WAATHIRIKA wa ubakaji wasiopungua 70 wamekuwa wakipata matibabu katika kijiji kidogo cha Minova huko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo-DRC ambacho karibuni kilivamiwa na watu waliovalia sare za jeshi, kwa mujibu wa Umoja wa mataifa.
Jeshi la DRC lina kituo kikubwa huko Minova na linasema limewakamata wanajeshi kadhaa huko walioshukiwa kwa ubakaji na wizi wa ngawira.
Mji wa Minova upo katika jimbo la Kivu Kusini ni mahali ambapo makundi ya jeshi la Congo yalijikusanya tena baada ya kushindwa na waasi wa M23 katika mapigano yaliyotokea mwezi uliopita huko Goma.
Hali ya usalama huko Minova ilikuwa mbaya mwishoni mwa mwezi uliopita na iliripotiwa kwamba wanajeshi walilikimbia eneo na walifanya wizi wa ngawira wakati wanavuka katika mji huo.
Kamanda mpya wa majeshi ya nchi kavu ya DRC, Jenerali Francois Olenga, aliitisha mkutano wa maafisa waandamizi huko Minova wiki iliyopita ambapo alitaka heshima ya ufanyaji kazi mzuri na kufuata haki za binadamu.
Radio Okapi inayomilikiwa na Umoja wa Mataifa ilisema jeshi liliwatambua watu waliohusika kwa ubakaji na wizi huko Minova na washukiwa hao walikamatwa.
Waasi wa kundi la M23 na makundi mengine yenye silaha pia yanakabiliwa na shutuma za unyanyasaji mbaya wa haki za binadamu uliofanyika katika wiki za karibuni.
Serikali inalishutumu kundi la M23 kwa kuhusika na mauaji ya watu 64 katika muda wao mchache walioudhibiti mji wa Goma.
Umoja wa Mataifa unasema unachunguza ripoti 50 za ukiukaji mbaya wa haki za binadamu uliofanywa na kundi la M23 lilipoudhibiti mji huo.
0 comments:
Post a Comment