge, Job Ndugai jana alionyeshwa kukerwa na maneno yaliyotolewa na wabunge wawili wa Chadema kuwa bunge dhaifu huzaa Serikali dhaifu.
Awali, mbunge wa Kibamba (Chadema) John Mnyika alinukuu kauli ya mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Peter Msigwa aliyoitoa bungeni mwaka 2002 kuwa bunge dhaifu huzaa Serikali dhaifu.
“Kinyume chake Serikali dhaifu husababisha bunge kuwa dhaifu na ndio hali tulionayo hivi sasa, bunge letu limefanywa dhaifu sana,” alisema Mnyika.
“Serikali hii ingekuwa na nguvu ingejiamini sana isingefanya bunge kuwa dhaifu lakini kwasababu Serikali ni dhaifu imefanya bunge pia kuwa dhaifu,” alisema Bunge hilo limekuwa dhaifu mpaka kufanya mkataba mmoja na itifaki mbili zinaletwa kwa siku moja.
“Wakati Bunge lenye nguvu lingesema leo tunajadili mkataba huu kesho mkataba huu, lakini kwa udhaifu huu wa Bunge unaoendelea tunaoijadili yote,” alisema.
Mnyika alisema kama wataruhusu Serikali na Bunge kuendelea kuwa dhaifu, ni wazi siku zote watapitisha mikataba lakini utekelezaji wake hautakuwapo. Akizungumza jana mara baada ya kipindi cha maswali na majibu, Spika Ndugai alisema kuwa kuna baadhi ya wabunge muda mrefu wanakuwa hawapo bungeni, lakini wakija huchafua hali ya hewa.
“Wenzetu ambao muda mwingi wanakuwa hawapo, wakija wanachafua hali ya hewa. Alisimama (mbunge) na kusema bunge hili ni dhaifu,” alisema.
Alisema kwa kanuni zake, hizo ndizo lugha za kuudhi kwa mbunge kuwaona wabunge wenzake kwa wingi wao bungeni kuwa hawana akili. “Kuna wenzetu wanasema Bunge hili ni dhaifu. Unapowaona wenzako waliochaguliwa ni dhaifu, lazima kuna matatizo. Huwezi tu hivihivi una akili timamu halafu ukawaona wenzako wote kundi la wajinga fulani,” alisema.
“Wewe una akili kuliko wao? Unatoa wapi maneno ya namna hii. Binadamu lazima uwe na staha ile ndogo kwa binadamu wenzako hata kama hukubaliani nao katika mawazo. Wabunge hao hao walikuwa wanamsema Rais Jakaya Kikwete ni dhaifu ndio hao wanasema kuwa Bunge hili ni dhaifu.
“Wakati mwingine utawala unaweza kuutengeneza mwenyewe na kuuharibu wenyewe kwa midomo yenu. Unasema utawala dhaifu unaanza kugangamala,” alisema.
Ndugai alihoji aliyefanya wagangamale nani kama sio mbunge mwenyewe (bila kuwataja majina) na mdomo wake.
“Mara mnakimbia huku huko na kule, mnafungua madudu gani sijui, hakuna kesi wala nini nasema mimi ndio Spika mwaka mzima mtu hakanyagi hapa,” alisema.
Akizungumzia kuhusu uletwaji wa miswada kwa hati ya dharura ambayo wabunge wa upinzani walipinga, Ndugai alisema wabunge ndio waliomchagulia watu wa kumshauri (Kamati ya Uongozi ya Bunge).
“Wajibu wangu si kukataa mambo juu kwa juu, nikilipata jambo napeleka katika kamati ya uongozi, tukiona jema tunalileta kwenu. “Tunaposhirikiana jambo tuitwe dhaifu. Kamati ina mamlaka ya kuishauri kamati ya uongozi...mfano hili lililokuja tunafanyaje?” alihoji.
Alisema pamoja na mambo mengine miswada hiyo inaboresha ushiriki na umiliki wa Watanzania katika masuala ya madini.
“Kuwa na hisa kuanzia asilimia 16 mpaka 50 kama tunavyolia siku zote. Hivi linapokuja suala la umiliki wa rasilimali zetu za asili waliozopewa na Mungu mimi Spika mlitaka nikatae...linakuja jambo ambalo madini yasiyo chenjuliwa hayasafirishwi tena nje ya nchi, nalo nilirudishe huko huko na kama yakisafirishwa walipe VAT (Kodi ya Ongezeko la Thamani),” alihoji Ndugai.
Pia, alihoji linapokuja jambo la kupunguza uwezo wa waziri, makamishna wa madini ambalo lilikuwa linaleta shida, sasa yanapunguzwa nalo alikatae.
“Si mlikuwa mnapiga kelele nalo nilirudishe huko huko eti ndo Spika mahili ama Spika makini. Pamoja na yote ni kuwa na heshima na mawazo ya watu wengine,” alisema.
“Hata majaji wanakaa jopo la majaji watatu, wawili wanaweza kuamua pamoja na mwingine kutofautiana na wenzake lakini wanaheshimu mawazo ya wengine.”
Alihoji mbona hasimami jaji mmoja (ambaye mawazo yake yamekataliwa) na kusema wenzake ni wapumbavu.
“Kama mtu hakuheshimu anakusemea mbovu kwanini umsikilize haiwezekani...kinacholeta matatizo ni tabia na lugha za humu ndani,” alisema.
Juzi, wakati akichangia maazimio ya Bunge, Msigwa alisema wabunge kuchelewa kupewa mikataba ili waisome kunaonyesha udhaifu kwa Bunge.
Msigwa alisema kitendo cha wabunge kuchelewa kupewa mikataba inayokuja kwa ajili ya kuridhiwa kinajionyesha jinsi Bunge ambavyo halitimizi wajibu wake.
“Hivi vifungu ukiwauliza wabunge wanavipitia saa ngapi? Kila siku itifaki zinapoletwa zinaletwa siku hiyo hiyo unavipitia saa ngapi? Unasoma saa ngapi? Tunapewa dakika tano kuchangia,” alisema.
Alisema hilo linaonyesha nguvu ya wabunge inapungua na kwamba inafanya kuwa Bunge haliwezi kusimamia Serikali.
Msigwa alihoji wabunge wamekuwa bungeni kama ‘rubber stamp’ (hawana maamuzi) na wakubaliane kuwa Bunge linaongozwa na Serikali. Alisema Serikali zote duniani huwa zinapenda kulifanya Bunge liwe kibogoyo ili ifanye mambo yake/Mwananchi
0 comments:
Post a Comment