BAADHI ya wasomi nchini wamesema kwamba licha ya hatua iliyochukuliwa na Rais Jakaya Kikwete kutengua uteuzi wa mawaziri wanne, kugusa mustakabali wa kuwania urais wa miongoni mwa wanasiasa hao katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, wanaweza kuwania nafasi hiyo kwa kuwa waliwajibika kisiasa.
Mawaziri walioenguliwa kutokana na athari za
Operesheni Tokomeza Ujangili ni wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel
Nchimbi, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David, Ulinzi na Jeshi
la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa Maliasili na Utalii,
Balozi Khamis Kagasheki.
Wakati Nchimbi akitajwa kuwa mmoja wa wanasiasa
tishio katika mbio za kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu ujao, Nahodha
anatajwa kuwa mmoja wa wale watakoingia katika kinyang’anyiro cha nafasi
hiyo upande wa Zanzibar lakini baada ya Dk Shein kumaliza muda wake wa
vipindi viwili.
Katika msingi huo, gazeti hili liliarifiwa kuwa
baada ya tangazo la kutenguliwa kwa uwaziri wao, baadhi ya kambi
zinazojiwinda kwa ajili ya kuwania nafasi za juu za uongozi wa nchi
2015, zilishangilia na kuandaa tafrija za kupongezana.
Kumekuwa na mawazo kwamba ikiwa Nchimbi na Nahodha
wanataka kuendelea na mipango yao, basi inabidi wafanye kazi kubwa
kwani kuondolewa kwao katika nafasi za uwaziri ni kete itakayotumiwa na
wapinzani wao kisiasa.
Hata hivyo, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa katika
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Emmanuel Mallya alisema kung’oka
kwa mawaziri hao kunaweza kusiyumbishe ndoto zao kisiasa siku za usoni.
“Inategemea wanazipangaje karata zao na tukumbuke
kwamba bado Rais anaweza kuwateua kwenye nafasi nyingine ijapokuwa ni
kweli kwamba kuenguliwa huku kutawayumbisha katika matamanio yao ya
baadaye kisiasa,” alisema Mallya na kuongeza:
“Dk Nchimbi na Nahodha siyo kwamba walikuwa tishio
kubwa kati ya wanaotajwa kuwania urais, ingawaje ni watu wenye mikakati
mingi na wako kwenye makundi mazuri yanayowaunga mkono. Itategemea
jinsi wanavyojipanga upya.”
Mtazamo wa Mallya unaungwa mkono na Profesa wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Gaudence Mpangala ambaye anasema kimsingi
matatizo yaliyotokea yanasababishwa si na watu binafsi, bali mfumo
mbovu. Profesa Mpangala alisema hakuna waziri anayeweza kufanikiwa
kiutendaji katika mfumo mbovu uliopo na unaoendelea kutumika.
Alisema haoni kama mawaziri hao wameathirika
kisiasa kwani wameathiriwa na mazingira wanayofanyia kazi. “Yaliyotokea
kwenye operesheni ya ujangili ni kielelezo cha mfumo wa ubabe
uliokithiri muda mrefu,” alisema Profesa Mpangala.
Nchimbi ni nani?
Nchimbi, ambaye ni Mbunge wa Songea Mjini ni kati
ya wanasiasa waliokuwa wanatajwa kuwania nafasi ya urais kutokana na
historia na rekodi yake ndani ya Serikali na CCM huku nafasi nyeti
alizoshika katika miaka ya karibuni zikimwongezea sifa. MWANANCHI.
0 comments:
Post a Comment