Afisa wa jeshi la polisi akiwa na silaha katika picha ya mtandao.
Juma Mtanda, Morogoro.
Watu wawili wameuawa kwa kufyatuliwa risasi na askari polisi baada ya kutokea kwa vurugu zilizopelekea ng’ombe zaidi ya 40 kuuawawa kufuatia kuibuka kwa vurugu hizo kati ya wafugaji na wakulima katika kijiji cha Nyalutanga kata ya Kisaki wilaya ya Morogoro.
Vurugu hizo zilitokea Septemba 18 mwaka huu saa 7 mchana katika eneo la ofisi za serikali ya kijiji hicho na kusababisha mkuu wa mkoa huo, Dk Steven Kebwe na wasaidizi wake kukesha kijijini humu kusaka suluhu.
Wakizungumza kwa njia ya simu na MTANDA BLOG mjini hapa, Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Nyalutanga kata ya Kisaki mkoani Morogoro, Said Athaman Masongele alisema kuwa vurugu hizo zimetokea baada ya mifugo ya wafugaji kuingia kwenye mashamba bonde la Kikwato kisha kukamatwa na askari mgambo na walinzi wa sungusungu.
Masongele aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Ramadhan Kiwenge na Kibwana Msipwile na maiti zao kuhifadhiwa katika zahanati ya kijiji cha Nyaluhanga huku Ismail Msagule akijeruhiwa kwa kupigwa risasi katika makalio na kulazwa kwenye zahanati hiyo.
“Tukio hili limetokea jana saa 7 mchana na watu watatu wamepigwa risasi na kati yao wawili wamekufa na mmoja ameejeruhiwa katika makalio, maiti na majeruhi walipelekwa zahanati ya kijiji cha Nyalutanga.”alisema Masongele.
Aliongeza kwa kusema jana (juzi) viongozi wa kijiji hicho walikuwa kwenye kikao cha kujadili mambo mbalimbali ikiwemo bima ya afya baada ya taarifa za mifugo kuvamia mashamba walitumwa mgambo kwenda kukamata na muda mchache alipokea simu ya kujeruhiwa kwa Mohamed Kassim aliyejeruhiwa kichwani na mfugaji wakati wa kukamata mifugo.
Kwa upande wa askari mgambo wa kijiji cha Nyalutanga, Kibwana Haji Mbegu alisema kuwa kufyatuliwa kwa risasi kwa watu watatu kumetokana na askari kuchukua jukumu la kujihami baada ya kutokea vurugu na wananchi kutaka kumnyang’anya silaha.
“Tumekamata mifugo isiyopungua 80 katika mashamba ya Kikwato wakati wakila mazao na wakati tunakamata mifugo ile mwenzetu mmoja alijeruhiwa kwa kupigwa fimbo kichwani na mfugaji lakini tuliwazidi nguvu wale wafugaji na kuswaga ile mifugo hadi katika ofisi za kijiji kwa hatua za kisheria.”alisema Mbegu.
Baada ya vurugu hizo ng’ombe 35 waliuawawa huku ng’ombe zaidi ya 40 wakijeruhiwa kwa kukatwa miguu na sehemu mbalimbali ya miili yao hali iliyopelekea kushindwa kutembea.
Mbegu alisema kuwa baada ya dakika chache, wafugaji walifika ofisi za kijiji wakiwa na silaha za jadi wakati huo wananchi wakiwa wanakusanyika kwa uwingi huku kukiwa na askari polisi mmoja aliyebeba silaha kulinda amani eneo hilo.
Mbegu aliongeza kwa kusema baada ya wafugaji hao kufika eneo hilo, walianza kuchukua mifugo kwa nguvu jambo lililomfanya askari polisi afyatue risasi hewani kwa lengo la kuwatawanya lakini zoezi hili halikufua dafu.
“Wale wafugaji walimfuata askari kwa lengo la kumpokonya silaha huku wananchi wakiwarushia mawe wafugaji na kutengeneza makundi mawili, kundi mmoja lenye wafugaji lilimsonga askari huku kundi la wananchi likiwarushia na kufyatua risasi mbili zilizowalenga marehemu.”alisema Mbegu.
Wananchi walipandwa na hasira kwanza, mazao kulimwa na mifugo lakini wafugaji kumjeruhi mtu na kuchukua mifugo kwa nguvu mbele ya askari jambo lililowakasirisha na kuwarushia mawe wafugaji na kumtaka askari kuwazuia kwa kuwafyatulia risasi.aliongeza Mbegu.
Mbegu alisema kuwa baada ya watu wawili kupigwa risasi askari huyo alikimbia eneo hilo lakini kundi la wananchi lilimfukuza na kusimama kisha kufyatua risasi nyingine iliyompata Ismail Msagule na kumjeruhi kwenye makalio.
Askari huyo alijificha ndani ya nyumba na kupiga simu kituo cha polisi Kisaki Gomero kuomba msaada na askari wenzake kumuokoa eneo ambalo tayari wananchi wamezingira nyumba hiyo.
Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro, Maisha Maganga alisema kuwa kupigwa kwa risasi kwa watu watatu kijiji cha Nyalutanga kata ya Kisaki wilaya ya Morogoro kumetokana na vurugu zilizojitokeza kati ya wafugaji kukamatwa mifugo yao ilikuwa ndani shamba la mmoja wa wakulima kijijini hapo.
Maganga alisema kuwa askari alilazimika kufyatua risasi kama njia ya kujilinda yeye na silaha baada ya wananchi waliokuwa wanamshurutisha askari huyo kuwafyatulia risasi wafugaji waliokuwa wanaondoa mifugo ofisi za kijiji hicho baada ya kupata suluhu na uongozi wa kijiji.
"Ni kweli watu watatu walifyatuliwa risasi na askari na kati ya hao wawili walikufa na mmoja kujeruhiwa kutokana na vurugu zilizojitokeza baada ya mifugo kukamatwa na kufikiwa suluhu ya mwenye mifugo lakini wananchi walimtaka askari afyatue risas kuwapiga wafugaji hao kabla ya kumvamia na yeye kujihami kwa kuwafyatulia risasi"alisema Kaimu Kamanda.
Maganga alisema kuwa wafugaji watatu wamekamatwa akiwemo mmiliki wa mifugo hiyo, Kilako Msando, Agnes Madinda na Ngulumbashi Mwingwa huku jeshi la polisi likiwasaka wananchi waliohusika kuwajeruhi na kuwaua ng'ombe hao.

0 comments:
Post a Comment