Wachezaji wa Azam wakishangilia bao la pili lililofungwa na mshambuliaji John Boko katika mechi ya robo fainali ya Kombe la Kagame dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana. Azam ilishinda 3-1.
Picha na Michael Matemanga.
Sosthenes Nyoni, Mwananchi.
MSITU wa Pande ni jina maarufu nchini kwa sasa kutokana na matukio ya watu kutekwa na kupelekwa huko kuteswa na kuuwawa kinyama.
Kitendo kama hicho cha kinyama ndicho kinachofananishwa na ilichofanyiwa Simba jana na mshambuliaji wa Azam, John Boko baada ya kufunga mabao matatu pekee na kuiwezesha timu yake kushinda 3-1 katika mechi ya robo fainali ya Kombe la Kagame kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kwa ushindi huo sasa Azam itacheza mechi ya nusu fainali ya Kombe la Kagame dhidi ya AS Vita ya DR Congo iliyoitoa Atletico ya Burundi kwa mabao 2-1 katika mechi iliyochezwa awali.
Boko alifunga bao lake la kwanza dakika 17, akiunganisha kwa kichwa krosi ya Ibrahimu Shikanda, kisha akapachika la pili kwa shuti dakika 46 akimalizia pasi ya Kipre Tchetche, kabla ya Shomari Kapombe kuifuta machozi Simba dakika 53, lakini Boko mfungaji bora wa msimu uliopita alizima ndoto za Simba kurudi kwa kupachika bao la tatu kwa shuti la chini lililomshinda Juma Kaseja na kujaa wavuni.
Katika kile kinachoonekana kujaa kwa imani za kishirikina jana klabu za Simba na Azam hazikutumia mlango mkuu wa kuingilia uwanjani baada ya kumaliza kufanya mazoezi.
Simba wenyewe walitokea geti la kaskazini na Azam walipita mlango tofauti wakati wakirejea vyumbani tayari kujiandaa na mechi hiyo.
Simba ilianza mchezo huo kwa kasi na kufanikiwa kufika langoni kwa Azam katika dakika ya kwanza na saba, lakini Haruna Moshi na Felix Sunzu na Uhuru Selemani walishindwa kutumia nafasi hizo.
Katika mechi hiyo Sunzu alipewa kadi ya njano na mwamuzi Issa Kangabo kutoka Rwanda kwa kumchezea vibaya Tchechte.
Mwanzoni mwa kipindi cha kwanza Uhuru Selemani alipoteza nafasi mbili za kufunga baada ya kuwatoka mabeki wa Azam, lakini jitihada zake ziliishia mikononi mwa kipa Deogratius Munishi, huku Azam wakijibu mapigo dakika 14 baada ya Kipre kuwatoka mabeki wa Simba na kupitisha pasi kwa Hamis Mcha aliyepiga fyongo shuti lake.
Dakika ya 17 beki Shikanda wa Azam alipokea pasi ndefu kutoka katikati ya uwanja na kupiga krosi iliyotua kichwani kwa Bocco ambaye alipiga kichwa kilichokwenda wavuni na kumwacha Kaseja akiwa amesimama.
Simba walijaribu kurudi mchezoni, lakini mashuti ya Kapombe na Mwinyi Kazimoto dakika 34 na 36 yalishindwa kulenga goli. Dakika 41 mwamuzi aliinyima Simba penalti baada ya Kazimoto kumuangusha Ramadhan Chombo kwenye eneo la hatari.
Azam walianza kipindi cha pili kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la pili dakika 46 kupitia Boko aliyemalizia vizuri kazi ya Tchetche aliyekuwa mwiba kwa ngome ya Simba.
Mchezaji bora wa mwaka wa Taswa, Kapombe aliifungia Simba bao dakika 53 akipokea krosi ya Haruna Shamte na kupiga shuti kali akiwa ndani ya 18 lililomshinda Munishi.
Kocha wa Azam, Stewart Hall aliwapumzisha Tchetche, Mcha na kuwaingiza George Odhiambo na Jabir Aziz, wakati Simba ilimtoa Uhuru, Jonas Mkude, Mudde Musa na kuwaingiza Kigi Makasi, Amri Kiemba na Hamis Kinje.
Mabadiliko hayo yalionekana kuwa na faida kwa Azam kwani dakika 73, Aziz alitoa pasi kwa Boko na kupiga shuti la chini akiwa nje ya 18 na kwenda moja kwa moja wavuni na kuwanyamazisha kabisa mashabiki wa Simba.
Awali Atletico ya Burundi inayosifiwa kwa kucheza soka ya kuvutia iliyaaga mashindano hayo kwa kuchapwa mabao 2-1 na AS Vita ya DR Congo.
Mshambuliaji Etekiama Taddy alifunga bao lake la sita kwenye michuano hiyo alipozifumania nyavu za Atletico katika dakika ya 8 na kuifanya AS Vita kumaliza kipindi cha kwanza wakiwa mbele kwa bao 1-0.
Atletico ilirudi vizuri na kufanikiwa kupata bao la kusawazisha dakika 48 kwa shuti kali lililopigwa naPierre Kwizera akiitumia vizuri pasi iliyopigwa na Henry Mbazumutima.
Wakati mashabiki wakidhani mpira huo utaamuliwa kwa mikwaju ya penalti, mshambuliaji Basilua Makola aliifungia AS Vita bao la ushindi katika dakika za nyongeza na kufanya mchezo huo kumalizika kwa 2-1.
Nusu fainali ya michuano hiyo itaendelea tena kesho kwa Azam kuivaa AS Vita saa nane mchana na mabingwa watetezi Yanga kupepetana na APR saa kumi jioni kwenye Uwanja wa Taifa.
0 comments:
Post a Comment