Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia Mkuu wa Mkoa wa Mara,
Mheshimiwa John Gabriel Tupa salamu za rambirambi kuomboleza kifo cha
Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Kepteni (mst) James Charles Yamungu.
Kifo hicho kimetokea alfajiri ya, Jumatano, Agosti 22, 2012, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam ambako alikuwa amelazwa.
Katika salamu hizo za Rais Kikwete amemwambia
Mheshimiwa Tupa.
“ Nimepokea kwa huzuni na mshtuko taarifa za kifo cha
Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Kepteni Mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa
Tanzania, Mheshimiwa James Yamungu"
Amesema Rais Kikwete katika salamu hizo: “
Kifo cha Kepteni Yamungu kimeinyang’anya nchi yetu na Serikali yetu
mtumishi hodari na mwadilifu wa umma ambaye katika utumishi wake wote
tokea alipokuwa Jeshi hadi anaingia uongozi wa siasa alithibitisha
uaminifu wake kwa nchi yetu na uongozi wake.”
“Kufuatia msiba huu mkubwa, nakutumia wewe
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Tupa, salamu zangu za rambirambi, na
kupitia kwako naitumia salamu zangu za dhati kabisa familia ya marehemu,
wana-Mara na Wana-Serengeti wote ambako ndio kwanza alikuwa ameripoti
kuanza kazi yake ya ukuu wa wilaya hiyo,” amesema Mheshimiwa Rais
Kikwete na kuongeza:
“Napenda kuwajulisheni kuwa moyo wangu uko
nanyi katika kipindi hiki kigumu. Nawaombea uvumilivu na subira na
naungana nanyi kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweke pema
peponi roho ya Marehemu James Charles Yamungu. Amen.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
22 Agosti, 2012
0 comments:
Post a Comment