Mwaka 1968, Jeshi la Korea Kaskazini (KPA), liliunda kikosi maalum cha makomando 31. Kikosi hicho kilipewa jina Kikosi 124 (Unit 124).
Makomando hao walipewa mafunzo maalum ya kutekeleza oparesheni ya kumuua aliyekuwa Rais wa Korea Kusini, Park Chung-hee.
Oparesheni hiyo ilipangwa kutekelezwa kwa siku 12, kuanzia Januari 17 mpaka 29, 1968. Siku ya nne ya oparesheni hiyo, yaani Januari 21, makomando wa Kikosi 124 wakiwa wanaelekea Ikulu ya Korea Kusini, Blue House, walivamiwa na jeshi la Korea Kusini. Makomando 29 waliuawa papohapo.
Makomando wawili wa Kikosi 124 walinusurika kifo. Mmoja, Sim Shin-jo, alikamatamwa, akashikiliwa mateka Korea Kusini. Aliachiwa baada ya mwaka mmoja, akiwa ameshatoa siri zote za KPA alizozijua na oparesheni ya Kikosi 124 aliyoitekeleza.
Shin-jo pia alichukua uraia wa Korea Kusini. Serikali ya Korea Kaskazini ilitafsiri kitendo hicho cha Shin-jo kuwa ni usaliti mkubwa kwa nchi yake. Adhabu ambayo walimpa ni kuiteketeza familia yake yote iliyobaki Korea Kaskazini. Hivyo, Shin-jo hana ndugu kabisa. Mwisho Shin-jo aliamua kuokoka na kuwa mchungaji.
Komando wa pili aliyenusurika kifo ni Park Jae-kyung. Huyu alifanikiwa kutoroka na kurejea Korea Kaskazini. Alipokelewa vizuri. Baadaye Jae-kyung aliteuliwa kuwa mkuu wa KPA kisha waziri wa Vikosi vya Majeshi ya Ulinzi wa Watu wa Korea Kaskazini.
KISASI
Baada ya Korea Kusini kujua siri za Unit 124 kupitia kwa Shin-jo, nao wakapanga kulipa kisasi.
Mwaka 1971, Idara Kuu ya Ujasusi Korea Kusini (KCIA), ilitoa mapendekezo ya kuundwa kwa kikosi ambacho kiliitwa 209th Detachment au 2325th Group. Hata hivyo, kikosi hicho hufahamika zaidi kama Kikosi 684 (684 Unit).
Jeshi la Korea Kusini likatekeleza mapendekezo hayo na Kikosi 684 kiliundwa. Jukumu la kikosi hicho lilikuwa kumuua aliyekuwa mtawala wa Korea Kaskazini, Kim II-sung.
Askari 31 walipewa mafunzo maalum jinsi ya kuingia Korea Kaskazini na kumuua II-sung. Askari hao walipelekwa kwenye kisiwa cha Silmido, ambako hakukuwa na nyumba yoyote.
Wakati wa mafunzo hayo, askari saba walifariki dunia, kwa hiyo wakabaki 24. Kipindi mafunzo yamekolea na askari hao wakiwa wameshakamilika tayari kwa utekelezaji wa mauaji hayo, lilitolewa agizo la Serikali kuwa mpango wa Kikosi 684 umefutwa.
Sababu ya kufutwa mpango huo ni kufuatia maelewano ya kidiplomasia kati ya Korea Kusini na Kaskazini kufikia hatua nzuri. Kipindi hicho Kikosi 684 kilikuwa bado kipo Silmido.
Agosti 23, 1971, makomando wa Kikosi 684 waliua walinzi wao pamoja na wahudumu, wakavuka Bahari ya Njano (Yellow Sea), wakateka basi na kupanda kuelekea mji mkuu wa Korea Kusini, Seoul.
Safari yao ikawa kuelekea Ikulu ya Korea Kusini, Blue House ili kumuua aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Park Chung-hee.
Vikosi vya Jeshi la Korea, vilikizingira Kikosi 684, katika eneo la Daebang-dong, Dongjack-gu, Seoul. Askari 20 wa Kikosi 684 waliuawa na wengine kujiua eneo la tukio, wanne waliobaki walihukumiwa kifo na walinyongwa Machi 10, 1972.
Mpaka leo swali limebaki ni sababu gani Kikosi 684 walitaka kumuua Rais Chung-hee? Huo ndiyo uasi wa kijeshi ambao haujawahi kubainika sababu yake.
MATOKEO
Serikali ya Korea Kusini ilinyamaza, haikutoa taarifa yoyote kuhusu makomando wa Kikosi 684.
Mwaka 2006, Korea Kusini iliamua kuvunja mzizi wa fitina kwa kueleza bayana kilichotokea kuhusu Kikosi 684.
Baada ya taarifa hiyo, familia za makomando wa Kikosi 684 waliipeleka Serikali mahakamani na kushinda kesi.
Serikali iliagizwa kuzilipa fidia familia za makomando wa Kikosi 684 kwa sababu makomando hao walipewa mafunzo makali bila tahadhari yoyote. Walivurugikiwa akili na kujaribu kufanya shambulio. Serikali badala ya kuwaelewa kuwa hawakuwa sawa, wakawachukulia kama waasi.
NINI UNAPATA?
Korea Kusini waliingia gharama kubwa zaidi walipojaribu kulipa kisasi. Walipoteza makomando wote 31. Chupuchupu Rais wao auawe. Zaidi, waliingia gharama ya kuendesha kesi na kunyonga kisha kulipa fidia familia za marehemu wote 31.
Adui yako akishindwa mpango wake mbaya juu yako, shukuru Mungu ambaye amekunusuru. Usijione umemzuia kwa nguvu na maarifa yako.
Ukijiona jabali na kupanga kulipa kisasi, unakuwa unamkosea Mungu aliyekulinda. Ni kukosa imani kuwa yupo kwa ajili yako na kwamba bila yeye usingepona.
Ukipanga kisasi hakitafanikiwa, mfano Korea Kusini, walichokozwa lakini hawakukubali, wakapanga kisasi. Na kisasi hicho kiliwagharimu.
Ukibaini mpango mbaya wa adui, amka utabasamu. Tabasamu lako limaanishe shukurani kwa Mungu anayekulinda. Baada ya hapo, ongeza umakini na Mungu ataubariki umakini wako. Usilipe kisasi. Kulipa kisasi ni kujiona unaweza kutenda kazi ya Mungu. Utashindwa!
Ndimi Luqman MALOTO
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
Home / kitaifa /
slider
/ SIMULIZI YA AINA YAKE ! ADUI AKISHINDWA MPANGO WAKE MBAYA, WALA USILIPE KISASI KWANI HUTAFANIKIWA
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment