Juma Mtanda, Morogoro.
Morogoro. Watoto wa kitanzania wametakiwa kujenga ujasiri kwa kupaza sauti pindi wanapoona kuna viashiria vya unyanyasaji na vitendo vya ukatili dhidi yao kutoka kwa baadhi ya wazazi, walezi na watu wengine ili tabia hizo zisiendelee kuota mizizi.
Usiri na ukimya umekuwa ukitoa nafasi kwao kukandamizwa na kupelekea kuwarudisha nyuma kimasomo, kuathiri akili na msongo wa mawazo baada ya kutendewa matukio hayo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni maalumu ya kutetea haki za watoto na vijana Manispaa ya Morogoro jana, Mkurugenzi wa idara ya shule ya taasisi ya Pamoja Youth Organization (PAYO) Dar es Salaam, Paul Gregory amesema kuwa watoto wanapaswa kuwa na ujasiri wa kufichua viashiria vya uvunjifu wa haki zao na vitendo vya ukatili.
Gregory amesema kuwa watoto wa kitanzania imefikia wakati wa kuiga kitendo cha mtoto mwenzao, Anthony Petro (10) mkazi wa Ngara aliyemzuia baba yake asiuze nyumba yao wanayoitegemea kwa kufichua jamo hilo kwa jeshi la polisi na kusaidia usitishaji wa uuzaji hivi karibuni.
“Anthony ni mwanafunzi wa darasa la kwanza kule Ngara mkoa wa Kagera na ameweza kujenga ujasiri mkubwa kwa kumzuia baba yake asiuze nyumba baada ya kwenda kituo cha polisi na kutoa taarifa ya baba yake kutaka kuuza nyumba yao wanayoitegemea.”alisema Grogory.
Grogory amesema kuwa vitendo vingi vya uvunjifu wa haki za watoto hufanywa na watu wa karibu hivyo ni vyema watoto wenyewe kuanza kupasa sauti ili jamii isaidie ikishirikiana na vyombo vya sheria kama alivyofanya Anthony.
“Siku hizi matukio mengi ya ukatili dhidi ya watoto yamekuwa yakiripotiwa kwenye luninga, redio na magazeti tofauti na zamani hivyo mkiona kuna dalili za mtu kukufanyia ukatili, kaseme jambo hilo kwa mtu mwingine atasaidia kukunusuru.”alisema Grogory.
Mwanafunzi wa darasa la nne shule ya msingi Pamoja ya Bonyoko Dar es Salaam, Mwasiti Hemes (10), amesema kuwa wana kila sababu ya watoto na vijana kuwa wajasiri hasa kwa kuwafichua watu wanaokandamiza haki zao na kuendesha vitendo vya ukatili dhidi yao.
“Ni matukio mengi wanafanyiwa watoto lakini watoto wengi wamekuwa wasiri sana hali inayopelekea matukio mengi ya ukatili, unyanyasaji na kukandamizwa kwa haki mbalimbali kutotambulika na jamii hata na vyombo vya sheria.”amesema Mwasiti.
Mwasiti ameomba serikali kutumia nafasi ya wakosaji wachache wanapelekwa kwenye vyombo vya sheria kuwachukulia hatua kali ili iwe fundisho kwa watu wengine.
Mkazi wa mtaa wa Area Six, kata ya Kichangani Manispaa ya Morogoro, Claudia Lucian amesema kuwa vitendo vya ukatili kwa watoto vimekuwa vikichangia kuporomoka kitaaluma shuleni.
Claudia amesema kuwa kuna namna ya kumwadhibu mtoto bila kumwadhiri kisaikolojia na endapo kiwango cha kuadhibu kitazidi kinatengeneza athari kuwa upande wa kiafya, kimasomo, malezi na tabia, hivyo wazazi wanapaswa kuwa waangalifu katika malezi ya watoto hasa wakati wa migogoro baina ya baba na mama.
0 comments:
Post a Comment