Saa 10 za mjamzito kituo cha polisi hadi kujifungua Morogoro.
Morogoro. Saa kumi ambazo Amina Mbunda, mkazi wa Morogoro, Mang’ula alitumia akiwa mahabusu ambako aliumwa uchungu na kisha kujifungua zimeibua mjadala mkubwa katika jamii.
Mjadala ulioibuka ni jinsi alivyokamatwa kwa kosa la mumewe, alivyokosa msaada pale alipoumwa uchungu hadi kujifungua kwenye majani, nje ya kituo cha polisi cha Mang’ula, alfajiri ya Juni Mosi.
Kwa maelezo yake, Amina alisema aliwekwa mahabusu Mei 31 kwa madai kuwa mumewe, Abdallah Mrisho alinunua kitanda cha wizi.
Akizungumza na mwandishi wetu aliyekwenda nyumbani kwa Amina, eneo la Kiswaswa, Kilombero juzi, mama huyo huku akiwa amekumbatia kichanga chake cha siku saba alisema siku hiyo saa saba mchana akiwa nyumbani kwake alikuja mgambo aliyemuulizia mumewe na kumjibu kuwa hakuwapo.
Alisema mgambo huyo, aliacha ujumbe kuwa atakaporudi akaripoti kituo cha polisi, “Ilipofika saa kumi na moja jioni alikuja askari anaitwa Andrew Mapunda akiwa ameambatana na Mwenyekiti wa Kijiji cha Mgudeni, Iddi Magunila na mtu mwingine ambao walitaka kufanya upekuzi.”
Amina alisema kwamba aliwaeleza kuwa mumewe yupo safarini kikazi lakini walilazimisha kuingia ndani ili kuangalia kitanda.
Alisema watu hao waliingia ndani wakiwa na mtu anayedai kuibiwa kitanda na kudai kukuta baadhi ya mbao za kitanda kilichoibwa.
“Wakaanza kukifungua na askari wakaniambia kwa kuwa mume wangu hayupo basi niende kituoni hadi atakapojitokeza. Nilimwambia naumwa na hali yangu anaiona lakini askari akasema nikikataa nitaenda kinguvu,” alisema.
Aliongeza, “Niliomba wampigie simu mume wangu na waliongea naye, akawaomba wasiondoke na mimi kwani naumwa lakini walimkatalia.”
Alisema polisi walimchukua na kwenda naye hadi kituoni na akawekwa mahabusu.
“Ilipofika saa mbili usiku alikuja mkuu wa kituo kuniona akaniuliza kwa nini wamenileta pale nikiwa katika hali ile? Mkuu wa kituo akasema, ‘bora mngemchukua mume wake, asije akazalia hapa kituoni.’ Akanipa pole na kuondoka,” alisema.
Alisema baada ya mkuu huyo kuondoka, askari wa zamu alifika kumuangalia na kumuuliza kwa nini halali, “Nikamjibu kuwa najisikia vibaya naumwa, akaniambia nilale hadi asubuhi labda ndugu zangu watakuja kunitoa.” Alisema ilipofika saa tisa usiku uchungu ulikazana akashindwa kukaa, “Nilimuita askari mmoja anaitwa Sele, nikamwambia anisaidie kunipeleka kituo cha afya. Wakati huo ilikuwa ni saa tisa usiku. Alitoka nje na kuwaambia askari wa zamu kuwa uchungu umemzidi.
“Saa tisa inaenda saa 10 wakaanza kutafuta usafiri na kunitaka nipande bodaboda lakini ilishindikana nikajifungua hapo nje kwenye majani,” alisema na kuongeza:
“Nikasema Mungu wangu kama nimenusurika mie basi tena mtoto sina maana alidondokea chini kwenye majani nilikuwa sina kitu chochote wala mtu yeyote wa kunisaidia mpaka najifungua.”
Amina ambaye ana watoto wengine wawili, alijifungua mtoto wa kike mwenye uzito wa kilo3.5.
Baada ya kuona hali imekuwa hivyo, polisi walimwamsha mwanamke mmoja anayeishi jirani na kituo cha polisi, aliyefahamika kwa jina la mama Eneriet Kipengula ili kumsaidia Amina.
“Alikuja na kumfunika mtoto kwa sababu wakati huo hatukuwa na nguo, wakanichukua na kunipeleka kwa daktari wa eneo hilo,” alisema.
Dk huyo aliyefahamika kwa jina la Lugusha aliwasaidia kufunga kitovu na akawataka waende kituo cha afya.
Alisema iliwalazimu kutumia usafiri wa bodaboda kwa kuwa alieleza kwamba gari la polisi lilikuwa bovu.
“Saa kumi na moja alfajiri tulifika kituo cha afya na kumkuta muuguzi aliyetusaidia kukata kitovu na kumchoma mtoto sindano na tukalazwa kwa siku tatu, kuanzia Juni mosi hadi tatu” alisema.
Amina alisema hali yake na ya mtoto zinaendelea vizuri isipokuwa ana maumivu makali ya kiuno.
Akizungumzia tukio hilo hilo, Mrisho ambaye ni mume wa Amina alisema, “Kuhusu kitanda ni kweli nilinunua kwa fundi kwa Sh160,000 lakini sikujua kama ni cha wizi.”
Aliiomba Serikali kuangalia kanuni za polisi za ukamataji wa raia na kutaka haki itendeke kwa kile alichofanyiwa mkewe.
Akizungumzia sakata hilo, Diwani wa Mwaya anapoishi Amina, Adamu Sungura alisema anashangazwa na askari kumpekua mama huyo bila askari wa kike kuwapo.
“Kimaadili hawakufanya vyema, pia unawezaje kumkamata mjamzito katika hali hiyo?” alisema.
Magunila alikiri kwenda nyumbani kwa Amina kwa ajili ya kumtafuta Mrisho, “Kivumbi ilikuwa pale kwenye kuondoka kwani mama kwa hali yake aliomba kutoondoka lakini askari aligoma. Mimi nilichukua jukumu la kumpigia mumewe na kumweleza hali halisi.”
Magunila alisema baada ya polisi kushinikiza kuondoka na Amina, alimwambia (Amina) aepushe shari na akubali kwenda kituoni.
Kamanda: Sheria haizuii
mjamzito kukamatwa lakini...
Akizungumzia suala hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei alisema hakuna sheria inayokataza mjamzito asiende kituoni au mahakamani. Hata hivyo, akasema polisi walitakiwa kuangalia mazingira.
“Ila ukielewa mazingira ya tukio unaweza kumruhusu akaendelea na shughuli zake kulingana na hali ilivyo wakati anakamatwa,” alisema kamanda.
Hata hivyo, Kamanda Matei alisema baada ya Amina kuonyesha dalili za uchungu, askari walimsaidia kumpeleka kituo cha afya kwa usafiri wa pikipiki kwa sababu gari la polisi ni bovu.Mwananchi
0 comments:
Post a Comment