MATUKIO YA KISIASA NCHINI CHINA.
KIONGOZI mpya wa China, Xi Jinping, ameahidi kuongoza serikali safi na
yenye ufanisi zaidi na kupambana na ufisadi baada ya ubadilishanaji wa
madaraka kwenye taifa hilo la kikomunisti lenye nguvu kubwa kiuchumi
duniani.
Katika hotuba yake ya mwanzo baada ya kuchaguliwa, Xi amesema kwamba
atapigania "kuiinua upya hadhi ya taifa la China," na kutaka kuchukuliwa
kwa jitihada za makusudi na kubwa kabisa kuendeleza dhamira ya China
kuwa taifa kubwa kabisa duniani.
Uongozi mpya wa China, ambao unatarajiwa kuwa madarakani kwa kipindi cha
muongo mmoja kama ule uliotangulia, umesema kwamba utatilia mkazo
kwenye matumizi ya kijamii na hatua nyengine za kusambaza maendeleo kwa
upana zaidi kwa lengo la kupunguza pengo kati ya matajiri wachache na
masikini walio wengi nchini humo, na vile vile kupambana na ufisadi.
Nguvu za kijeshi
Waziri mpya wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi.
Wito huo wa kuipandisha hadhi ya China duniani umekuwa kauli
ya kawaida tangu Xi kuchukua nafasi za juu nchini China, ikiwemo ya ukuu
wa Chama cha Kikomunisti, uongozi wa jeshi na hii ya uongozi wa dola.
Ingawa hajaelezea undani wa namna China itakavyojiimarisha kilimwengu,
Xi ana mafungamano makubwa na jeshi la nchi hiyo na amekuwa akilihimiza
jeshi lijiimarishe ili "lishinde vita."
China iko kwenye mgogoro wa siku nyingi na Japan juu ya visiwa kwenye
Bahari ya Mashariki ya China na pia inalumbana na mataifa mengine jirani
juu ya udhibiti wa Bahari ya Kusini ya China.
Hotuba ya Xi ilizungumzia pia ufisadi, ambao aliuita kuwa ni kitisho kwa
Chama cha Kikomunisti na kuwataka wajumbe kupingana na tamaa na maisha
ya kifahari na badala yake wapambane na tabia ya ufisadi.
Bunge laidhinisha baraza jipya la mawaziri
Waziri Mkuu mpya wa China, Li Keqiang.
Kabla ya kukamilisha kikao chake siku ya Jumapili (17.03) ,
bunge hilo liliidhinisha uongozi mpya wa watu wanaoonekana kuwa wasomi,
wengi wao wakiwa na uzoefu mkubwa kwenye siasa za kimataifa, ambao
wanaunda baraza la mawaziri lililopewa jukumu la kuuinua uchumi
unaozorota na kuijengea China hadhi kubwa ulimwenguni.
Miongoni mwa mawaziri muhimu kwenye baraza hilo jipya ni wale wa fedha,
biashara na mambo ya kigeni, ambapo balozi wa zamani nchini Japan, Wang
Yi, ametangazwa kuwa waziri mpya wa mambo ya kigeni.
Mawaziri wengine wapya ni pamoja na Lou Jiwei, ambaye anakuwa waziri
fedha, akitokea kwenye uongozi wa taasisi maalum uwekezaji kwa mashirika
ya umma.
Waziri Mkuu aigeukia Marekani
Katika kile kinachoonekana kama hatua za mwanzo kukabiliana na mataifa
ya nje, Waziri Mkuu mpya Li Keqiang, amekanusha vikali tuhuma za
Marekani kwamba China inashiriki kwenye udokozi wa mitandao ya Marekani,
akisema kwamba serikali yake haiungi mkono ujasusi kwenye mitandao.
Kauli ya Li imekuja baada ya Rais Barack Obama wa Marekani kuingilia
kati kulizungumzia suala hilo, ambalo kwa siku kadhaa limekuwa
likizungumzwa na maafisa wa ngazi za juu wa Marekani.
"China yenyewe ni muathirika wa mashambulizi ya mitandaoni," alisema Li
baada ya mkutano wa bunge.
"Nadhani hatupaswi kutoa tuhuma zisizo na
msingi wowote dhidi ya wengine na badala yake tunapaswa kujitahidi
kufanya yale yatakayochangia kwenye usalama wa mitandao."
Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
0 comments:
Post a Comment