Nembo ya Kanisa la Moravian.
KANISA la Moravian Jimbo la Kusini, limetangaza kuwafukuza kazi
wachungaji wake 14 na makatibu wanne wa idara mbalimbali kwa kosa la
kuchochea vurugu ndani ya kanisa hilo.
Uamuzi huo ulifikiwa jana na Halmashauri Kuu ya
Jimbo la Misheni Mashariki na Zanzibar baada ya wachungaji hao
kujitangazia halmashauri yao mpya, wakijitenga na uongozi ndani ya
kanisa.
Pamoja na kuwaondoa wachungaji hao, uongozi huo wa
jimbo, umefanya mabadiliko ya uongozi katika Wilaya ya Morogoro na
kuwateua wachungaji wengine kadhaa kuziba nafasi zilizoachwa wazi na
wachungaji waliofukuzwa.
Uamuzi huo umekuja wakati aliyekuwa Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Jimbo la Mashariki na Pwani ya Kanisa la Moravian
Tanzania, Clement Fumbo na wenzake saba wakiwa wamefungua kesi namba 222
Mahakama Kuu ya Tanzania, dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Kanisa la
Moravian Jimbo la Rungwe kupinga kuvuliwa madaraka na kusimamishwa kazi.
Katika kesi hiyo iliyopangwa kuendelea kusikilizwa
Februari 6, mwaka huu mbele ya Jaji Augustini Mwarija, Fumbo na wenzake
saba wanapinga kuondolewa madarakani na kusimamishwa kazi na wanaiomba
mahakama iamuru walipwe Sh500 milioni kama fidia na gharama ya kesi.
Kadhalika uamuzi wa kufukuzwa kwa wachungaji hao
umefanywa wakati Mchungaji Fumbo akidai kwamba yeye bado ni mwenyekiti
halali na kutangaza halmashauri yake mpya, jambo ambalo uongozi wa
Kanisa la Moravian unasema ni kinyume cha katiba wa kanisa hilo.
Akitoa taarifa ya hatua hiyo mbele ya waumini wa
kanisa hilo lililoko Ushirika wa Mabibo jijini Dar es Salaam, Katibu
Mkuu wa Jimbo la Misheni Mashariki na Zanzibar, Adolf Mwakanyamale,
aliwataja wachungaji waliofukuzwa kuwa ni pamoja na mwenyekiti wa Wilaya
ya Kaskazini, Alinanuswe Mwakilema.
Wengine na nyadhifa zao kwenye mabano ni Noel
Mwakalinga,(Mjumbe wa Halmshauri Kuu), Fanny Ndemange (Katibu wa Idara
ya Kina Mama), Angelina Mwamakula (Mchungaji Msaidizi Ushirika wa
Kimara) na Mariamu Kasendeka wa Ushirika wa Pugu Kajiungeni.
Wachungaji wengine na sharika zao kwenye mabano ni
Tumaini Mwakijale (Tanita) Mosted Kibona (Kitunda), Eliza Kipesile
(Kawe), Lugano Anganisye (Mwenge), Baraka Mwakijale (Mlandizi), Azaria
Lwaga (Segerea) na Fredy Mwakyusa wa Usharika wa Kiwalani.
Katibu huyo aliwataja wakuu wa idara wanne
waliofukuzwa kuwa ni Mchungaji Anyasime Kasebele (Uwakili), Emmanuel
Mwaijande (Kwaya), Hezron Mwangaja (Uinjilisti) na Silas Mwakibinga
(Miradi na Maendeleo).
“Tumeamua kuwaita pia wachungaji wetu wastaafu,
lengo likiwa ni kuziba mapengo yote yaliyotokana na ndugu zetu ambao
wameamua kuasi na kujitangazia kanisa lao,” alisema Mchungaji
Mwakanyamale.
0 comments:
Post a Comment