KWA UFUPI
“CCM tuna wanachama zaidi ya milioni sita, hivyo tusipowafanya kuwa jeshi moja lenye mshikamano ni sawa na kazi bure. Mimi sikuwa kwenye chama muda mrefu tangu nimalize miaka yangu kumi nikiwa Katibu Mkuu wakati wa Rais mstaafu Benjamini Mkapa, hivyo sasa sijui kwa undani kama hakuna nidhamu na maadili ndani ya chama ila itajulikana huko mbele,”
Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara) Philip Mangula.
MAKAMU Mwenyekiti wa CCM (Bara) Philip Mangula, amemshukuru Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete kwa kuteua jina lake kwa ajili ya kushika wadhifa huo, na kuahidi kushughulikia nidhamu na maadili ndani ya chama ili kurudisha sifa na hadhi ya chama hicho kwa wananchi.
Akizungumza kwa nyakati tofauti na mamia ya wafuasi wa chama hicho waliompokea katika Miji ya Makambako na Njombe, Mangula alisema kama hakutakuwa na nidhamu na maadili ndani ya chama kwa kutekeleza mambo muhimu wanayokubaliana nayo nidhahiri amani ya nchi itapotea.
“CCM tuna wanachama zaidi ya milioni sita, hivyo tusipowafanya kuwa jeshi moja lenye mshikamano ni sawa na kazi bure.
Mimi sikuwa kwenye chama muda mrefu tangu nimalize miaka yangu kumi nikiwa Katibu Mkuu wakati wa Rais mstaafu Benjamini Mkapa, hivyo sasa sijui kwa undani kama hakuna nidhamu na maadili ndani ya chama ila itajulikana huko mbele,” alisema.
Alisema Serikali ya Tanzania ina chama kimoja kinachoshika dola, hivyo ni lazima kitekeleze ilani ya uchaguzi kwa kuwasimamia vyema watendaji wa Serikali, huku akiahidi kupambana na rushwa ndani ya chama hicho.
Mangula aliwataka Watanzania kuendelea kudumisha amani iliyopo kwa kuwa msingi wa maendeleo kwa taifa lolote duniani ni amani, na kwamba wananchi wanastahili kufuata taratibu, kanuni na sheria walizojiwekea ili amani iendelee kuwepo.
“Hakuna maendeleo ambayo yanaweza kupatikana nchini bila ya kuwa na amani, mimi ni shahidi wa nchi ambazo hazikuwa na amani hakuna maendeleo yaliyoweza kufanyika kwa wakati huo,” alisema.
Alitolea mfano vita vya kimbari vya Rwanda na Burundi mwaka 1994 pamoja na machafuko ya Zanzibar yaliyotokea mwaka 2000 wakati wa uchaguzi, kwa kusema kuwa hakuna shughuli za kimaendeleo zilizokuwa zikifanyika kwa wakati huo.
“Mimi nilibahatika kuwa Mkuu wa mkoa wa Kagera, ndiye niliyepokea wakimbizi laki saba wa Rwanda na Burundi, hivyo nayajua vyema matatizo yanayotokana na uvunjifu wa amani, pia machafuko ya Zanzibar yalipotokea shughuli za kiuchumi zilisimama,” alisema.
Mangula alivitaka vyama vya siasa nchini kuwa na uvumilivu na ukomavu wa kidemokrasia ili kulifanya taifa kuwa na umoja, kwa kufanya vikao halali bila kuvuruga amani.
0 comments:
Post a Comment