BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

NYUMBA 50 ZAVUNJWA, 160 WAKOSA MAKAZI, WAJANE, WAJONJWA, YATIMA WATAABIKA

Na Venance George, Kilosa.

PICHA ZAIDI ZA NYUMBA ZILIZOBOMOLEWA ENDELEA KUSHUKA CHINI.


ZAIDI ya wananchi 167 wa kitongoji cha Mateteni, kijiji cha Mbigiri, kata ya Magole, wilayani Kilosa ambao nyumba zao zaidi ya 50 zilivunjwa na tingatinga kwa amri ya mahakama ya ardhi mkoa wanaishi maisha ya taabu katika mahema yaliyotolewa na mkuu wa wilaya hiyo, Halima Dendego.

Timu ya waandishi wa habari na wanaharakati wa haki za binadamu wa mkoani Morogoro waliotembelea eneo hilo juzi walishuhudia maisha magumu wanaoyoishi katika mahema hayo, huku familia zingine zenye baba, mama na watoto zikilazimika kulala katika hema moja.

Akieleza kutokea kwa tukio hilo, Francisca William ambaye nyumba zake mbili zimevunjwa katika sakata hilo, alisema tukio hilo lilitokea Februari 16, mwaka huu majira ya saa 9 alasiri ambapo tinga tinga lilivunja nyumba hizo chini ya ulinzi mkali wa polisi zaidi ya 15 waliotoka kituo kikuu cha polisi na wengine kutoka kituo cha polisi za Dumila.

Alisema kuwa hakukuwa na taarifa yoyote iliyotolewa kuwataka kuondoka katika eneo hilo na hata kufanyika kwa zoezi hilo kulifanywa kwa nguvu kubwa, huku kashifa na matusi vikitawala.
“Walipokuwa wakivunja walikuwa wanatuambia wazi kabisa kwamba tokeni tuvunje tumetumwa na wenye pesa,” alisema William.

William alisema kuwa walihamia katika eneo hilo miaka mitatu iliyopita wakitokea katika eneo lililokuwa likikumbwa na mafuriko kila mwaka na hiyo ilikuwa ni baada ya aliyekuwa mkuu wa mkoa huo, Issa Machibya ambaye kwa sasa ni mkuu wa mkoa wa Kigoma na mkuu wa wilaya ya Kilosa kuwataka kutoka mabondeni na kuhamia kwenye maeneo ya mwinuko.


Muathirika mwingine wa tukio hilo, Fatuma Mohamed, ambaye ni mjane na anayeishi na watoto wawili, Emmy Anthony (12) anayesoma darasa la sita katika shule ya msingi Mbigiri na Vivian Anthony (10) anayesoma darasa la tatu katika shule hiyo alisema kuwa amesikitishwa sana na kitendo cha kunjiwa nyumba yake ambayo ameishi humo kwa muda mfupi sana.


“Mume wangu alifariki mwaka 2007 akaniachia watoto hawa na mimi katika kuhangaika kwangu nimefanikia kujenga nyumba hii tena ilikuwa ni ‘self container’ kwa ajili ya watoto wangu, sasa leo hawa wamekuja kunivunjia nitakwenda wapi na watoto, serikali haioni hata huruma?” alihoji
Mohamed.


Alisema kuwa serikali ndiyo iliyowahamisha kutoka mabondeni walikokuwa wakikubwa na mafuriko kila mwaka na kuwahamishia katika eneo hilo ili kuishi pale kwa muda wakati serikali ikitafuta sehemu nyingine kwa ajili ya kujenga nyumba za kudumu.


Kwa upande wake Elizabeth Joachim akizungumzia tukio hilo, alisema kuwa siku ya tukio mume wake, Peter Paulo alikuwa ni mgonjwa hawezi hata kusimama lakini iliwalazimu kutolewa nje ili nyumba yao ivunjwe na baada ya uvunjaji kufanyika familia hiyo na zingine zilizokuwa zikiishi ndani ya nyumba zilizovunjwa zililazimika kulala nje kwa siku mbili kabla ya kupelekewa mahema na mkuu huyo wa wilaya.


Naye diwani wa kata ya Magole wilayani Kilosa, Juma Rajab Chewe, alisema kuwa yeye binafsi hayuko tayari kuzungumzia suala hilo kutokana na suala hilo kuvuta hisia za watu wengi na kufikia mahali suala hilo kutaka kugharimu maisha yake na familia yake.


“Sitaki kuzungumzia masuala hayo kwa kuwa yamekuwa yakitishia amani yangu nay a familia yangu, hata hivyo siku ambayo zoezi hili lilifanyika wako watu waliokuja nyumbani kwangu hapa wakitaka kuchoma moto nyumba yangu, hivyo naomba mniache ili isije kuniletea shida,” alisema diwani huyo.


Akizungumzia sakala hilo, mkuu wa wilaya hiyo alisema kuwa licha ya wananchi hao kuishi katika eneo hilo kinyume cha sheria lakini mmiliki wa shamba hilo hakutumia uungwana katika kuwaondoa watu hao.

Alisema kuwa mmiliki wa shamba namba tisa ambalo wananchi hao wanadaiwa kuvamia ambaye aliwahi kuwa katibu mkuu katika awamu za serikali zilizopita, Timoth Opio, alikwenda kuonana na mkuu wa mkoa wa Morogoro, Joel Bendera, akiwa na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa alikuli ombi la kwapa muda wananchi hao wakati serikali ikifanya jitihada za kuwapatia
eneo la kudumu.


“Nilishangaa baada ya kupigiwa simu na kuambiwa tayari wamekuja kuvunja, sikuwa na taarifa yoyote na ndipo nilipolazimika kutafuta na mahema ili kuwasitili watu wangu,” alisema mkuu wa wilaya hiyo.

Alisema baada ya kuwapatia mahema hayo aliagiza kuwa waliovunjiwa na wananchi ambao nyumba zao hazikuvunjwa na wako katika eneo hilo waendelee kuishi katika maeneo hayo wakati serikali ikitafuta suluhu ya tatizo hilo.


Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa alishangaa pia kuona polisi waliotumika kusimamia zoezi la uvunjaji wa nyumba hilo wakitoka kituo kikuu cha polisi mjini Morogoro badala ya kutokea Dumila ambapo ni jirani ya eneo hilo.

Kwa upande wake jeshi la polisi mkoani Morogoro limekiri kushiriki polisi wake kusimamia uvunjaji wa nyumba hizo na kudai kuwa kutokana na unyeti wa jambo lenyewe polisi ililazimika kutuma askari wake kutoka kituo kikuu cha polisi mjini Morogoro na wengine kutoka kituo cha
Dakawa.

“Hakukuwa na ulazima kwa tukio kama lile kumjulisha mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya, hii ilikuwa ni amri ya mahakama na sisi tuliombwa na dalali wa mahakama ili tukasimamie utekelezaji wa amri hiyo,” alisema kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro,
Joseph Rugira.


Hata hivyo, Mkuu wa mkoa wa Morogoro Joel Bendera, alisema kuwa mkoa wa Morogoro umekuwa na migogoro sugu ya ardhi na kwamba amekuwa akipokea watu watatu mpaka watano kila siku wenye malalamiko ya ardhi hivyo mkoa umeweka mkakati wa kushughulikia suala
hilo.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: