WAWILI WAGOMA KUWASILISHA BARUA , WAZIRI MKUU KUTOA TAMKO BUNGENI KESHO
WAZIRI MKUU MIZENGO KAYANDA PINDA:
WAKATI kishindo cha
shinikizo la kutakiwa kujiuzulu mawaziri nane wa Serikali ya Rais Jakaya
Kikwete kikizidi kurindima, Waziri Mkuu Mizengo Pinda amesema Serikali itatoa
tamko lake rasmi kesho.
Awali Katibu wa Wabunge wa CCM, Jenister Mhagama aliwaambia waandishi wa habari
juzi usiku kuwa chama hicho kimefanya maamuzi magumu ambayo yangetangazwa na
Pinda mjini hapa jana.
Hata hivyo, Waziri Mkuu Pinda alipoombwa na waandishi wa habari jana kuzungumzia sakata hilo, hakukanusha wala kukiri kuwapo kwa azimio hilo zaidi ya kusema wananchi wasubiri hadi kesho atakapotoa taarifa rasmi.
Hata hivyo, Waziri Mkuu Pinda alipoombwa na waandishi wa habari jana kuzungumzia sakata hilo, hakukanusha wala kukiri kuwapo kwa azimio hilo zaidi ya kusema wananchi wasubiri hadi kesho atakapotoa taarifa rasmi.
Alipoulizwa kama kuna mawaziri ambao wameshawasilisha barua zao za kujiuzulu hadi kufikia jana mchana, Pinda alijibu kwa kifupi kuwa ‘bado hatujapokea, lakini kama wapo watatuletea tu”.
Ingawa Waziri Mkuu hakukiri kupokea barua yoyote, taarifa zisizo rasmi, zilisema mawaziri watano waliokumbwa na msukosuko huo wamekabidhi barua zao huku Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Cyril Chami akikataa kufanya hivyo.
Mwingine ambaye anatajwa kuwa hajawasilisha barua yake, ni Waziri wa Fedha Mustapha Mkulo ambaye kwa sasa yuko nje ya nchi.
Chami ajitetea
Dk. Cyril Chami amesema hataandika barua ya kujiuzulu wadhifa huo na kusema anawaachia wananchi wapime kama kweli anastahili kujiuzulu ama la.
Akizungumza na Mwananchi Jumapili jana alisema yuko tayari kujiuzulu endapo tu wananchi na wabunge watampa fursa ya kusikiliza utetezi wake na kama bado wataona ana makosa,yuko tayari kuachia ngazi.
Dk Chami ni mmoja wa mawaziri ambao Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia kikao cha Wabunge wa chama hicho, kimewapa muda hadi kufikia kesho wawe wameandika barua za kujiuzulu.
Kiini cha D. Chami kutakiwa kujiuzulu, ni kauli za Wabunge wa CCM kuwa anamkingia kifua Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango nchini (TBS), Charles Ekelege anayetuhumiwa kwa ufisadi.
Hata hivyo Dk Chami alisema hadi jana wizara yake ilikuwa haijapatiwa ripoti ya Mamati Maalumu ya Bunge ya Mashirika ya umma iliyokwenda kumchunguza Ekelege katika nchi za Hongkong na Singapore.
“Nataka wananchi wanielewe nitamwajibishaje Ekelege wakati ripoti ya kamati teule ya Bunge iliyomchunguza mimi sina…ningejengaje hoja kwa Rais bila kuwa na tuhuma zake?”alihoji D. Chami.
Alisema Mkurugenzi wa TBS ni mteule wa Rais na kuna taratibu zake ambapo taarifa ya kamati hiyo ndiyo ingeisadia Bodi ya Wakurugenzi ya TBS kumjadili na kupitisha maamuzi,”alisema.
Alifafanua hata ripoti maalumu ya ukaguzi iliyofanywa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) hawakuwa wamepewa na wamepatiwa siku tatu zilizopita mjini Dodoma.
“Bado najiuliza CAG alikuwa na agenda gani na wizara yangu kwa sababu hakutupa ripoti yake lakini akawapa baadhi ya wabunge mpaka tulipofuatulia juzi baada ya kelele za wabunge”alisema.
Aliongeza kusema Waziri wa Fedha, Mustapha Mkulo, leo anashutumiwa kwa kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma(CHC) bila kufuata utaratibu.
“Utashangaa leo Mkulo anashutumiwa kwa kutofuata taratibu kumsimamisha Mkurugenzi Mkuu wa CHC lakini leo mimi nashinikizwa nimsimamishe kazi Mkurugenzi wa TBS bila kufuata taratibu,”alisema.
Dk Chami alisema amejitahidi kuomba taarifa hiyo ya Kamati Teule iliyomchunguza Ekelege lakini hadi jana hajapatiwa zaidi ya kuambiwa ilipelekwa kwa Spika na hajaambiwa baada ya hapo ilikwenda wapi.
Hata hivyo habari za uhakika ambazo gazeti hili inazo , zinaonyesha kuwa baada ya ripoti hiyo ya kamati kufika kwa Spika, Spika naye aliipeleka kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Katika kuthibitisha Wizara ya Viwanda na Biashara haikuwa imeipata barua hiyo, Februari 2,2012 Katibu Mkuu, Joyce Mapunjo alimwandikia barua Katibu wa Bunge akimkumbusha awapatie ripoti hiyo.
Barua hiyo yenye kumbukumbu namba GA96/352/01 iliyopelekwa kwa Katibu wa Bunge Dk Thomas Kashilila, ilisema”nimeona nikukumbushe unisaidie ripoti hiyo niweze kutekeleza maagizo ya kamati”.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, Februari 10,2012 Kamati za PAC na POAC na ile ya Viwanda na Biashara zilikutana Dodoma ambapo Kamati iliendelea kumtuhumu Mtendaji Mkuu wa TBS.
Katika kikao hicho, wizara iliagizwa kuwasilisha kwa CAG ripoti ya idadi ya magari aliyokaguliwa na mapato yake, na wizara ikakabidhi ripoti hizo Februari 15,2012 kwa barua yenye kumb GA.96/352/01.
Ni kwa maelezo hayo, Dk. Chami alidai tangu wakati huo ofisi yake haijawahi kupokea ripoti nyingine yoyote iwe ya CAG au kutoka kwa Spika zaidi ya kufahamu kuwapo kwake bungeni wiki hii.
Dk Chami alifafanua kuwa kukosekana kwa ripoti hizo kulimfanya afungwe mikono ya kwenda kwa Rais kumshauri amuondoe Ekelege kwa kuwa hakuwa na ripoti iliyokuwa ikionyesha tuhuma zake.
Kutokana na msingi huo, Dk. Chami alisema chombo alichobakia nacho kuchukua maamuzi ni Bodi ya Wakurugenzi ya TBS na bodi hiyo iliundwa na kuzinduliwa Machi 29, 2012.
Dk Chami alisema bodi hiyo ilikutana Aprili 5,2012 na Wizara yake ikapokea ushauri wa Bodi hiyo Machi 19,2012 na wakati ripoti ya ukaguzi maalumu wa CAG akiipokea Aprili 18 akiwa Bungeni Dodoma.
Omari Nundu
Kwa upande wake Waziri wa Uchukuzi,Omari Nundu jana alitumia Bunge kurusha kombora kwa Kamati ya Mindombinu kuwa imekuwa na taarifa zisizo sahihi.
Kwa upande wake Waziri wa Uchukuzi,Omari Nundu jana alitumia Bunge kurusha kombora kwa Kamati ya Mindombinu kuwa imekuwa na taarifa zisizo sahihi.
Nundu alisema taarifa zote juu yake ni za uongo huku akikanusha kwamba hajawahi kusaini makubaliano (MoU) yoyote kuhusu mradi wa upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam gati namba 13 na 14.
Ngeleja
Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja ambaye pia ni Mbunge wa Sengerema, alipoulizwa na mwandishi wetu kupitia ujumbe mfupi wa maandishi(SMS) alijibu kwa kifupi ‘Tuziachie mamlaka za maamuzi”.
Mawaziri wanaotakiwa kujiuzulu ili kuinusuru Serikali ni Waziri wa Fedha, Mustapha Mkulo,Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja na Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige.
Wengine ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hadji Mponda na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Lazaro Nyalandu.
Taarifa zilizopatikana juzi usiku zilieleza kuwa katika kikao hicho, mawaziri hao kwa pamoja waliwekwa katika eneo maalumu na wakawa wakiitwa mmoja mmoja kwa ajili ya mahojiano na wabunge na baadaye kupewa msimamo wa chama.
Baada ya kumalizika kwa kikao hicho, Waziri Mkuu akaendesha kikao kingine cha faragha, safari hii kikimhusisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali,Frederick Werema na Waziri William Lukuvi.
Wengine walioitwa katika kikao hicho ni Katibu wa Uchumi na Fedha wa CCM, Mwigulu Mchemba,Katibu wa Oganaizesheni na Mahusiano ya Nje Januari Makamba na Katibu wa wabunge wa chama hicho, Jenister Mhagama.
Hata hivyo mwenye mamlaka ya kuwafukuza Mawaziri kwa mujibu wa Katiba ni Rais Jakaya Kikwete aliyewateua ingawa hata hivyo badhi ya wabunge wanamtuhumu Rais kuwa si mtu wa kufanya maamuzi haraka na kwa shinikizo.
Jana baadhi ya mawaziri wanaotakiwa kuachia ngazi waliingia katika ukumbi wa Bunge na kukalia viti vyao lakini mara baada ya kuahirishwa kwa kikao, waliondoka haraka katika viwanja vya Bunge.
Baadhi yao walipotafutwa kwa simu ili watoe ufafanuzi na msimamo wao kuhusiana na azimio hilo la CCM, ama simu zao zilikuwa hazipatikani kabisa na zingine hazikupokelewa, zilikatwa.
Zitto aendelea kutafuta saini
Katika hatua nyingine,Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe alisema hoja ya kumpigia Waziri Mkuu kura ya kutokuwa na imani ipo pale pale kama mawaziri wanaotajwa kwa ufisadi hawatajiuzulu kufikia kesho.
“Sisi tunasema bila kumwajibisha Waziri Mkuu hawa mawaziri waliotajwa hawatatoka na wasipotoka madudu haya yatarudia…kwa hiyo ni wao mawaziri kupima na kuwajibika au wamweke reheni Waziri Mkuu,”alisema.
Mbunge huyo alirejea wito wake wa kuwaomba wabunge wenye uchungu na ubadhirifu na ufisadi waunge mkono utiaji wa saini hizo na kwamba kama mawaziri watajiuzulu ifikapo Jumatatu, wataondoa hoja hiyo.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Kambi rasmi ya upizania Bungeni, Freeman Mbowe alirejea msimamo wake wa kuomba kufanyiwa mabadiliko ya katiba ya nchi na kanuni za Bunge ili Spika asiwe anatokana na chama chochote cha siasa.
Mbowe alitoa kauli hiyo kutokana na kile alichodai, hatua ya Spika Anne Makinda kutafsiri vibaya kanuni za Bunge na Katiba ya nchi ili tu kuilinda Serikali na Waziri Mkuu wake ili asipigiwe kura ya kutokuwa na imani.
“Mambo ya ajabu sana eti Spika anasema hili zoezi letu ni batili…sisi tunamshangaa, wanasheria wanamshangaa na hata wananchi wanamshangaa… anatoleaje mwongozo kwa kitu ambacho hakipo mezani kwake?”alihoji.
Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, alisema kanuni inataka ili hoja ya kumpigia kura ya kutokuwa na imani na Waziri mkuu iweze kufikishwa ofisi ya Spika, ni lazima ipate sahihi za wabunge 70 na ndicho wanachokifanya.
Wasomi wazungumza
Baadhi ya wasomi wa Chuo Kikuu wamelitaka Bunge kufuata sheria na kanuni za Bunge kabla ya kufanya maamuzi hayo kwa sababu mawaziri hao wanaripoti kwa Rais Jakaya Kikwete na si Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam jana, wasomi hao walisema kuwa, kutokana na hali hiyo wabunge hao wanapaswa kufuata kanuni ili waweze kutambua kuwa mwenye mamlaka ya kuwaondoa mawaziri hao ni Rais na si Waziri Mkuu, hivyo basi kumlazimisha aondoke madarakani ni sawa na kumuonea.
“Mimi naona wanamuonea bure Waziri Mkuu Pinda, kwa sababu hana mamlaka ya kuwaondoa Mawaziri madarakani badala yake wanatakiwa kuangalia kanuni kwanza ndipo waweze kufanya maamuzi,”alisema Profesa Simon Mbilinyi mwasiasa mstaafu nchini.
Aliongeza kutokana na hali hiyo wabunge hao walipaswa kumuandikia barua Rais Kikwete na kumtaarifu kuwa mawaziri wake wameshindwa kufanya kazi badala yake wanatakiwa kuwajibika kulingana na makosa waliyofanya.
Alisema kutokana na hali hiyo maamuzi ambayo yangeweza kutolewa na rais yangekuwa sahihi kwa sababu yamefuata sheria na taratibu zilizotungwa na Bunge.
Alisema kitendo cha wabunge hao kumshinikiza Waziri Mkuu kujiuzulu au kuwaondoa mawaziri hao ni kinyume na sheria na ni sawa na kumuonea, jambo ambalo linaweza kumfanya afanye maamuzi bila ya kufuata taratibu.
Hata hivyo, Profesa Abdalah Safari alisema kuwa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) ni wanafiki, na kwamba wanashindwa kufanya maamuzi mpaka wasubiri nguvu kutoka kwa wapinzani.
Alisema kutokana na hali hiyo wabunge hao wamepoteza mwelekeo na kwamba wamejaa woga jambo ambalo limesababisha kuendekeza ufujaji wa mali za umma kwa makusudi.
Naye Makamu Mkuu Chuo Kikuu cha Matakatifu Agustino cha Mwanza (Sauti) Dk Charles Kitima amesema mchakato unaofanywa na wabunge kwa lengo la kumg’oa Waziri Mkuu Pinda sio suluhu ya kutibu tatizo la uwajibikaji kwa viongozi serikalini.
“Tunalia watu wajiuzulu wakati tumebaki na mfumo ambao unaruhusu siasa chafu, Mahakama inaingiliwa katika maamuzi yake Tume ya Uchaguzi haiko huru, hili haliwezi kuleta mabadiliko sababu Rais atateua mtu mwingine kufanya kazi hiyo na shughuli zitaendelea kama kawaida”alisema Dk Kitima.
Dk Kitima ambaye alikuwa akichangia mada katika kipindi cha jicho letu katika habari kinachorushwa na kituo cha Televisioni cha Star Tv cha jijini Mwanza jana, alisema njia pekee ambayo inaweza kuleta mabadiliko ni kubadilisha mfumo utakaowezesha viongozi kuwajibika kwa wananchi.
“Walijiuzulu Edward Lowasa, Nazir Karamagi na Dk Ibrahim Msabaha nini kimebadilika, rais ameteua wengine matatizo bado yanaendelea serikalini tatizo si watu bali mfumo uliopo ambao unatoa fursa kwa viongozi na watendaji kuwajibika kwa waliowateua”alisema Dk Kitima.
Habari hii imeandikwa na Daniel Mjema na Habel Chidawali, Dodoma, Patricia Kimelemeta, Geofrye Nyang’oro
Orodha ya wabunge waliosaini:
- 2. Rashid Ali Abdallah – CUF
- 3. Chiku Aflah Abwao- Chadema
- 4. Saluim Ali Mbarouk – CUF
- 5. Salum Khalfam Barwany – CUF
- 6. Deo Haule Filikuchombe- CCM
- 7. Pauline Philipo Gekul- Chadema
- 8. Asaa Othman Hamad- CUF
- 9. Prof.Kuliyokela Kahigi- Chadema
- 10. Naomi Mwakyoma Kaihula – Chadema
- 11. Sylvester Kasulumbayi- Chadema
- 12. Raya Ibrahim Khamis - Chadema
- 13. Mkiwa Hamad Kiwanga - CUF
- 14. Susan Limbweni Kiwanga- Chadema
- 15. Grace Sindato Kiwelu –Chadema
- 16. Kombo Khamis Kombo – cuf
- 17. Joshua Samwel Nassari – Chadema
- 18. Tundu Antiphas Lissu- Chadema
- 19. Aphaxar Kangi Lugola- CCM
- 20. Susan Anselim Lymo- Chadema
- 21. Moses Machali – NCCR Mageuzi
- 22. John Shibuda Magalle – Chadema
- 23. Faki Haji Makame- CUF
- 24. Esther Nicholas Matiko- Chadema
- 25. Joseph Osmund Mbilinyi- Chadema
- 26. Freman Aikaeli Mbowe- Chadema
- 27. Kurudhum Jumanne Mchuchuli – Chadema
- 28. Halima James Mdee-Chadema
- 29. John John Mnyika- Chadema
- 30. Augustino Lyatonga Mrema- TLP
- 31. Maryam Salum Msabaha- Chadema
- 32. Peter Msingwa-chadema
- 33. Christowaja Gerson Mtinda- Chadema
- 34. Philipa Geofrey Mturano- Chadema
- 35. Christina Lissu Mughwai- Chadema
- 36. Joyce John Mukya – Chadema
- 37. Mchungaji Israel Yohane Natse – Chadema
- 38. Philemon Ndesamburo- Chadema
- 39. Ahmed Juma Ngwali- CUF
- 40. Vincent Josephat Nyerere- Chadema
- 41. Rashid Ali Omar- CUF
- 42. Meshack Jeremiah Opulukwa- Chadema
- 43. Lucy Philemon Owenya- Chadema
- 44. Rachel Mashishanga- Chadema
- 45. Mhonga Said Ruhwanya – Chadema
- 46. Conchesta Rwamlaza – Chadema
- 47. Moza Abedi Saidy- CUF
- 48. Joseph Roman Selasini – Chadema
- 49. David Ernest Silinde- Chadema
- 50. Rose Kamili Sukum - Chadema
- 51. Cecilia Daniel Paresso- chadema
- 52. Kabwe Zuberi Zitto- Kigoma Kaskazini
- 53. Magdalena Sakaya – CUF
- 54. Rebecca Mngodo- CUF
- 55. Sabreena Sungura -Chadema
- 56. Hamad Rashid Mohammed- CUF
- 57. Rukia Kassim Ahmed- CUF
- 58. Mustapha Boay Akoonay -Chadema
- 59. Abdalla Haji Ali -CUF
- 60. Khatibu Said Ali -CUF
- 61. Hamad Ali Hamad -CUF
- 62. Riziki Omar Juma -CUF
- 63. Haji Khatibu Kai -CUF
- 64. Anna Marystella John Malack -Chadema
- 65. Hamad Rashid Mohamed -CUF
- 66. Rajab Mbarouk Mohamed -CUF
- 67. Thuwayba Idrissa Muhamed -CUF
- 68. Masoud Abdallah Salum -CUF
- 69. Muhamad Ibrahim Sanya -CUF
- 70. Ali Khamis Seif -CUF
- 71. Haroub Muhammed Shamis -CUF
- 72. Amina Amour Nassoro -CUF
0 comments:
Post a Comment