BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MUACHE DK SLAA-KADA CCM

ADAI NCHEMBA, WASIRA WANAHARIBU CHAMA.
http://www.freemedia.co.tzMwigulu Nchemba

VIONGOZI waandamizi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira, na Naibu Katibu Mkuu (Tanzania Bara), Mwigulu Nchemba, wameaswa kuacha siasa za kueneza chuki kwa CHADEMA na Katibu wake, Dk. Willibrod Slaa.

Badala yake wametakiwa kunadi sera na ilani ya uchaguzi ya CCM ili wananchi wajue serikali ya chama chao inafanya nini katika kutekeleza kile ilichowaahidi mwaka 2010.

Rai hiyo ilitolewa jana na kada wa CCM mkoani Morogoro, David Mgesi, katika mahojiano maalumu na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam.

Mgesi ambaye alikuwa Mwenyekiti wa CHADEMA mkoani Morogoro kabla ya kujiunga CCM mwaka 2005, alisema kuwa anasikitishwa kuona Mwenyekiti wao, Rais Jakaya Kikwete, akiwafumbia macho Wasira na Nchemba wakati wakiendelea kukiua chama.

Hata hivyo, Wasira alipotafutwa kujibu tuhuma hizo alizungumza kwa kifupi akitaka kujua nani amesema na alipotajiwa alisema, “Hayo ni maoni yake.”

Wasira alipoulizwa kama ni kweli anatumia mgongo wa CHADEMA kujitafutia umaarufu wa kupitishwa na CCM kuwania urais 2015 alijibu: 

“Kama ungekuwa unaandika kwa Kiingereza ungeweza kusema ni ‘rubbish’, mimi niko huku jimboni hata sasa nakagua shughuli za maendeleo.”
Kuhusu Nchemba, yeye simu zake zilikuwa hazipatikani muda wote.

Katika madai yake Mgesi alisema, “Kila wanaposimama kuzungumza iwe jukwaani au kwenye vyombo vya habari propaganda yao ni moja ya kuitukana CHADEMA na Dk. Slaa kana kwamba CCM haina ajenda wala ilani.”

“Wasira na Nchemba wamekuwa viongozi wa kueneza matusi, chuki kuhusu CHADEMA wala hawana hoja lakini wameachwa waendelee kukiua chama,” alisema.

Kada huyo ambaye alitamba kuwa yuko radhi kusulubiwa hata ikiwa ni kutobolewa macho, alidai kwamba viongozi wengi wa CCM wamekuwa na tabia ya kutotaka kukosolewa, kama walivyo Wasira na Nchemba ambao wanaendeleza chuki kwa kila anayewakosoa.

“Waache kumwandamna Dk. Slaa bali CCM itafute mgombea makini atakayekuwa na vigezo vya kupambanisha naye katika uchaguzi mkuu ujao.”

“Hawa wote wanaojitapa na kupigiwa debe ndani ya CCM ili kugombe urais, hakuna mwenye sifa za kulinganishwa na Dk. Slaa. 

Sasa badala ya sisi kujipanga kwenye chama kumtafuta mtu asiye fisadi, tunajadili propaganda za uzushi kwa CHADEMA,” alisema.

Mgesi alifafanua kuwa wananchi wa sasa wamebadilika na kwamba hawawezi kuelezwa uongo kila wakati wakaukubali, hivyo salama ya CCM ni kuwaeleza imefanya nini badala ya kueneza propaganda za chuki kama wanavyofanya viongozi wake.

“Hata ukiwatisha wananchi kwa kuwanyofoa kucha, kuwang’oa meno na kuwatoboa macho wale wanaojitokeza kusema ukweli wa kukosoa bado haisaidi isipokuwa ni kuukubali ukweli na kujipanga.”

“Mimi kama kada mtiifu wa CCM sijaona mtu wa kumkabili Dk. Slaa kati ya wale wanaojitokeza kuutamani urais. Chaguzi zetu zimejaa rushwa sasa unategemea kwa staili hiyo mtu muadilifu kama huyo utampataje?” alihoji Mgesi.

Kada huyo aliongeza kuwa aliondoka CHADEMA na kujiunga CCM akiwa na matumaini kuwa Kikwete ni muumini wa sera ya ujamaa, hivyo angeweza kurejesha misingi ya Azimio la Arusha.

“Matumaini yangu yalikuwa kinyume, wala hakuna tena ujamaa lakini ninachopigania sasa ni utetezi wa watu hasa wanyonge. Nitaendelea kuwa ndani ya CCM na anayekataa ukweli huu aje nitamuelimisha,” alitamba.

Kuhusu CCM kushughulikia kero za wananchi, Mgesi alidai viongozi wengi ni wabinafsi na ndiyo maana wameshindwa kumsaidia Rais Kikwete.

Alitolea mfano mamilioni ya fedha za wananchi zilizopotea katika upatu wa DECI akidai viongozi wakuu wengi wa serikali walishiriki katika kuhamasisha biashara hiyo haramu.

“Mathalani mkoani kwangu tawi la DECI lilikuwa katika ofisi za CCM na aliyelifungua ni aliyekuwa Mkuu wa Mkoa, Saidi Kalembo, akiwaagiza watumishi wote wa ofisi yake kuhakikisha wanapanda mbegu.

“Kilosa tawi lilifunguliwa na aliyekuwa Waziri wa Fedha, Mustafa Mkullo. Hawa ndiyo viongozi wa serikali na CCM. 

Nilipohoji ufisadi huu wakadai kuwa mimi bado nina Uchadema. Hapa tunawezaje kuwakomboa wanyonge,?” alihoji.

Mgesi aliongeza kuwa hali hiyo iko hivyo hata kwenye ardhi, kwamba wananchi wa wilaya ya Kilosa wameporwa ardhi yao na viongozi kwa mgongo wa wafugaji na hivyo kuibua mgogoro mkubwa baina ya jamii za wakulima na wafugaji.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: