
Magonjwa ya afya ya akili yanaendelea kuitesa jamii huku baadhi yake yakiangukia kwenye unywaji wa pombe kupita kiasi, uvutaji bangi na matumizi ya dawa nyingine za kulevya.
Wataalamu wa afya wamebaini kuwa siyo watu wote wanaovuta bangi na kunywa pombe kupita kiasi hupenda kufanya hivyo, wengine hulazimika kutokana na maradhi ya afya ya akili.
Mtaalamu wa kitengo cha afya ya akili wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk Saidi Kuganda anasema maradhi hayo yanaweza kumsababisha mtu kutumia mihadarati na kunywa pombe.
“Unajua akili inapopata shida mhusika husikia kelele kichwani na hutafuta mbinu za kukabiliana na hali hiyo. Akibaini akinywa pombe hatazisikia, basi hukimbilia kunywa na akibaini kuwa akivuta bangi hatasikia karaha au usumbufu anaoupata, basi atakuwa anavuta na atafanya hivyo kila anapohisi kupata shida hiyo,” anasema Kuganda.
Anasema mara nyingi wanaume ndiyo hukimbilia mbinu hizo ukilinganisha na wanawake ambao wengi wao hufikishwa hospitalini kwa ajili ya matibabu.
Dk Kuganda anafafanua maana ya magonjwa ya afya ya akili na kusema, ni yale yanayoathiri uwezo wa mtu kufikiri, kuhisi, kutambua na kutenda katika utashi wake.
“Hivyo mgonjwa anakuwa na tabia au mwenendo ulio tofauti au usioendana na jamii husika kiimani, kimila na desturi,” anabainisha mtaalamu huyo.
Anasema ikitokea mtu amevuta bangi ikamchanganya akili akafikishwa hospitalini akiwa amefungwa kamba hukaa naye akipatiwa huduma ya kwanza hadi pale nguvu ya bani itakapokwisha.
“Kama ni mvutaji wa kawaida nguu ya bangi ikiisha anakuwa sawa na anaruhusiwa kurudi nyumbani na jambo hilo ni kawaida kabisa, lakini akiwa anavuta kwa sababu ya matatizo ya akili hata nguvu ya bangi ikiisha anakuwa hayupo sawa na hafanyi vitu vya kawaida, ”anasema.
Mtaalamu huyo anasema bahati mbaya ni asilimia 40 ya watu wenye maradhi hayo hufikishwa hospitali, tofauti na hapo unyanyapaa husababisha wengi wao kukimbia na kuingia mitaani.
Kauli ya Dk Kuganda inaungwa mkono na makala iliyochapishwa kwenye jarida lijulikanalo kama Journal American Psychiatry la nchini Marekani, iliyoeleza kuwa matumizi ya pombe na dawa za kulevya mara nyingi hutumiwa kukabiliana na hali mbalimbali za afya ya akili, ikiwa ni pamoja na kutojitambua.
“Watu wengi wanaopata shida ya maradhi ya akili hushindwa kukabiliana nayo na hutafuta liwazo la hali hiyo, mwisho huangukia katika matumizi ya pombe na dawa za kulevya,” anasema mtaalamu wa afya, Dk Robert Freedman.
Freedman ambaye ndiye mhariri mkuu wa jarida hilo, anasema hata hivyo siyo kila anayekunywa pombe na kutumia dawa za kulevya anakuwa anapigana na matatizo ya akili, “Wapo wanaotumia kwa utashi wao tu,” anasema.
Chanzo cha maradhi ya akili.
Akizungumzia sababu za watu kuugua magonjwa ya akili, Dk Kuganda anasema zipo sababu za kibaolojia, maradhi ikiwamo Ukimwi, kifua kikuu na uraibu.
“Wengine tangu wamezaliwa vipashio vya mwili havijakaa sawa (neurotransimitters) ambavyo kazi yake ni kupasha habari wakati mwingine vinakuwa na tatizo, hivyo vinamuweka mtu katika hatari ya kupata maradhi ya afya ya akili,” anasema.
Anasema maradhi kama Ukimwi, malaria na kifua kikuu huweza kumuathiri mtu kulingana na namna atakavyoyapokea na kukabiliana nayo.
“Maradhi yanasababisha kimoja miongoni mwa maradhi ya afya ya akili ambacho ni msongo. Kwa mfano, mtu mwenye presha akifurahi inapanda, akichukia inapanda, asiposamehe inapanda, hivyo anakuwa kwenye hatari ya kupata maradhi ya afya ya akili,” anasema.
Anaitaja sababu nyingine kuwa ni ya kisaikolojia. “Kila binadamu ana nafsi, mambo ya kiroho ambayo hayashikiki yanavyofanya kazi kama huna nafsi wewe siyo mtu, hiyo nafsi huwa inalelewa kuanzia tumboni hadi kukua ili kutambua mambo, kutafsiri mazingira yake na kukabiliana na changamoto za maisha kama vile watu wanavyotaka ukabiliane nazo.
“Ikishindikana kukabiliana na masuala hayo inaonyesha ni kwa jinsi gani huyo mtu hayupo sawa.
“Kwa mfano jinsi mtu anavyokabiliana na misiba, kukosa kazi, hivyo kama saikolojia yake tangu anakuwa haikulelewa vizuri atakuwa kwenye hatari ya kupata maradhi ya afya ya akili, ”anasema.
Mtalaamu huyo anasema mazingira yana mchango mkubwa kuleta shida ya akili kwa sababu karibu watu wote ili waishi lazima waingiliane na mazingira lakini siyo rafiki sana na yana changamoto zake.
Changamoto.
Dk Kuganda anasema changamoto duniani kote zinatoka kwenye mazingira. Anaeleza kuwa umasikini kupita kiasi ni changamoto ngumu kuikabili kisaikolojia, lakini wanaoweza kukabiliana nayo wanaishi kitajiri kuliko matajiri wenyewe.
“Hivyo umasikini ni jinsi ambavyo mhusika anautafsiri, kila mmoja anavyotafsiri umasikini inawezekana mtu ana vitu ambavyo mwingine hana na akajiita masikini akapata msongo wa mawazo na hata kutamani kujinyonga, ” anasema Dk Kuganda.
Dk Kuganda anaitaja changamoto nyingine kuwa ni migogoro isiyokwisha kwenye jamii inayomzunguka, kazini, nyumbani na kwenye nyumba za ibada.
Anasema pia katika jamii ambayo inaamini mwanamke asipoolewa hana maana na haheshimiki ni changamoto .
Mtalaamu huyo anasema changamoto nyingine ni aina ya maisha ikiwamo ulevi, ulaji usiozingatia taratibu.
Aina za maradhi ya afya ya akili.
Dk Kuganda anazitaja dalili kuu mbili za maradhi ya afya ya akili akisema zinatofautishwa na mambo mawili.
Jambo la kwanza ni kufanya mambo yasiyo ya kawaida makubwa na yasiyo ya kawaida lakini madogo.
“Kwa mfano, mtu mzima anacheza ngoma hadharani, ameweka nguo kichwani badala ya kuzivaa, mwingine anacheka peke yake,” anasema.
Dalili zake
Anazitaja dalili kubwa tano za maradhi ya afya ya akili ikiwamo kuhisi, kugusa, kuona, kusikia na kunusa.
Wapo wanaohisi kuwashwa, kutembewa na vitu ambavyo havipo au kuhisi anakimbizwa.
Anasema kuna watu wengine wakila chakula huhisi harufu tofauti na iliyopo muda wote wakila wanatema.
Anaongeza kuwa hisia potofu ni pamoja na imani za ajabu ambazo haziendani na mila, tamaduni au desturi za jamii kama vile yeye ni mtu maarufu, au anaamini kuwa yeye ni nabii au bila yeye hakuna kitakachofanyika.
Dk Kuganda anasema mtu huyo anaweza kusikia watu wanamzungumzia, redio au runinga zinaiga mambo anayopaswa kuyafanya yeye na hata kupiga kelele kuwa kuna mtu usalama wa taifa anamkimbiza.
“Anaweza kusema fulani ananiroga, hilo halina shida lakini ili ujue kuwa akili ina shida matendo atakayoyafanya kuhusu madai hayo ndiyo yatakupa jibu kuhusu utimamu wa akili yake,” anasema.
Mtalaamu huyo wa afya anasema wapo wanaohisi kuwashwa na kutembewa na vitu ambavyo havipo.
“Kwa mfano wanaotumia mihadarati muda wote wanajikuna kama kuna vitu vinawatembea, kiuhalisia hakuna kitu kinachowatembea wala kuwawasha.
“Wengine huhisi ladha tofauti na ndiyo maana wakila chakula huhisi harufu tofauti na iliyopo, muda wote wakila wanatema,” anasema Dk Kuganda.
Kwa watoto
Dk Kuganda anasema yapo, lakini mara nyingi husababishwa na watu wengine. Anasema watoto huathiriwa na maisha ya familia wanazoishi jambo linalosababisha akili yao kupata shida na kuchanganyikiwa.
“Ukiachilia wale waliozaliwa hivyo kwa sababu za kibaiolojia kama nilivyosema hapo mwanzo, watoto walio wengi familia zao huwasababishia kupata maradhi haya,” anasema Dk Kuganda.Mwananchi

0 comments:
Post a Comment