RAIS Mohamed Mursi aungwa mkono na Wamisri katika duru ya kwanza ya kura
ya maoni juu ya katiba mpya ambayo anataraji itaitowa nchi hiyo kwenye
mzozo wakati wapinzani wakiipinga kwa kukandamiza haki za jamii ya
wachache.
Katika siku ya kwanza ya kura ya maoni juu ya rasimu ya sheria za
msingi za nchi hiyo asilimia 56.5 ya kura zimeikubali kwa kura ya ndio.
Duru ya pili ya kura hiyo ya maoni hapo Jumamosi ijayo yumkini ikapiga
kura nyengine ya ndio kutokana na maeneo mengi yanayotarajiwa kupiga
kura hiyo yana wafuasi wa itikadi kali za Kiislamu na hiyo ina maana
kwamba katiba hiyo itapita.
Lakini wakati kura ya hapana ikiwa ni
asilimia 43 jambo ambalo linaloonyesha kukaribiana kwa matokeo hayo
hakumpi faraja kubwa Mursi kutokana na mgawanyiko mkubwa katika nchi
ambapo anahitaji kuwa na muafaka kwa ajili ya kufanya mageuzi makubwa ya
kiuchumi.
Kura zikihesabiwa baada ya kumalizika zoezi la kura ya maoni mjini Cairo.
Muungano wa Ukombozi wa Taifa umesema hautotambuwa matokeo yoyote
yale yasiyo rasmi na utasubiri matokeo ya mwisho baada ya kura ya duru
ya pili.
Umetowa wito kwa wananchi wa Misri kuandamana barabarani hapo
Jumanne kutetea uhuru wao, kuzuwiya hujuma na kuikataa rasimu hiyo ya
katiba.Pia umesisitiza kwamba kura ya maoni ya hapo jana imegubikwa na
ukiukaji wa taratibu za kupiga kura.
Taratibu za kupiga kura zakiukwa
Mkuu wa muungano huo Mohamed El Baradei ambaye ni mkuu wa zamani wa
Shirika la Nishati ya Nuklea la Umoja wa Mataifa amesema kupitia mtandao
wa twitter kuhusu duru hiyo ya kwanza ya kura ya maoni kwamba nchi
imegawika.
Taratibu za kupiga kura zimekiukwa,watu wachache wamejitokeza
kupiga kura,hali ya kukatishwa tamaa na Waislamu wa itikadi kali imekuwa
ikizidi kuongezeka na hali ya kutojuwa kusoma na kuandika inaendelea
kuwa kikwazo nchini humo.
Makundi kadhaa ya kutetea haki za binaadamu na
yale yalioangalia kura hiyo yamesema kulikuwa na ukiukaji wa taratibu na
kutaka kura hiyo irudiwe.
Yamesema waangalizi waliondolewa kutoka baadhi
ya vituo vya kupigia kura, majaji hawakuwepo, mahala pengine
walionekana majaji wa bandia na kuna matukio ambapo wanawake walizuiliwa
kupiga kura.
Nchi inaweza kutumbukia kwenye udikteta
Waziri wa Masuala ya Maendeleo wa Ujerumani Dirk Niebel.
Wakati huo huo waziri wa masuala ya maendeleo wa Ujerumani Dirk
Niebel ameelezea wasi wasi wake juu ya hali hiyo ya Misri.
Amesema ana
hofu kwamba nchi hiyo chini ya Rais Mursi na Chama cha Udugu wa Kiislamu
inaweza kutumbukia kwenye udikteta. Ujerumani imepunguza mawasiliano na
serikali hiyo ya Misri na ule mpango wa msamaha wa madeni wa euro
milioni 240 kwa nchi hiyo umesitishwa kwa sasa.
Lakini wakati Misri
itakapokuwa na demokrasia na uhalali wa katiba Ujerumani itatowa msaada
wake kwa juhudi hizo.
Iwapo mchakato huo wa katiba utapita uchaguzi wa taifa unaweza
ukafanyika mapema mwakani jambo ambalo wengi wanatumai litaleta utulivu
ambao umekosekana nchini Misri tokea kuanguka kwa Hosni Mubarak takriban
miaka miwili iliopita.
0 comments:
Post a Comment