SERIKALI YASTUSHWA NA DENI LA TAIFA BAADA YA KUFIKIA KIWANGO CHA KUTISHA
Waziri Mkuu wa Malaysia Dk Mahathir Mohamad.
Putrajaya, Malaysia. Waziri Mkuu wa Malaysia Dk Mahathir Mohamad amesema Deni la Taifa la Malaysia limefikia kiwango cha kutisha cha RM1 trilioni (sawa na Sh 575 trilioni) na kwamba hatua madhubuti lazima zichukuliwe haraka ili kudhibiti.
Dk Mohamad ambaye alichaguliwa hivi karibuni alisema kwamba nchi ilizoea kuwa na deni la RM300 bilioni alipokuwa waziri mkuu lakini limepanda kiasi cha kutisha.
"Lakini sasa, deni letu limefikia zaidi ya trilioni na tunapaswa kupata ufumbuzi wake," alisema katika mkutano wa kila mwezi wa Baraza la Wafanyakazi chini ya Idara ya Waziri Mkuu.
Dk Mahathir alisema mabadiliko kadhaa yanatakiwa kufanyika na kwamba ana uhakika hilo litawezekana kwa msaada wa watumishi wa umma.
Dk Mohamad, 92, aliyestaafu baada ya kuongoza kwa miaka 22 alisababisha tetemeko la kisiasa alipogombea kupitia chama cha upinzani kilichoshinda na kumwondoa waziri mkuu Najib Razak aliyechafuka kwa kashfa.
Ushindi wa Mahathir kupitia muungano wa upinzani ulihitimisha utawala wa muungano wa Barisan Nasional ulioongoza tangu nchi ilipopata uhuru kutoka kwa Uingereza mwaka 1957.
"Tunajiamini kwamba tunaweza kukabiliana na changamoto zilizopo lakini tunahitaji watumishi wa umma ambao ni madhubuti na wanaoaminika kufanikisha mabadiliko tunayotaka,” alisema Dk Mohamad.Mwananchi
0 comments:
Post a Comment