BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

ZITTO KABWE AWASHA MOTO MPYA CHADEMA, UAMUAZI WA KUGOMBEA URAIS UPO NDANI YA CHAMA.



MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), amevunja ukimya kuhusu hatima yake ya kisiasa ndani ya chama hicho. 

Amesema kwamba, hivi sasa ndani na nje ya Chadema kuna kundi la watu ambalo limekuwa likipika fitna na majungu ya kuwagombanisha viongozi wa chama hicho.

Kwa mujibu wa Zitto, kundi hilo limekuwa likifanya mradi huo kwa lengo la kutaka kutimiza maslahi yao binafsi kuliko kukisaidia chama.

Zitto, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, aliyasema hayo mjini hapa jana, alipokuwa akihutubia mamia ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Cine Atlas, Ujiji, mkoani Kigoma.

Pamoja na uwepo wa makundi hayo, alisema nia yake ya kugombea urais mwaka 2015 itabaki kuwa ndani ya Chadema na siyo chama kingine kama baadhi ya watu wanavyosema.

“Hakuna ugomvi ndani ya Chadema, bali kuna kupishana mitazamo na hili ni jambo la kawaida katika taasisi yoyote ya kisiasa inayoamini katika misingi ya utawala bora.

“Nataka kuwaambia kwamba hakuna migogoro Chadema, ila kuna watu wachache ambao wamekuwa wakiwagombanisha viongozi wa chama chetu. Binafsi sina ugomvi na mtu yeyote, ila kutokana na ubinafsi wa baadhi ya watu, watu hao wanakiweka chama katika taswira ambayo haijengi.

“Kama ni urais wa Zitto, Mungu akipenda utatokana na Chadema na hautatoka nje ya chama hiki. Kama kuna matatizo ya ndani ya chama, tutayamaliza na kama kuna jambo zito, nitarudi kwenu wananchi wangu ili mniambie ni nini cha kufanya.

“Katiba yetu imeweka misingi mizuri sana, hasa katika kutatua matatizo yetu na hii tutaitumia katika kuyamaliza, ingawa zipo juhudi za watu ambao wamekuwa wakipandikiza chuki.

“Leo Chadema ikipasuka kwa migogoro, nawaambieni wana Kigoma wenzangu, kwamba katu hakitatokea chama kingine cha upinzani chenye nguvu kwa muda wa miaka ishirini ijayo.

“Kama urais upo, basi utatoka ndani ya chama hiki nilichopo na siyo nje, hasa kwa kusukumwa na mipango ya Mungu,” alisema Zitto.

Akizungumzia maendeleo ya Mkoa wa Kigoma tangu upinzani ulipoingia, alisema hatua hiyo imekuja kutokana na wananchi wa mkoa huo kuyakubali mageuzi ya dhati.

Alisema kwamba, baada ya wananchi kuyakubali mabadiliko ya kisiasa, Serikali ya CCM ilihakikisha inafanya kila jitihada za kutaka kuwagawa wananchi wa mkoa huo, kwa kuwa iliamini ndiyo njia ya kuwafanya wakipende chama hicho.

“Upinzani ni asili ya Kigoma, ila ninataka kusema hata hawa wabunge wa NCCR-Mageuzi wote walikuwa ni vijana wa chama chetu. Lakini kutokana na ugomvi wetu wa kipuuzi, wakaona ni bora watafute ubunge kwa kukimbilia NCCR-Mageuzi.

“Hata hivyo, pamoja na Serikali kuifungua Kigoma kimaendeleo, hali hii imetokana na uwezo wetu wabunge wa mkoa huu bila kujali itikadi za vyama vyetu, kwani kila mara tumekuwa tukiwabana mawaziri kwa lengo la kuharakisha huduma za maendeleo katika mkoa wetu,” alisema.

Katika hatua nyingine, alitangaza mbele ya mkutano huo, kwamba atawalipia ada wanafunzi wote waliofaulu kwenda kidato cha kwanza katika shule za Serikali, hasa wa Kata ya Kagera, ambayo inaongozwa na Chadema.

“Niliahidi kwamba, kama kuna kata itafanya vizuri kwa kuwa na viongozi wote wa Chadema kuanzia mtaa hadi udiwani, nitatoa zawadi na leo hii ninatangaza kulipa ada kwa wanafunzi wote wa kata hii kwa mwaka mzima,” alisema Zitto na kushangiliwa.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: