AIBU YAIKUMBA WILAYA YA MOSHI KATIKA SHULE YA MSINGI.
Mwanafunzi wa shule ya msingi Ghona akionyesha choo cha shule ya jirani wanachokitumia, ambacho nacho pia kimejaa. Picha na Rehema Matowo.
Kilimanjaro ya zamani sio ya sasa. Ile sifa ya mkoa huo kinara wa elimu nchini ilishaporomoka siku nyingi.
Zamani ilikuwa ni jambo la ajabu kusikia kuwa kuna shule katika mkoa huo ikikabiliwa na changamoto zinazoepukika kama vile ukosefu wa madawati, vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo na walimu.
Hata hivyo, Kilimanjaro ya leo hasa wilaya maarufu ya Moshi ina shule ambazo wasimamizi wake wameshindwa kujenga hata miundombinu ya vyoo.
Angalau basi ingekuwa shule moja, la hasha! Ni shule kadhaa ambazo kwa hali ilivyokuwa tete, wanafunzi na walimu wanalazimika kujisitiri porini au katika nyumba za jirani na shule zao.
Wakati tatizo la ukosefu wa matundu ya vyoo likishtadi hasa katika shule za msingi za Ghona, Makame juu, Mabirang’a na Sagana, viongozi, wazazi na jamii kwa jumla wanarushiana mpira kuhusu ufumbuzi wa kadhia hiyo inayoitia doa wilaya ya Moshi.
Hali halisi
Shule ya Msingi Saghana iliyoanza mwaka 2005 haijawahi kuwa na choo kabisa hali inayowalazimu walimu pamoja na wanafunzi kujisasaidia vichakani au katika vyoo vya nyumba zilizopo jirani na shule.
Mwenyekiti wa kamati ya shule hiyo, Haruni Msuya, anakiri kuwa hiyo ni fedheha kwa walimu na wanafunzi, lakini anaitupia mzigo serikali kwa kukubali kuisajili shule hiyo ikiwa haina choo.
“Mwandishi hata sisi hatufurahi shule yetu kutokuwa na choo. Ni aibu kwetu lakini kama unavyoona wazazi walichangia shule ikajengwa na sasa hali ya maisha imekuwa ngumu ukimwambia mzazi achangie kunakuwa na mvutano,’’ anasema.
Anasema kinachokwaza maendeleo shuleni hapo ikiwamo ujenzi wa choo, ni baadhi ya wanasiasa kuingilia miradi ya maendeleo wakiwaeleza wananchi kuwa ujenzi ni jukumu la serikali.
“Hapa tunajitahidi kuwaelimisha wazazi kuhusu umuhimu wa kuchangia elimu, lakini wanasiasa nao wanapita wakiwaambia wazazi msichangie… inakuwa nivute nikuvute na ndio maana elimu hapa haiendelei anaeleza Msuya.
Kwa upande wake, Diwani wa kata ya Makuyuni ilipo shule hiyo, Mangachi Mrema anasema jitihada za ujenzi za wa choo kipya zinafanyika na sasa wameanza na uchimbaji wa shimo.
Katika Shule ya Msingi Ghona, wanafunzi wanalazimika kujisaidia vichakani huku wengine wakijisaidia katika shule jirani ya Mabiranga ambayo nayo haina matundu ya kutosha. Shule hiyo ina matundu nane tu yanayotumiwa na wanafunzi 720 wakiwamo wa shule jirani ya Ghona.
Kwa mujibu wa taratibu za kielimu kama zinavyoainishwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, tundu moja la choo linapaswa kutumiwa na wanafunzi 25 ambao ni wa kiume. Kwa wanafunzi wa kike tundu moja linatumiwa na wanafunzi 20.
Kwa takwimu hizi, ni dhahiri kuwa hivi sasa katika shule ya msingi Mabiranga inayowasitiri pia wanafunzi wa shule jirani, tundu moja la choo linatumiwa na wanafunzi 90 kiwango ambacho ni zaidi ya mara tatu ya utaratibu wa wizara.
Mwenyekiti wa kamati ya shule ya Ghona, Seph Ngate, anasema shule hiyo haina choo tangu mwaka 2010, kufuatia choo kilichokuwepo kusombwa na mafuriko.
Anaeleza kuwa pamoja na wazazi kuchangia ujenzi mpya wa choo, haukukamilika baada ya choo kuporomoka kwa sababu ya kujengwa chini ya kiwango.
“ Kitendo cha choo kuporomoka kabla ya kukamilika kimewakatisha tamaa wazazi na kukataa kuendelea kuchangia ujenzi wa choo na hivyo kusababisha wanafunzi kujisaidia vichakani na wengine katika shule jirani,’’ anasema.
Diwani wa kata ya Kahe Mashariki, Idd Mchomvu, anakiri shule ya Ghona kutumia choo kimoja na shule ya mabirang’a lakini akasema changamoto kubwa ni wazazi kutokuwa na mwamko wa kuchangia.
Anasema hali duni ya maisha inayowakabili wananchi wa kata hiyo imesababisha michango kutochangwa kwa wakati.
Mchomvu anasema tayari wameanza mchakato wa ujenzi wa choo ili kuwanusuru wanafunzi na magonjwa ya mlipuko. Anasema tayari wameshapewa Sh 1 milioni kama hamasa ya haramabee ya ujenzi huo.
Shule nyingine ni Makame juu ambayo wanafunzi wanalazimika kujisaidia kwenye mashamba ya migomba kufuatia choo chao kujaa
Serikali inasemaje?
Ofisa Elimu wilaya ya Moshi, Simon Sheshe, anakiri shule nyingi kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa madawati, vyoo na miundombinu ya madarasa pamoja na walimu.
Anasema fedha zinazotengwa na serikali kwenye sekta ya elimu ni kidogo hivyo hazitoshi kugawanywa katika kila shule.
Ukiondoa kutumia kiasi kidogo wanachotumiwa na serikali, ofisa huyo anawashukia wazazi kwa kuwa na mwamko mdogo wa kuchangia miradi ya elimu wakiamini hilo ni jukumu la serikali.
“Watu huku hawana mwamko wa kuchangia elimu, wanasubiri kufanyiwa kila jambo hata ukiwahamasisha wachangie hawako tayari. Wao wanaamini hiyo ni kazi ya serikali tu,” anabainisha.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment