BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

BAKWATA YATANGAZA RASMI KUSUSIA ZOEZI LA SENSA 2012.



Mufti mkuu wa Tanzania Shekhe Issa Bin Shabaan Simba aliyekaa katika kiti akifafanua jambo wakati akiongea na waumini wa dini ya kiislam mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa ofisi mpya ya Bakwata wilaya ya Kilosa katika msikiti mkuu wa Bakwata wa Manyema wilayani huo katika ziara ya siku tatu Februari 14, 2012 mkoani Morogoro.


BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) limetangaza rasmi kutoshiriki sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika nchi nzima Agosti, hadi ombi lao la kuingizwa kwa kipengele cha dini kwenye dodoso la sensa kitakapofanyiwa kazi.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Amir Mkuu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Shehe Mussa Kundecha, alisema uamuzi huo umetokana na Serikali kushindwa kusikiliza upande wa Waislamu na kuamua kutokiingiza kipengele hicho.

Alisema katika mkutano wa viongozi wa dini na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) uliofanyika Dodoma Juni 11, waliwasilisha ombi lao la kipengele cha dini kuingizwa kwenye dodoso za sensa ili kupata idadi kamili ya Watanzania kidini.

“Kwa kweli mkutano ulikwenda vizuri, tulitoa sababu zetu za kutaka kipengele hicho kiwemo ili kuondoa utata wa sasa wa kila taasisi na dini kutoa takwimu zinazotofautiana na Kamishna wa Takwimu alipokea maombi yetu na kuahidi kuyawasilisha serikalini na kuyafanyia kazi,” alisema Shehe Kundecha.
Alisema cha kushangaza wakati akifunga mkutano huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Uhusiano na Uratibu, Stephen Wasira alibainisha wazi kuwa kamwe Serikali haiwezi kukiingiza kipengele hicho kwenye dodoso za sensa, kwa kuwa kinavunja umoja, amani na utulivu wa Taifa.

Aidha, alisema katika kutetea hoja hiyo, Serikali ilitoa mifano ya nchi za Nigeria na Kenya, ambazo zimefanya sensa na kuingiza kipengele hicho kwenye dodoso, lakini kutokana na kuibuka kwa vuguvugu la kidini katika nchi hizo, hadi leo matokeo ya sensa hizo hayajatangazwa.

Shehe Kundecha alisema Baraza hilo limepokea hoja hizo na kuzisikiliza ingawa halikubaliani nazo kwa kuwa kwa Tanzania bado zipo taasisi na madhehebu ya dini yanayotoa takwimu za kidini yakionesha idadi ya Wakristo, Waislamu na Wapagani huku umoja na amani vikiendelea kuwapo.

“Kama tatizo ni kuvurugika kwa amani, umoja na utulivu, mbona basi vyombo hivi visivyohusika na takwimu vinatoa takwimu hizi tena hadi kwenye mitandao na Serikali kuvifumbia macho, huku kukiwa hakuna umoja wala amani iliyovunjika? Kwa nini isifanyike sensa ya kidini na kupatikana takwimu halisi?” Alihoji.

Alisema kutokana na kauli hiyo, inaonekana wazi kuwa Serikali haijasikiliza kilio cha Waislamu kutaka kipengele cha dini kiingizwe kwenye dodoso za sensa, ili zipatikane takwimu sahihi na rasmi za Watanzania kidini.

“Hivyo basi tunasisitiza Waislamu hatutashiriki sensa mpaka mapendekezo yetu yatakapofanyiwa kazi, tunataka idadi halisi ya Waislamu, ili nasi tujue tunawasaidiaje kimaendeleo na kidini,” alisema.

Ustaadh Sadiki Gogo, alisema mfano uliotumiwa na Serikali kukataa ombi la kuingizwa kwa kipengele cha dini kwenye dodoso la sensa hauna nguvu, kwa kuwa umeegemea upande mmoja na kusahau nchi kama Uganda, Uingereza, Australia na Canada, ambazo katika sensa zao wanatumia kipengele cha dini na hazina matatizo.

Hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Shura ya Maimamu Tanzania, Shehe Ponda Issa Ponda, alisema atahakikisha Waislamu hawashiriki Sensa ya Watu na Makazi iwapo Serikali haitarudisha kipengele cha dini katika maswali wanayoulizwa wananchi.

Alisema haoni hoja ya msingi ya kuondoa kipengele hicho kwani uzoefu unaonesha kuwa baada ya Serikali kukiondoa, makundi yenye mwelekeo maalumu hutumia nafasi hiyo kutoa takwimu za idadi ya Waislamu, Wakristo na Wapagani.

Pamoja na kauli ya Wasira, Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Dk Albina Chuwa, alikataa ombi la mashehe la kujumuisha kipengele cha dini katika dodoso za maswali wakati wa sensa. Alisisitiza mbele ya viongozi wa dini mbalimbali wakiwemo mashehe kuwa maswali yanayohusu kabila na dini hayatajumuishwa kwenye dodoso kwani Serikali haipangi mipango ya maendeleo ya wananchi kwa kufuata itikadi za kidini au ukabila.

Chanzo Habari Leo
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: