Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusu vurugu zilizotokea kati ya Jeshi la Polisi na wananchi Wilayani Tandahimba, mkoani Mtwara na kuitaka serikali kuwajibika na kumfukuza mkuu wa Wilaya hiyo. Kulia ni naibu mkurugenzi wa Uenezi na Mahusiano, Abdul Kambaya. Picha na Rafael Lubava
MWENYEKITI cha CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ameitaka jamii kutomhukumu Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwa kushindwa kushughulikia madai ya wabunge kutaka mawaziri wajiuzulu akidai kuwa Rais Jakaya Kikwete amemziba mdomo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana, Profesa Lipumba alisema hata kama Pinda angekuwa na utashi wa kuzungumzia suala hilo, asingeweza kusema chochote kwa kuwa Rais Kikwete alimziba mdomo... "na suala hilo pia liko juu yake."
Profesa Lipumba alimtuhumu Rais Kikwete kuwa chanzo cha kuwapo kwa mawaziri wabadhirifu kwa kile alichoeleza kuwa mara zote amekuwa akiwakingia kifua.
Tatizo la ubadhirifu haliwezi kuisha katika Serikali ya Awamu ya Nne maana tatizo siyo watendaji wala mawaziri, ni Rais Kikwete mwenyewe… amekuwa ni mtu asiyekuwa na uamuzi,” alisema Profesa Lipumba na kuongeza:
“Haishangazi kuona mawaziri katika wizara moja hawaelewani. Kuna mawaziri wana nia njema na wanasimamia haki, lakini hata wakitoa mapendekezo yao yanapuuzwa na wapo ambao wanatumia nafasi zao vibaya huku Rais akiendelea kuwachekea.”
Alisema CUF kinaangalia namna kitakavyounganisha nguvu na vyama vingine vya upinzani kikiwemo Chadema kuongoza maandamano nchi nzima ili kushinikiza mawaziri wanaotuhumiwa kwa madai mbalimbali wajiuzulu.
Alisema kwa namna yoyote ile Waziri Mkuu asingeweza kuamua jambo bila kupewa ruhusa na Rais na kushindwa kuwawajibisha watu hao ni dhahiri kuwa Rais hakumtaka kufanya hivyo.
Alidai kuwa Baraza la Mawaziri limegawanyika katika makundi na baadhi wamejenga chuki baina yao kutokana na Rais kuendelea kuwalea watendaji wabovu huku akipuuza ushauri anaopewa.
Alipongeza na kuunga mkono hoja ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe ya kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu.
Alisema jukumu kubwa la wabunge sasa ni kushinikiza Waziri Mkuu kujiuzulu kutokana na kushindwa kutumia nafasi yake kuwawajibisha mawaziri wanaotuhumiwa kwa ubadhilifu wa fedha za umma.
Profesa Lipumba alisema katika kumshinikiza Rais Kikwete kuchukua hatua dhidi ya watendaji wabadhirifu serikalini wakiwemo mawaziri, watawashirikisha wananchi kwa kuandaa maandamano nchi nzima.
Alimpongeza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh kwa kutoa ripoti aliyoeleza kuwa imeibua madudu bila upendeleo.
Alisema jamii inahitaji kujua matumizi ya Serikali katika shilingi inayotokana na kodi za wananchi na namna zinavyosimamiwa huku akisema ubadhilifu uliojionyesha katika ripoti ya CAG, ni aibu kubwa kwa Serikali ya Kikwete.
Kauli hiyo ya Profesa Lipumba imekuja wakati tayari Chadema kimetangaza kuitisha maandamano ya wananchi ili kuiwajibisha Serikali, iwapo Rais Kikwete hatawafukuza mawaziri wanaokabiliwa na tuhuma hizo.
Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika imeeleza kuwa chama hicho kitatumia Ibara ya 8 (1) (a) ya Katiba kuunganisha nguvu za wananchi katika kutimiza azma hiyo.
“Iwapo Rais Kikwete hatavunja Baraza la Mawaziri au kuwafukuza mawaziri hao… pamoja na hatua zinazoendelea sasa za kuwasilishwa hoja ya kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu; Kurugenzi ya Habari na Uenezi itawasilisha taarifa kwenye vikao vya chama ili Ibara ya 8 (1) (a) Katiba ya nchi itumike kuunganisha nguvu za wananchi kuiwajibisha Serikali,” alisema Mnyika katika taarifa hiyo.
Ibara hiyo inaeleza kuwa, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya kidemokrasia na kwamba wananchi ndiyo msingi wa mamlaka yote na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake kutoka kwa wananchi.
Mnyika alisema Rais Kikwete anapaswa kutekeleza haraka wito wa kuvunja Baraza la Mawaziri au kuwafukuza baadhi, kwani sehemu kubwa ya masuala yaliyokuwa yakijadiliwa bungeni yakiwemo ya ufisadi na matumizi mabaya yanatokana na udhaifu wa uongozi wao.
Alimtaka Rais Kikwete kutumia mamlaka anayopewa na Katiba katika Ibara ya 57 (1) (c) inayomruhusu kufuta uteuzi na kuwaondoa madarakani mawaziri pindi anapoona inafaa kufanya hivyo.
0 comments:
Post a Comment