CCM YAPOTEZA TENA JIMBO LA IGUNGA-TABORA.
MAHAKAMA YATENGUA MATOKEO YA MBUNGE WAKE IGUNGA, CHADEMA WAIBUKA KIDEDEA.
Mustapha Kapalata na Hastin Liyumba, Nzega
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimepata pigo baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, kutengua matokeo ya ubunge Jimbo la Igunga yaliyompa ushindi mgombea wake, Dk Dalaly Peter Kafumu.Dk Kafumu aliibuka mshindi katika uchaguzi mdogo uliofanyika Oktoba 2, mwaka jana kuziba nafasi ya Rostam Aziz ambaye alijiuzulu kwa madai kwamba anaachana na siasa chafu ndani ya CCM.
Uchaguzi huo ulikuwa wa ushindani mkubwa kati ya Dk Kafumu na aliyekuwa mgombea wa Chadema, Joseph Kashindye ambaye hakuridhishwa na mwenendo wa uchaguzi huo, hivyo kuamua kupinga matokeo hayo mahakamani. Kesi hiyo ilifunguliwa Machi 26, mwaka huu.
Akitoa hukumu hiyo, Jaji Mary Nsimbo Shangali alisema Mahakama ilipokea malalamiko 15 ambayo yaliridhiwa na pande zote mbili, lakini baadaye yakaongezwa madai mengine mawili hivyo kufikia 17.
“Madai yaliyopokewa na Mahakama ni 17 na kati yake imethibitisha madai saba,” alisema Jaji Shangali katika hukumu hiyo.
Mbali na Dk Kafumu, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya uchaguzi walikuwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Igunga aliyetangaza matokeo hayo.
Dk Kafumu akizungumza na Radio One jana alisema tangu awali, hakuwa na imani na jaji aliyesikiliza kesi hiyo. Alisema hana mpango wa kukata rufaa, bali anawaachia viongozi wa CCM kufanya hilo.
Alisema baada ya ubunge wake kutenguliwa, anaendelea na shughuli zake za madini kwa kuwa ni mtaalamu wa sekta hiyo... “Ndugu mwandishi karibu Singida, mimi narudi kuendelea na shughuli zangu za madini.”
Sababu za kutengua matokeo.
Alisema hoja zilizothibitishwa na Mahakama na ambazo zimetumika kutengua matokeo hayo ni pamoja madai kwamba Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli alitumia nafasi yake ya uwaziri kutoa ahadi ya ujenzi wa Daraja la Mbutu ambalo lilikuwa ni moja ya kero kubwa kwa wananchi wa Jimbo la Igunga.
Dk Magufuli akiwa katika moja ya kampeni za uchaguzi huo, alitumia nafasi ya uwaziri kwa kuwatisha wapigakura wa jimbo hilo kwa kusema kama hawatamchagua mgombea wa CCM, watawekwa ndani.
Jaji Shangali aliendelea kueleza kuwa Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Aden Rage alitangaza kuwa mgombea wa Chadema alikuwa amejitoa katika uchaguzi huo, jambo ambalo Mahakama imeridhishwa na ushahidi uliokuwa ukitolewa.
Jaji Shangali alitaja hoja nyingine iliyotumika kufuta matokeo hayo kuwa ni kauli ya Imamu Swaleh Mohamed wa Msikiti wa Ijumaa Igunga, kuwatangazia waumini wa msikiti huo kuwa wasikichague Chadema, kwa kuwa baadhi ya viongozi wake wamemdhalilisha Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatuma Kimario.Alisema hoja nyingine ni Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama kudai kuwa Chadema kilileta makomandoo katika uchaguzi huo na kupanga kuuvuruga.
Hoja nyingine ambayo Jaji Shangali aliikubali ni ugawaji wa mahindi ya kuwawezesha wakazi wa Igunga kukabiliana na njaa wakati wa uchaguzi huo kwamba ulitumiwa vibaya na baadhi ya wanasiasa kuwashawishi wananchi wawapigie kura.
Jaji huyo alihoji iwapo wakazi wa Jimbo la Igunga walikuwa na njaa sana wakati wa uchaguzi huo kiasi cha viongozi wa Serikali kuona kuwa ulikuwa wakati mwafaka wa kugawa mahindi hayo.
Kuhusu hoja ya upande wa utetezi kwamba mgombea wa Chadema, Kashindye alipaswa kupeleka malalamiko hayo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), alisema siyo ya msingi yanayoweza kumzuia mlalamikaji kupeleka malalamiko hayo katika Mahakama Kuu na hakuna kifungu chochote kinachomzuia mlalamikaji kufanya hivyo.
Kutokana na hali hiyo, Jaji Shangali alisema kuanzia sasa Jimbo la Igunga lipo wazi na kwamba: “Milango iko wazi kwa walalamikiwa kukata rufaa ikiwa hawajaridhika na uamuzi.”
Hali ya usalama katika mahakama hiyo ilikuwa imeimarishwa, huku wafuasi wa Chadema wakiwa wengi zaidi na wakionekana kuwa na furaha hasa baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo.
Dk Slaa, Nape wazungumza.
Baada ya hukumu hiyo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema: “Mahakama imedhihirisha yale ambayo tumekuwa tukisema kila wakati kwamba CCM inatumia mabavu.”
Alisema anashukuru Mahakama kwa kutoa haki na kukubaliana na Chadema kuwa CCM iligawa vyakula kwa wananchi ili kuwashawishi wawapigie kura.
Pia alisema kwamba imeudhihirishia umma kauli kwamba CCM kinatumia vibaya rasilimali za nchi katika mambo ya siasa akitoa mfano wa mawaziri kuwalazimisha watu wawachague wagombea wao.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema alikuwa hana taarifa kuhusu hukumu ya kesi hiyo.
Hata alipopata taarifa kuhusu matokeo hayo, alisema atakuwa tayari kuyazungumzia pindi akiyapata kutoka katika mfumo wa chama chao.“Siwezi kuzungumzia matokeo ya hukumu unayoniambia wewe. Nitakuwa tayari pindi nitakapoyapata rasmi kutoka kule Igunga (CCM),” alisema Nape.
Uchaguzi
Oktoba 3 mwaka jana Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Igunga, Magayane Protas alimtangaza Dk Kafumu kushinda ubunge kwa kura 26,484 akifuatiwa na Kashindye ambaye alipata kura 23,260, huku Leopold Mahona wa CUF akipata kura 2,104.
Ushindi huo wa CCM ulihitimisha mojawapo ya michuano mikali ya kisiasa nchini ambayo Chadema, CUF na CCM vilionekana kufukuzana vikali. Dk Kafumu kabla ya nafasi yake hiyo alikuwa Kamishna wa Madini katika Wizara ya Nishati na Madini.
Ushindi wa CCM katika jimbo hilo ulikuwa ni pigo kubwa kwa Chadema kwani ulikifanya chama hicho kushindwa kuibuka na ushindi hata katika mazingira ambayo kilitarajiwa au kuonekana kukubalika zaidi. Chaguzi nyingine ambazo Chadema kilidhaniwa kushinda ni zile za Babati, Busanda na Biharamulo ambako kote CCM kilitetea viti vyake.
Nyongeza na Leon Bahati.
0 comments:
Post a Comment