BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

TFF YAMKAMATA MWESIGWA KUWA KATIBU MKUU MPYA, SHAFII DAUDA NA WAMBURA WAPATA NAFASI KATIKA SHIRIKISHO HILO.


Rais wa TFF, Jamal Malinzi

Na Baraka Mpenja
SHIRIKISHO la soka Tanzania (TFF) limemuajiri Katibu Mkuu wa zamani wa Yanga, Selestin Mwesigwa kuwa Katibu Mkuu mpya wa shirikisho hilo.


Rais wa TFF, Jamal Malinzi amesema kuwa, Mwesigwa alizaliwa mwaka 1970, ana digrii ya masuala ya kimataifa kutoka Chuo Cikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na diploma ya mafunzo ya sheria.


Malinzi aliongeza kuwa Mwesigwa amefanya kozi kadhaa za masuala ya utawala ndani na nje ya nchi zikiwemo kozi za utawala wa mpira zilizotolewa na FIFA.


Rais huyo alisema ajira yake ya mwisho ya Mwesigwa ilikuwa Ukatibu Mkuu wa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam, hivyo ana uzoefu mkubwa wa masuala ya uongozi ikizingatiwa amefanya kazi katika mashirika mbalimbali ikiwemo shirika la Plan International.



Aidha, Malinzi alisisitiza kuwa Mwesigwa alipokuwa Katibu Mkuu wa Yanga alishiriki kikamilifu katika mchakato wa kuanzisha Bodi ya Ligi kuu na ule wa Yanga kuingia udhamini na kampuni ya bia ya TBL, hivyo amekidhi vigezo vya kushika wadhifa huo mkubwa ndani ya TFF.



TFF pia imemuajiri katibu wa Simba SC, Wakili Evodius Mtawala kuwa Mkurugenzi wa Vyama na Masuala ya Kisheria ya TFF.


Rais Malinzi alisema Mtawala ana Shahada ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Shahada ya Uzamili ya uongozi wa Biashara ya Chuo Kikuu cha ESAMI.


Rais aliongeza kuwa Mtawala ambaye ajira yake ya mwisho ilikuwa Ukatibu Mkuu wa Simba SC, Klabu mwanachama wa TFF, ana uzoefu ambao utasaidia sana kukabili changamoto mbalimbali za vyama wanachama wa TFF.


Aidha Rais alisema uzoefu wake na ujuzi wa masuala ya sheria utasaidia kutatua masuala mbalimbali ya kisheria na kikatiba ndani ya shirikisho hilo.


Nafasi ya Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF imeachwa wazi kufuatia waombaji wote walioomba wa ndani na nje ya nchi kutokidhi vigezo, hivyo kamati ya utendaji imeagiza nafasi hii itangazwe upya na wale walioomba mara ya kwanza wasiombe tena.

Rais Malinzi alisema Idd Mshangama atakaimu nafasi hii kwa sasa mpaka mtu mwingine atakapopatikana.


Pia nafasi ya Mkurugenzi wa ufundi imebaki wazi baada ya waombaji wote kutokidhi vigezo, hivyo, Salum Madadi atakaimu nafasi hiyo na Rais Malinzi ameagiza itangazwe tena na walioomba wasiombe tena.


Nafasi nyingine iliyobaki wazi ni Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, hivyo itatangazwa tena na kwa sasa, Danny Msangi atakuwa ana Kaimu.


Afisa Habari wa TFF ataendelea kuwa Boniface Wambura Mgoyo. Rais Malinzi alisema ajira zote zitaanza rasmi Januari Mosi mwakani na anawatakia kazi njema, huku akiwa na imani kubwa kuwa watasukuma mbele gurudumu la maendeleo ya mpira wa miguu.

Katika hatua nyingine, TFF imeteua wajumbe wa kamati ya uchaguzi na kamati ya Rufani ya Uchaguzi na kamati ya soka la ufukweni.




Kamati ya uchaguzi inaundwa na Mwenyekiti, Wakili Melchesedek Lutema, Makamu wake, Wakili Walter Chipeta na Wajumbe Hamidu Mahmoud Omar, Jeremiah John Wambura na Hassan Dalali.

Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya TFF itakuwa chini ya Mwenyekiti , Wakili Julius Lugaziya, Makamu wake, Wakili Mwita Mwaisaka na Wajumbe Juma Abeid Khamis, Rashid Dilunga na Masoud Issangu.

Na kamati ya Soka la Ufukweni itakuwa chini ya Mwenyekiti Ahmed Mgoyi, Makamu Mwenyekiti, Shafii Dauda na Wajumbe Deo Lucas, Juma Mgunda, Boniphace Pawasa, Joseph Kanakamfumu na John Mwansasu. (Chanzo:fullshangweblog).
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: