KATIBI MKUU TEF, NEVILLI MEENA.
JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF) limetoa maazimio matano yaliyojikita kuboresha tasnia ya habari nchini, huku likitangaza vita dhidi ya vyuo vya uandishi wa habari vya kati.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu TEF, Nevilli Meena alisema, maazimio yao yamejikita kwenye katiba na sheria za habari, utendaji wa vyombo vya habari, hali na mwelekeo wa uandishi na utangazaji kupitia redio na televisheni pamoja na wamiliki wa vyuo vya uandishi wa habari.
Alisema katika suala la Katiba na sheria za habari, TEF imesikitishwa na Katiba iliyopo sasa ya mwaka 1977, kutokuwa na kifungu au eneo lolote linalotamka uhuru wa vyombo vya habari.
Alisema pamoja na upungufu huo, TEF imeiomba Serikali kuweka ibara maalum itakayotoa uhuru wa vyombo vya habari katika Katiba mpya ijayo.
“Kwa kuzingatia maslahi ya tasnia ya habari na maendeleo ya nchi, Wahariri tunataka Katiba mpya ijayo iwe na kifungu kinachotoa haki ya kupata habari kwa wananchi wote, bila kubaguliwa wala kuwekewa vikwazo.
“Pia umefika wakati sasa Serikali ikubali kutunga sheria ya huduma kwa vyombo vya habari na kwa kauli moja tunasema tutashirikiana na Serikali kufanya kazi za weledi kwa maslahi ya taifa na watu wake,” alisema.
Katika suala la utendaji wa vyombo vya habari, alisema TEF imebaini kuwapo na kasoro ndani ya vyumba vya habari na kufafanua kuwa baadhi yao hutoa taarifa zinazotoa hukumu, kushtaki na kupendekeza adhabu.
Alisema si kazi ya vyombo vya habari kuhukumu jambo, bali vipaswa kutoa habari kwa uhalisia na ufasaha kwa kuzingatia pande zote husika.
Meena alisema, maazimio hao ya TEF yaliafikiwa katika mkutano wao uliofanyika Desemba 13-16,2012 mkoani Tanga.
Hata hivyo, suala la uandishi wa habari na utangazaji, TEF imesema imebaini kuwapo udhaifu mkubwa wa uandishi wa habari nyingi za magazeti ambazo hazikidhi vigezo sambamba na zile zinazotangazwa kwenye redio na televisheni.
Akizungumzia vyuo vya uandishi wa habari, Mwenyekiti wa TEF, Absalom Kibanda, alisema suala la utoaji elimu ya uandishi wa habari bado mitaala yake ina kasoro kadhaa.
Alisema kutokana na kasoro hizo, tayari mchakato wa kuandaa mtaala mmoja kwa vyuo vyote, umekamilika ikiwa lengo ni kuhakikisha elimu inayotolewa inazingatia matakwa na vigezo.
“Mtaala huo uliandaliwa baina ya Baraza la Elimu ya Ufundi (NACTE), Baraza la Habari Tanzania (MCT), wawakilishi wa vyuo vya uandishi wa habari.
“Sasa kuanzia Januari 2013, TEF tutasubiri miezi sita ipite na baada ya hapo tutafanya utafiti ili kubaini iwapo vyuo vyote vya uandishi vinatumia mtaala huo.
0 comments:
Post a Comment