Wabunge sasa wahamia katika kuosha magari Dodoma
Dodoma. Ile ajira ya kuosha magari, jana ilichukuliwa kwa muda na wabunge.
Wabunge hao walikuwa wakifanya kazi hiyo ili kuchangisha fedha za ujenzi wa vyoo vya kisasa kwa watoto wa kike shuleni.
Kampeni hiyo ya wabunge kuosha magari, imeandaliwa na Chama cha Wabunge Wanawake, ambao wamedhamiria kujenga vyoo bora kwenye majimbo yote na vitagharimu zaidi ya Sh 3bilioni.
Wabunge waliosha magari leo Juni 9, katika uwanja wa Jamhuri, na kila mmoja aliosha gari na kisha kulipwa kiasi cha fedha na mmiliki wa gari hilo.
Spika wa Bunge, Job Ndugai, aliongoza shughuli hiyo na aliosha magari kadhaa likiwamo la Mussa Azzan Zungu, na kisha kulipwa Sh1milioni.
Ndugai pia aliosha gari la Mbunge wa Urambo, (CCM) Margreth Sitta na la Mbunge wa Kuteuliwa, Salma Kikwete. Ndugai alikusanya zaidi ya Sh8 milioni.
Mbunge wa kuteuliwa Salma Kikwete naye aliosha gari la Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Risala Kabongo, kwa gharama ya Sh1 milioni. Zungu yeye aliosha gari la mbunge wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba, na akapewa na Serukamba Sh 1milioni.
0 comments:
Post a Comment