SPIKA WA BUNGE ASHANGAZWA NA KITENDO CHA BENKI YA NBC KUIGAWIA SERIKALI FEDHA KIDOGO
Dodoma. Spika wa Bunge, Job Ndugai ameiagiza Kamati ya Bunge ya Uwekezaji Mitaji (PIC) kutafuta chanzo cha Benki ya NBC kulipa gawio kidogo serikalini ukilinganisha na benki nyingine kama NMB.
Ndugai alitoa kauli hiyo jana wakati akifungua semina ya siku moja kwa kamati hiyo na uongozi wa NBC.
Spika alishtushwa na taarifa zilizotolewa kuwa katika kipindi cha miaka mitatu benki hiyo ilitoa gawio kwa Serikali Sh1 bilioni wakati wenzao wa NMB katika kipindi hicho walitoa gawio la Sh48 bilioni.
“Haiwezekani labda tuelezwe vinginevyo na hapo ndipo ninapotaka muangalie, Serikali ina hisa asilimia 30 NBC na pia kwa benki ya NMB kuna hisa kama hizo lakini malipo yanatofautiana, hapa lazima kutakuwa na tatizo naomba liangaliwe,” alisema Ndugai.
Alifafanua kuwa kwa asilimia 30 ya hisa ambazo Serikali inazo kwa benki hiyo, gawio hilo ni kidogo na linatia shaka.
Alisema benki hiyo inadhihirisha kuwa haina urafiki na wananchi kutokana na kutokuwa karibu nao kwa kushindwa kufungua matawi wala kutoa mikopo kwa wananchi wa vijijini kama ilivyo kwa benki nyingine.
Aliiagiza PIC kuyapitia mashirika yote 272 ya umma ambayo Serikali ina hisa ili kujua maendeleo yake na kuagiza waende hadi katika mashirika ambayo serikali inataka kuingia mikataba ili kuondoa malalamiko yanayoweza kujitokeza siku za usoni.
Mwenyekiti wa Kamati ya PIC, Raphael Chegeni aliitaka benki ya NBC kuacha kulala na kuamka kwani ni wakati wa kufanya kazi kwa ufanisi na serikali na wadau wengine kwani ni kipindi cha ushindani.
Kaimu Mkurugenzi wa NBC, Theobald Sabi alipotakiwa kueleza chanzo cha kutoa gawio kidogo alisema hivi sasa wanasonga mbele wakiendelea kuikuza benki kwani mwaka 2,000 ilikuwa na jumla ya mtaji wa bilioni 326 leo wanazungumzia mtaji wa benki wa Sh1 trilioni.Mwananchi
0 comments:
Post a Comment