BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

TP MAZEMBE FC YAFUZU ROBO FAINALI YA RWAKATARE CUP 2017 KWA MBINDE MOROGORO




Mbunge wa kuteuliwa kupitia CCM mkoa wa Morogoro, Mchungaji Dk Getruda Rwakatare.

Na Juma Mtanda, Morogoro.
Timu ya soka ya TP Mazembe FC imefuzu kwa mbinde na kutinga hatua ya robo fainali ya mashindano ya Rwakatare Cup 2017 kituo cha Mkamba katika mashindano hayo yanayoendelea kutimua vumbi katika vituo saba katika wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro.

Mashindano hayo yanaendelea kuchezwa kwenye vituo saba vya Mngeta, Mlimba, Namawala, Ifakara, Mkamba, Mang’ula na Chita ikishirikisha jumla ya timu 80 ambazo kila kituo itatoa mshindi wa kwanza na pili ili kupata timu 14 za kuwania ubingwa wa Rwakatare Cup 2017.

Akizungumza na MTANDA BLOG mjini hapa, Msimamizi wa kituo cha Mkamba, Clarence Msavila alisema kuwa kituo hicho tayari timu nane zimefuzu kucheza robo fainali lakini TP Mazembe ililazimika kupambana ili kupata nafasi katika mchezo wake wa mwisho kwa kupata ushindi.

Msavila alisema kuwa TP Mazembe FC yenye maskani yake kijiji cha Nyanga kata ya Msolwa Stesheni ilikumbana na vipigo kutoka kwa timu Serengeti Boys FC kwa kutandikwa bao 2-0 na kuambulia kipigo kingine kutoka kwa Maquapa FC kwa kufungwa idadi hiyi hiyo ya bao 2-0.

“TP Mazemba FC imefuzu robo fainali kwa bahati tu kwani ilianza vibaya kwa kupoteza michezo miwili, kutoa sare mchezo mmoja na kuja kupata ushindi mchezo wake wa mwisho kwa kuishinda bao 2-0 dhidi ya Mkamba B na kujikusanyia pointi nne zilizoisaidia kufuzu hatua hiyo.”alisema Msavila.

Timu nyingine zilizofuzu hatua hiyo ni pamoja na Kidatu Kijiweni FC iliyofuzu kundi A kwa kukusanya pointi 10, CDA FC ikitinga kwa pointi tisa, Mkamba Rangers FC pointi sita na Mwendokasi FC ikiwa na pointi nne.

Nyingine zilizofuzu kutoka kundi B ni Maquapa FC iliyopata pointi 10, Chicago FC pointi tisa, Serengeti Boys FC point inane na TP Mazembe FC ikikusanya pointi nne ambapo michezo ya robo fainali itaanza agosti 19 hadi 22 mwaka huu kusaka timu za kuingia nusu fainali.alisema Msavila.

Katika kituo cha Mngeta, timu ya Supare Mahakama ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mngeta Rangers FC kwa kuifunga katika mchezo wa robo fainali na kutinga nusu fainali katika kituo hicho.

Bao pekee la Super Mahakama FC lilifungwa na Peter Magwala dakika ya 70 huku leo ikichezwa robo fainali nyingine kati ya City Boys FC itayoonyeshana ubabe na Stone Fire FC kwenye uwanja wa Lukolongo.

Kwa upande wa kituo cha Namawala, timu Warred Jamaica FC ilifungua panzia mbele ya Idandu FC ambapo Warred Jamaica FC iliibuka na ushindi wa bao 2-0.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: