Magonjwa ya kuku ni mengi wakati wa mvua kuliko kiangazi
Wakati nchi zilizoko ukanda wa Afrika Mashariki zikipokea mvua nyingi, kuna maeneo yameanza kuingia katika hali ya majira ya kiangazi.
Ilivyo ni kuwa hali ya hewa ina uhusiano wa moja kwa moja na magonjwa ya kuku, hivyo wafugaji wawe na tahadhari katika kukinga kuku wao wasidhulike na magonjwa.
Magonjwa mengi huambukizwa kwa njia ya hewa, maji na chakula. Ikumbukwe hewa, maji na chakula ndiyo mahitaji muhimu kwa kuku.
Wafugaji hupata hasara na taharuki ya kupoteza mifugo yao na pesa walizotumia kuwekeza miradi yao hiyo.
Ukijua sababu au chanzo cha maambukizi kwa kuku wako na njia ambayo ugonjwa unaingia kushambulia mifugo yako, huna budi kusema umepiga hatua.
Ili ugonjwa utokee lazima mazingira yaruhusu maambukizi kutokea. Bila hivyo ugonjwa hauwezi kuingia eneo hilo hata kama upo maeneo mengine.
Aina ya magonjwa.
Magonjwa yanayosababishwa na vimelea aina ya bakteria: Magonjwa haya yana dawa na yanatibika. Kwa mfano, ugonjwa wa kipindupindu cha kuku na salmonella au mharo mweupe ni magonjwa ambayo hushamiri sana wakati wa mvua.
Kuku hudhoofika, kuharisha, kupumua kwa shida, kupoteza hamu ya kula na hatimaye kufa kama hawapati huduma ya haraka.
Wafugaji wengi husubiri kuona dalili za ugonjwa ndipo wanachukua hatua kudhibiti. Inatakiwa kujua mazingira yenye kuleta magonjwa na kudhibiti kwani kusubiri dalili ni kusubiri janga kubwa.
Unaposhughulikia ugonjwa wa bakteria ama kwa njia ya usafi au kwa dawa, ni vizuri kutumia dawa yenye kutibu walau magonjwa zaidi ya moja ili kuondoa hata ugonjwa ambao dalili zake zimemezwa na ugonjwa unaoonekana.
Magonjwa ya virusi.
Ugonjwa wa kwanza ni Gumboro; ugonjwa huu husababishwa na virusi ambao hushambulia kuanzia kuku wenye umri wa wiki tatu hadi 18.
Ugonjwa huu hauna tiba ila kuku hukingwa kwa njia ya chanjo ambayo hupewa kuku wakiwa chini ya umri wa kuugua. Kinga yake ikitolewa sawa sawa inatosha kukinga maisha yote ya kuku.
Ugonjwa wa pili wa virusi ni Ndui ya kuku (fowl pox). Ugonjwa huu hauna tiba na kuku hukingwa kwa njia ya chanjo ambayo hutolewa kuku wakiwa na umri wa wiki sita hadi tisa au chini ya umri huo endapo kuna viashiria vya mbu au wadudu wengine wenye tabia za kunyonya damu kwa kuku.
Mbu huchangia ugonjwa kusambaa, hivyo kuku wanaweza kupata ugonjwa mapema wakiwa wadogo. Hakikisha hakuna maji yaliyotuama jirani na makazi ya kuku ili mbu wasizaliane. Pia, ukiona mazingira haya toa chanjo mapema kabla ya wiki ya sita ili kukinga maambukizi kwa tahadhari.
Dalili za ndui zinaonekana kwa kutoa vipele vyeusi kichwani sehemu zenye uwazi bila manyoya, utando mweupe kwenye ulimi lakini sio rahisi kuona dalili hizi kwa vifaranga wenye umri chini ya wiki nne kutokana na hali yao ya uchanga.
Kuku hupata homa kali kutokana na ugonjwa, huku vifaranga wakifa na wengine kuwa vipofu pindi vipele vinapotokea machoni.
Chanjo moja ikitolewa sawa sawa inatosha kuwakinga kuku maisha yao yote.
Ugonjwa wa tatu wa virusi ni Kideri (New castle disease) Ugonjwa huu hauna tiba na kuku hukingwa kwa chanjo ambayo hutolewa mapema siku saba baada ya vifaranga kuanguliwa. Kinga dhidi ya ugonjwa huu hushuka mara kwa mara.
Kuku wanahitaji kupewa chanjo kila baada ya miezi miwili au mitatu hadi maisha yao yatakapokoma. Ugonjwa huu huambukizwa hasa kwa njia ya hewa inayosambaa zaidi wakati wa kiangazi na majira ya upepo mkali.
Hiki ndicho kipindi ambacho watu wengi huita pepo za msimu mbaya kwa kuku. Ugonjwa huu ni hatari kwani huharibu na kushusha kinga ya mwili kwa magonjwa mengi ya bakteria na protozoa ambayo huongeza kazi ya kuua kuku.
Ugonjwa wa Kideri hautokani na upepo mbaya, bali ni vimelea wenye kushamiri wakati huo wa kiangazi na upepo ndiyo njia yao kusambaa.
Jipange kutoa chanjo mara kwa mara hasa kipindi cha kuhama kutoka masika kuingia kiangazi. Zuia kuku wako kuzagaa ovyo kwenda kwa majirani na epuka kununua kuku kutoka sehemu nyingine kwani utaingiza ugonjwa na kuku wako wataisha.
Ugonjwa mwingine ni kuhara damu unaosababishwa na vimelea aina ya protozoa na sio bakteria. Kuku huharisha damu, kupoteza hamu ya kula, kudhoofika na kufa ghafla kwa kujirusharusha kama amechinjwa.
Dawa zenye salfa hutibu haraka kuku wakiwa kwenye hali hii. Epuka unyevunyevu bandani au maranda kuganda.
Mwisho ni minyoo. Minyoo sio ugonjwa bali husababisha upungufu kutokana na kunyang’anyana chakula na kuku.
Minyoo huzaliana sana wakati wa mvua. Kuku hupata minyoo wakati huo kutokana na tabia yao ya kula vitu kutoka kwenye udongo.
Minyoo inatibika kwa dawa ambazo hutolewa kila baada ya miezi miwili au mitatu.
Dalili za minyoo kwa kuku ni pamoja na kuona minyoo kwenye kinyesi cha kuku, kuku kukohoa mara kwa mara, kupungua uzito au kupunguza uzalishaji kwa kuku wanaotaga.
Njia bora ya kudhibiti magonjwa nyakati zote ni usafi wa mazingira, vyombo vya maji na chakula.
Pia, kutoa chanjo kwa kufuata kalenda ya ugonjwa husika, hewa safi na nafasi ya kutosha bandani.
Hakikisha unawapa kuku chakula cha kutosha chenye ubora wa kuweza kuwapa kinga ya asili dhidi ya magonjwa na kuepuka kununua ovyo kuku na kuwaigiza bandani kwako.Mwananchi
0 comments:
Post a Comment