BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

CCM KITANZINI

 YATUHUMIWA KUASISI UDINI, SASA WAUTAFUNA, WABUNGE WAKE WAHOFIA AHADI ZA RAIS KIKWETE, TOFAUTI KATI YA MASIKINI NA MATAJIRI WAIWEKA NJIA PANDA.
 http://www.mtanzania.co.tzKATIBU MKUU CCM, ABDULRAHAMAN KINANA 

SAKATA la udini sasa limechukua sura mpya, baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kushikwa pabaya, kikitajwa kuwa ndio chanzo cha matukio yote ya sasa, MTANZANIA Jumatano linaripoti.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanadai kuwa ushahidi wa kihistoria na kimazingira unaonyesha wazi kwamba CCM kimehusika katika kuasisi suala la udini, ambalo sasa limeanza si tu kulitafuna taifa, bali hata chenyewe, baada ya siku za hivi karibuni kuibuka matukio ambayo hayajawahi kutokea katika historia ya nchi hii.


Katika chaguzi kuu zilizopita, CCM kinatuhumiwa kupanda mbegu za udini kikitumia propaganda hiyo kuvimaliza vyama vya upinzani, ambavyo vilikuwa vikionekana kuwa tishio dhidi yake.



Wafuatiliaji wa masuala mbalimbali wanadai kuwa matukio ya sasa ni matokeo ya propaganda hiyo ya udini, iliyofanikisha kwa kiwango kikubwa mpango wa kukimaliza Chama Cha Wananchi (CUF) mwaka 2005, baada ya kuonekana kuwa tishio kwake.

Hata hivyo, inadaiwa kuwa CCM ilitumia hoja hiyo baada ya kile kinachodaiwa kuwa CUF nao wamekuwa wakitumia udini kama silaha yao ya kujipatia wapiga kura katika chaguzi mbalimbali.

Inadaiwa kuwa sumu hiyo iliyomwagwa na timu ya makada wa CCM waliokuwa wakimtafutia urais Jakaya Kikwete kwa vipindi viwili tofauti mwaka 2005 wakati akiomba kura kwa mara ya kwanza na mwaka 2010, ndiyo ambayo sasa inaitafuna serikali ya chama chake.

Wakati Rais Kikwete katika hotuba yake ya hivi karibuni akikiri kwamba hali ya mpasuko wa kidini inayotokea hivi sasa haijawahi kufikiwa katika historia ya nchi hii, kiini chake pia ni mwaka 2010, ambako chama chake kilidaiwa kumtafutia kura kwa kuendeleza propaganda za udini, kikikituhumu Chadema kuwa ni chama cha Wakristo na kwamba mgombea wake, Dk. Willbrod Slaa alikuwa ametumwa na maaskofu kugombea urais.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanadai kuwa, CCM kilitumia udhaifu wa Chadema ambacho nacho kilidaiwa kutumia turufu ya dini kujinadi katika baadhi ya maeneo.

Hata hivyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Azaveli Lwaitama, anasema karata ya kuibua vuguvugu la chuki za kidini limesababishwa na viongozi wachache wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Dk. Lwaitama anasema chuki za kidini zilianza kuibuka mwishoni mwa mwaka 2009 na ilipofika 2010, hali hiyo ikajidhihirisha wazi.

“Kuna viongozi wachache wa chama tawala ambao walianzisha hili na wala wasilikwepe, waache liwaumbue, hakuna ubishi, si unajua mambo haya hayachelewi kumuumbua mtu….wao ndio walianzisha jambo hili katika uchaguzi uliopita, kwa hiyo wasitafute mtu wa kumtupia lawama,” alisema Dk. Lwaitama.

Kuibuka kwa chokochoko hizo za kidini, ambazo sasa zinaelekea kuota mizizi, kumeelezwa kuwa tishio kwa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi, baada ya jambo hilo sasa kuonekana likikizidi nguvu.

Ofisa mmoja mwandamizi wa Serikali aliyekaribu na vyombo vya dola, ameliambia MTANZANIA Jumatano kuwa hivi sasa suala hilo la udini linaiumiza kichwa Serikali ya CCM, hasa baada ya kudhihirika kwamba jambo hilo pia limechochewa na pengo kati ya walionacho na wasionacho.

Kwamba tofauti kati ya masikini na matajiri imekuwa kubwa kiasi cha upande fulani sasa kuanza kuhisi wakionewa.

Jambo hilo pia linaungwa mkono na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ali, ambaye anasema viongozi wa Serikali wasitumie ajenda ya udini kuondoa fikra za wananchi kwenye ukweli.

Bashiru anasema suala la chuki za udini ni dogo sana nchini, Serikali inatakiwa ijibu hoja za kuibuka kwa utofauti mkubwa wa watu walionacho na wasionacho.

Anasema kuwapo kwa daraja hilo kumeibua mpasuko mkubwa katika jamii, ambapo watu wasiokuwa nacho ni wengi kuliko walionacho na hivyo ni rahisi kwa wale masikini kutumiwa vibaya katika kusababisha migogoro.

“Enzi za Baba wa Taifa tulikuwa tunapigana na maadui watatu, ambao ni ubepari, ukabaila na ubeberu, lakini maisha ya leo jitihada hizo ziko wapi?” alihoji msomi huyo.

Kauli aliyoitoa hivi karibuni Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, kuwa viongozi wa kizazi kipya wamesahau misingi iliyoachwa na marehemu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, pia inaungwa mkono na Mhadhiri huyo.

Bashiru anasema viongozi wamesahau misingi aliyoiacha Baba wa Taifa, akitolea mfano utekelezaji wa azimio la Arusha na hivyo kuwataka viongozi wa serikali wasikimbilie hoja ya udini kujitetea, huku kukiwa na sababu kubwa inayosababisha jamii kuchukiana.

Kauli hiyo ya Mkapa pia imetafsiriwa na baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa kuwa kiongozi huyo ameonyesha wazi kwamba hakubaliani na mwenendo wa CCM na serikali yake katika suala zima la kushughulikia udini.

Wakati hayo yakitokea, tayari Rais Kikwete ameshitukia uzito wa jambo hilo, akitumia sehemu ya hotuba yake ya mwisho wa mwezi uliopita kuwasihi viongozi wa dini, serikali kukemea suala hilo kwa uzito unaostahili.

Mbali na Rais Kikwete kushituka, chama chake, CCM nacho kupitia Kamati Kuu yake (CC), kinatarajia kukutana mjini Dodoma hivi karibuni kwa ajili ya kujadili suala hilo.

Mmoja wa viongozi wa chama hicho aliliambia gazeti hili kuwa Kamati Kuu ya chama hicho imeamua kukutana kuzungumzia suala hilo, baada ya kuona sasa linatishia mustakabali wa chama na taifa kwa ujumla.

Wakati suala la udini likikiweka CCM katika wakati mgumu, ahadi mbalimbali zilizopata kutolewa na Rais Kikwete wakati akiomba kura mwaka 2010, nazo zimeonekana kuwa mwiba mkali kwa serikali ya chama chake.

Tayari ahadi hizo kwa vipindi tofauti zimezua mzozo Bungeni, baada ya baadhi ya wabunge, wakiwemo wa chama chake kuhofia utekelezaji wake.

Hali hiyo ilitokea tena jana bungeni mjini Dodoma, baada ya Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), kuitaka Serikali ipeleke bungeni orodha ya ahadi zote za Rais Kikwete za ujenzi wa barabara, ili wabunge waweze kujiridhisha kama kweli zinatekelezeka.

Hoja kama hiyo iliwahi kuibuliwa na Mbunge wa Buhambwe, Felix Mkosamali (NCCR- Mageuzi), katika Mkutano wa Bunge uliopita, akihoji utekelezaji wa ahadi ya Rais Kikwete ya kujenga Barabara ya Nyakanazi-Kibondo-Kigoma katika kiwango cha lami.

Jana akiuliza swali Bungeni, Lugola alisema ahadi hizo za Rais zimekuwa kama madeni ambayo yameelekezwa kwa wabunge wa majimbo husika.

“Lini Serikali italeta orodha ya madeni hayo hapa bungeni ili wabunge wajiridhishe kama kweli yanalipika kwa kuwa wabunge wanaendelea kudaiwa?” alihoji.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Agrey Mwanri, alisema suala la ahadi za Rais halina mjadala kwa kuwa lazima zitekelezwe.

Alisema orodha ya ahadi zote za Rais ilishaandaliwa na ofisi ya TAMISEMI na kwamba lazima ahadi zote hizo zitekelezwe kulingana na upatikanaji wa fedha.

Awali Mbunge wa Moshi Vijijini, Cyril Chami (CCM), alihoji ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Rais ya kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami.

Akijibu swali la msingi la Mwanri, alisema Halmashauri ya Wilaya ya Moshi imeshauriwa kuandaa maombi maalumu kwa ajili ya ujenzi wa Barabara ya Old Moshi kwa kiwango cha lami.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: