BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

SERIKALI WASABABISHA VIPEPEO KUWATESA WAFUGAJI WA MUHEZA TANGA

Wafugaji wa vipepeo katika Hifadhi ya Amani Nature Reserve wamelizwa na zuio la Serikali la kusafirisha nje ya nchi wanyamapori hai kibiashara, huku wakidai kuzuiwa kwao kufanya biashara ya vipepeo kunawaweka katika wakati mgumu.

Wakizungumza na wahariri wa vyombo vya habari waliofanya ziara katika hifadhi hiyo iliyopo katika milima ya Usambara Mashariki mwishoni mwa wiki, wafugaji hao waliwaomba kuwasilisha kilio chao kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe ili asitishe zuio hilo wakisema biashara ya vipepeo nje ni tofauti na ya wanyamapori.

Meneja mradi wa vipepeo wa eneo hilo, Amiri Sheghembe alisema ufugaji ulianza mwaka 2003 na hadi sasa wapo wafugaji 156 ambao kabla ya kuzuiwa walikuwa wakiuza nje vipepeo vyenye thamani ya Dola 90,000 za Marekani, huku wakijipatia Sh500 milioni kwa mwaka.

“Kwa eneo la hapa Amani vijiji sita vinafuga aina 31 za vipepeo ambavyo vilikuwa vikipata soko katika nchi za Ulaya na Marekani kutokana na aina yake kuwa ya kuvutia zaidi kuliko vya ukanda wa Kenya na Asia,” alisema.
Alisema kabla ya kujumuishwa katika kundi la wanyama wasiotakiwa kuuzwa nje, Serikali ilistahili kufanya utafiti kwanza na kujiridhisha kwa kuwa mchakato wa kuanzia kufuga hadi kusafirisha nje huchukua muda mfupi na hata vikizuiwa vinaishia kufa.

Wakizungumza katika kitongoji cha Panusi kilichopo Kijiji cha Kisiwani, wafugaji hao walisema miaka mitatu iliyopita kabla ya Serikali kupiga marufuku biashara hiyo walikuwa wakijipatia fedha zilizowawezesha kumudu mahitaji yakiwamo ya ujenzi wa nyumba.

“Tangu Serikali ilipozuia biashara hii maisha yetu yamekuwa magumu, baadhi ya wanawake wametelekezwa, nyumba zilizokuwa zimeanza kujengwa zimesimama, vifo vya wajawazito vimeongezeka na hata kuwapa wanafunzi fedha za kujikimu shuleni hatuna,” alisema Mwanaisha Ali (56).

Alisema hakuna soko la ndani la vipepeo na mchakato wa kuanzia kufuga hadi kuvisafirisha nje ya nchi hauna madhara.

Wahariri kumfikishia waziri

Wahariri waliahidi watawasiliana na Waziri Maghembe na kumweleza jinsi wafugaji hao ambao wengi wao ni wanawake wa kipato cha chini walivyoathirika.

“Tutaonana na Waziri Maghembe haraka iwezekanavyo kumweleza athari za kuzuia biashara ya vipepeo kwa jamii ya kipato cha chini hapa Amani lakini pia namna Taifa linavyokosa fedha za kigeni kwa kuwa uzalishaji wake unatokana na juhudi za wafugaji wenyewe,” alisema mhariri wa gazeti la Jamhuri, Manyerere Jackton.

Mwenyekiti mstaafu wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda alisema ziara hiyo imewapa funzo kwamba licha ya kuwa zuio la Serikali la kuuza wanyama nje lilikuwa zuri, lakini lilitakiwa kuainisha aina kwa kuwa hadhani kama ilikuwa sahihi kuzuia biashara ya vipepeo. 


Hifadhi ya Amani Nature Reserve ni maarufu duniani kwa ufugaji wa vipepeo wa kila aina.Mwananchi
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: