WAZIRI MKUU PINDA.
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda ameiagiza Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kumfukuza kazi Mkandarasi anayejenga bandari ndogo nne katika mwambao wa Ziwa Tanganyika, kwenye mikoa ya Rukwa, Kigoma na Katavi.
Pinda ametoa agizo hilo baada ya mkandarasi huyo, Kampuni ya Modspan Enter Limited ya jijini Dar es salaam kushindwa kuikamilisha kazi hiyo kwa zaidi ya miaka miwili sasa.
Mkandarasi huyo alishinda zabuni ya kujenga bandari ndogo za Kipili wilayani Nkasi (Rukwa) na Karema (Katavi) na Bandari za Lagosa na Sibwesa mkoani Kigoma zilizopo katika mwambao wa Ziwa Tanganyika zaidi ya miaka miwili iliyopita kwa kukosa uwezo wa kuimudu kazi hiyo.
Pinda alitoa agizo hilo juzi akiwa mjini Mpanda, baada ya kutaarifiwa na Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Dk Rajab Rutengwe kuwa mkoa huo hauna bandari ya kisasa katika mwambao wa Ziwa Tanganyika kwa ajili ya kupakia na kushusha abiria na mizigo.
Waziri Mkuu alielezwa pia kuwa pamoja na Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi kuanza kujenga bandari kijijini Karema, kwa sasa ujenzi umesimama baada ya mkandarasi kushindwa kuimudu kazi kwa kukosa uwezo na kwamba kama ingekamilika bandari hiyo ingefungua soko kubwa la bidhaa katika nchi jirani na kuvutia wawekezaji katika Ukanda wa Ziwa Tanganyika wenye Mikoa ya Kigoma, Rukwa na Katavi.
Kufuatia maelekezo hayo Pinda alishangazwa na kuhoji iweje mkandarasi mwenye uwezo huo mdogo ambaye ameshindwa kuimudu kazi hiyo ashinde tenda za kujenga bandari tatu za Kipili, Karema na Sibwesa katika mwambao mwa Ziwa Tanganyika.
Dk Rutengwe alisema kuwa hivi karibuni mkandarasi huyo alinaswa na vyombo vya dola akijiandaa kutorosha vyombo vyake vya ujenzi.
0 comments:
Post a Comment